KILA kukicha napata ujumbe kutoka kwa wanandoa ambao hulalamika kuwa hawawaelewi wenza wao kwani wamebadilika lakini malalamiko mengi yanaelekezwa kwenye tabia hizi ambazo nitakueleza hapa na kama zinakuhusu, kabla ndoa yako haijapinduka unatakiwa kuzifanyia kazi.
Tabia hizo unaweza kuzipitia moja baada ya nyingine, yawezekana ukawa huna zote lakini ukawa na moja au mbili ambazo zinakuhusu. Fuatilia hapa chini…
MOJA; HUNA MUDA KWA MWENZA WAKO
Wanandoa wengi au wapenzi hawana muda wa kupumzika na wapenzi wao na kubadilishana mawazo. Hii ni kutokana na maisha ya sasa yanavyoenda. Tatizo hili au tabia hii inaweza kukusababishia mwenza wako kukukosa na kuona kuwa hana muda na wewe. Kwa maana hiyo inaweza kusababisha yeye kuvunjika moyo na kuizoea tabia ambayo kimahusiano inafifisha mapenzi.
MBILI; KUSEMA UONGO
Hakuna anayependa kudanganywa hasa pale ambapo hapastahili lakini pia hakuna ambaye anapenda kuahidiwa kitu kisha asitimiziwe. Baadhi ya watu tulio kwenye uhusiano, tunapenda kudanganya sana, kitu ambacho unaweza kukidharau lakini mwenza wako kikamuumiza sana.
Lakini pia hili la kuahidi halafu unapotezea. Kumbuka uliye naye ni mtu mzima, ukimwambia nikirudi safari nitakuletea zawadi halafu unarudi mikono mitupu bila kuwa na maelezo, ni lazima mwenza wako atakuona unamchukulia kama unamdharau.
TATU; KUTOMUAMINI
Kuwa na wasiwasi na mwenza wako kila wakati ni tabia mbaya ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuivunja ndoa. Jenga imani hata kama unatilia shaka jambo flani, lifanyie kazi kwa makini na usimuoneshe umpendaye kuwa una mashaka naye mara kwa mara.
NNE; KUCHUKULIA POA KILA KITU
Kama mwenza wako hakulalamikii kwa jambo baya unalomfanyia au unalomnyima, ni rahisi kujisikia vibaya. Unapokuwa unajaribu kumwambia mpenzi wako kuhusu jambo ambalo amekuumiza na limeku-changanya ni vema ili uweze kukupa furaha,
ni vizuri kama atafahamu unahitaji nini na unataka nini lakini usipolalamika atakushangaa kwani moja kwa moja atahisi huna upendo naye. Wanandoa wengi huhisi wanapendwa kama watalalamikiwa jambo, hasa wanandoa wanawake wao wakilalamikiwa na waume zao huamini wanapendwa.
TANO; KUKACHA FARAGHA
Mara nyingi wapendanao, penzi hujengwa na tendo la ndoa. Sasa ikitokea wewe ni mtu ambaye una tabia ya kupenda kupuuza tendo hilo hasa anapokuhitaji mpenzi au mumeo/ mkeo, unamkatisha tamaa mwenza wako. Kumbuka kuwa mahusiano bila ya tendo yataenda pabaya. Kuwa bize mara kwa mara na mambo yako au maisha yanayokufanya uwe na sababu ya kukosa muda wa kutosha wa kucheza na mwenza wako ni tatizo, kumbuka tendo ni muhimu kuliko chochote.
SITA; BIZE KUSAKA PESA
Kuwa na kazi kwa ajili ya kuwaendeleza kimaisha ni muhimu hasa kwa maisha ya sasa lakini linapokuja suala la mahusiano au ndoa ukiendekeza kazi wakati wote unaweza kujikuta ukivunja ndoa au uhusiano kwa ujumla.
SABA; MATUMIZI MABAYA YA PESA
Pesa ni kitu muhimu sana kwa maisha ya binadamu lakini isipochukuliwa kwa umakini inaweza kuleta balaa. Usipoangalia pesa inaweza kukupa ‘stresi’, unaweza kuingia kwenye malumbano na mwenza wako sababu tu ya pesa.
Kushindwa kwako kupanga bajeti vizuri, uchumi unaweza kushuka kwenu. Kukosekana kwa utunzaji mzuri wa pesa kunaweza kuwakosesha furaha ya ndoa kabisa. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unakuwa na matumizi mazuri ya pesa hata kama mnazo nyingi.
0 Comments