ABURUZWA MAHAKAMANI KWA KUMSHIKA SEHEMU ZA SIRI MTOTO WA MIAKA MITATU

Mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Vicent Marseli mkazi wa Mbezi jijini Dar Es Salaam, Amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, akikabiliwa na shtaka la kumshika sehemu za siri mtoto wa miaka mitatu ili kujiridhisha kimapenzi.

Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Neema Moshi, Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, amedai mnamo Februari 18, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa alifanya shambulio la aibu kwa kumshika mtoto huyo sehemu za siri ili ajiridhishe kimapenzi.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na mwendesha mashtaka wa Jamhuri alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kusogeza mbele tarehe ya kutajwa tena.

Kwa upande wa dhamana ya mshtakiwa, Hakimu Kiliwa alisema dhamana iko wazi kwa masharti ya wadhamini wawili watakaotoa bondi ya Tsh 50,000 kila mmoja.

Hata hivyo, Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yake itakaposomwa tena Juni 25, mwaka huu.


Post a Comment

0 Comments