JAMBO MUHIMU LA KULIJUA UNAPOANZISHA MAHUSIANO YA KIMAPENZI NA MTU

Na ramadhani Masenga

WEWE na mpenzi wako kila mmoja ana malezi na historia yake. Kutokana na vitu hivyo, kila mmoja ana mtazamo, tabia na itikadi zake. Kutokana na utofauti huu, umakini na busara kubwa sana inahitajika ili mahusiano yenu yaweze kuwa na furaha, raha na amani.

Utofauti wa tabia umefanya watu wengi watafsiriane tofauti hali inayopelekea kuachana ilhali wakiwa bado wanapendana.

Kabla hujatoa hukumu yoyote kwa mwenzako, jiulize unamjua kwa kiasi gani? Familia yake unaijua kwa kiwango kipi, yeye kapata malezi ya namna gani katika familia yao?

Malezi anayopata mtu yana mchango mkubwa katika tabia yake. Sasa kuna wakati anaweza kukufanyia matendo fulani, wewe ukadhani anakufanyia makusudi kumbe ni athari ya malezi aliyopata kwao. Uimara wa mahusiano unahitaji busara. Kabla ya kutoa hukumu ya haraka, inabidi umfikirie mwenzako na kutafuta njia bora ya kumbadilisha.

Wapo wengine kutokana na kulelewa na wazazi wenye kupenda fujo, kujibizana hovyo na wao wamekuwa hivyo. Unaweza kuwa unaoangea naye kwa heshima na ustaarabu ila ukashangaa anaanza kukujibu kwa ovyo na ufedhuli. Usikimbilie kuachana. Tafuta wataalamu wa masuala ya saikolojia na ushauri ili wakwambie nini cha kufanya.

Wapo watu wengi waliokuwa na watu wa ovyo na kuna wakati walitamani kuachana nao, ila baada ya kupata msaada wa kitaalamu wamejikuta wakiwa na maisha mazuri, ya furaha na amani.

Katika uhusiano kuachana kunatakiwa kuwa suala la mwisho kabisa kufikiria. Utofauti wa tabia na mitazamo baina yenu unaweza kubadilishika kukiwa na upendo na jitihada.

Hata unapoona watu wakiwa katika uhusiano kwa muda mrefu, usidhani mwanzo wa mahusiano kulikuwa na mteremko na walikuwa wakiridhishana kwa kila kitu. Hapana. Wengi wamepitia changamoto sana mwanzo wa uhusiano wao, ila uvumilivu, hekima na busara katika maamuzi umewafanya kufikia hapo walipo leo.

Baada ya kuingia katika ndoa yafaa ufahamu umeingia katika mechi kamili baada ya kutoka katika urafiki wa mapenzi na uchumba ambao kimsingi ilikuwa kama michezo ya majaribio. Kuna kazi zaidi katika ndoa kuliko hatua nyingine ulizotoka. Kwa kulijua hili yafaa ujizatiti zaidi.

Kuishi na mtu pamoja ni kitu kinachohitaji busara na hekima. Kama ndugu wanagombana, inakuwaje wapenzi ambao wamekutana ukubwani?

Ili kushinda majaribu ya ndoa inabidi umfikirie zaidi katika namna bora kuliko kuchukulia matendo yake juu juu.

Ifahamike ndoa haidumu kwa sababu ya watu kupendana tu. Kudumu kwa ndoa inategemea na mtindo wa maisha ya wanandoa kwa ujumla.

Kama mnapendana ila mnashindwa kusikilizana, kuelewana na kurekebishana kwa staha, tambua hiyo ndoa kudumu kwake kunategemea miujiza ya Mungu tu.

Mfikirie vema mwenzako muwapo katika ndoa. Usipende kuongea sana kuliko kusikiliza. Msikilize mwenzako. Heshimu anayolalamikia kwako kisha yatafakari kama yana ukweli. Kama kuna ukweli katika hizo lawama zake juu yako yafaa ufanye mpango wa haraka ubadilike.

Ila pia kama hakuna ukweli ila anakupa lawama kutokana na kutokukuelewa vizuri, yafaa utumie busara katika kumwelewesha.

Ndoa si sehemu ya kuoneshana ubabe, ujeuri ama ujuaji. Ni sehemu ya kuelewana, kubembelezana na kupeana sababu ya furaha.

Kila mtu katika ndoa anatakiwa aone sababu ya kumsikiliza, kumwelewa na kuheshimu hisia za mwenzake. Kama ukijiona uko sahihi kila siku, si tu ndoa yenu itatawaliwa na ugomvi kila siku ila pia utamfanya mwenzako adhani hayuko na mtu sahihi katika maisha yake.

Tambua kuwa baada ya kuingia katika ndoa unalazimika kufikiria pia kwa niaba ya mwenzako na si kujifikiria mwenyewe.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUMFANYA MWANAMKE AKOJOE HARAKA WAKATI WA TENDO

JINSI YA KUMKOJOLESHA MWANAMKE KWA HARAKA

JINSI YA KUMFANYA MWANAMKE ASIKUSAHAU KATIKA TENDO LA NDOA