KUNA WATU, KUNA WAUAJI KWENYE MAPENZI,JIELIMISHE

 NI Jumatatu nyingine tunakutana kwenye darasa letu. Hapa tunajifunza na kupeana misingi ya kuhusu masuala mbalimbali ya uhusiano na maisha kwa jumla Uhusiano mzuri ni ule ambao hausikii kelelekelele kila wakati. Hata ikitokea wametofautiana kauli kidogo, wanarekebisha na maisha yanaendelea.
Dunia ya leo makelele ni mengi zaidi kuliko amani. Watu wanagombana zaidi kwenye uhusiano wa kimapenzi kuliko kuwa na wakati mzuri wa kufurahia maisha yao ya uhusiano. Ndugu zangu, mnapokuwa kwenye aina hii ya maisha ni hatari. Unapaswa kuishi ukiwa na amani ya moyo, mfurahie uwepo wenu hapa duniani vya kutosha huku mkijiandaa na kurudi kwake Muumba maana ukweli ni kwamba sisi sote tutakufa hivyo tujiandae pia na kifo. Kwenye masuala ya kusaka mwenza wa maisha, mara zote kumekuwa na changamoto sana kwani kwa vyovyote vile huwezi kumjua mtu moyoni mwake yukoje. Hujui anawaza nini, akikasirika anakuwaje au tabia zake zikoje.
Ndiyo maana nasema kweli eneo hili lina changamoto sana. Ili kuweza kuvuka salama ni lazima uwe na jicho zuri la kibinadamu, lakini pia uongozwe zaidi na lile la Kimungu. Wapo watu wamejikuta kwenye matatizo makubwa kwa sababu tu walishindwa kuona vizuri.
Walianzisha uhusiano, wakaendelea na safari bila kujiridhisha vizuri na mwisho wa siku wakaja kugundua kwamba wameingia kwenye uhusiano na wauaji. Mtu unajikuta umeingia kwenye uhusiano na mtu ambaye kuua kwake siyo jambo zito. Mtu ambaye kukudhuru na panga au silaha yoyote kwake si jambo la ajabu. Mtu wa aina hiyo anaweza kufanya lolote, wakati wowote na wala hajali, mtu wa aina hiyo anakuwa si yeye. Ni kama shetani, unapokuwa naye kwenye uhusiano ni hatari sana.
Ndiyo maana leo hii nazungumza na wewe ili uweze kuwatambua. Uweze kujifunza mapema unapokuwa kwenye hatua za awali. Omba sana kwa imani yako unapotaka kuingia kwenye uhusiano na mtu kwa sababu dunia ya sasa mambo yamebadilika sana. Usikurupuke kuingia, tafakari sana na ikiwezekana jipe muda wa kumjua yule unayetaka kuingia naye kwenye uhusiano ni mtu wa aina gani, ukijiridhisha angalau kidogo, ingia!
Mbali na wauaji, wapo watu ambao wana tabia mbaya kupita maelezo. Ukimuona barabarani au mahali popote pale unaweza kumuona ni mtu mstaarabu na mwenye hekima, lakini kumbe wapi. Ana upande wake wa pili ambao huo ukija kuuona utatamani dunia ipasuke uingie ndani.
Wapo baadhi ya wanawake ni wafanyabishara kabisa ya miili, lakini ukiwaona huwezi kuwadhania. Wapo pia wanaume ambao ni malaya kupindukia, lakini ukikutana naye mahali unaweza kusema mume si ndiye huyu, kumbe wapi bwana, hata ufanye nini huwezi kumtuliza.
Mbali na macho yako ya kibinadamu, muombe Mungu sana akuoneshe mume au mke mwema. Akuongoze kumjua mapema mtu ambaye kweli hana maneno, hana fujo na ana hofu ya Mungu. Mtu mwenye hofu ya Mungu siku zote hawezi kuwa muuaji.
Mwenye hofu ya Mungu hawezi kukufanyia ukatili wowote maana anatambua kwamba kufanya hivyo ni kinyume na matakwa ya Mungu. Ukimpata mtu wa aina hiyo usimkwaze, mtie moyo na muiboreshe safari yenu kila siku Kosoaneni kwa busara, msahihishe mwenzako kwa kutumia hekima pale unapoona ameenda mstari usio sahihi, mvumiliane na mtashangaa miaka inakatika tu mkiwa pamoja.
Nifuate Instagram & Facebook; Erick Evarist, Twitter: ENangale.

Post a Comment

0 Comments