BINTI WA RAIS WA ZAMANI WA ANGOLA ATOROKEA ULAYA

Luanda, Angola/AFP.Welwitschia "Tchize" dos Santos, mmoja wa mabinti wa rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos na ambaye alikuwa mwanasheria wa chama tawala, amedai kuwa amelazimika kuikimbia nchi yake baada ya kupata vitisho.
"Nilipata vitisho kutoka kwa kiongozi wa kundi la bunge na maofisa wa usalama," anasema Welwitschia katika sauti iliyorekodiwa na kutumwa kwa vyombo vya habari juzi Alhamisi.
"Nilikimbia baada ya kumteka mbunge kwenye ndege" mwezi Januari alisema.
Manuel Antonio Rabelais, waziri wa zamani na mbunge wa chama tawala cha MPLA (People's Movement for the Liberation of Angola), alizuiwa kuondoka nchi hiyo wakati alipokuwa akipanda ndege kwenda Lisbon kutokana na tuhuma za rushwa.
Juzi, MPLA ilipendekeza kumzuia Welwitschia kuingia bungeni baada ya kutoweka nchini Angola kwa siku 90, kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa spika baada ya mkutano wa wabunge wa chama hicho.
Welwitschia ni mkosoaji mkubwa wa rais aliyemrithi baba yake, na anaituhumu MPLA kwa kujaribu kumshusha hadhi.
Wakati wa kampeni zake za urais, Lourenco, waziri wa zamani wa ulinzi, aliahidi kutomshughulikia dos Santos.
Kwa sasa Welwitschia yuko Uingereza akiwa na dada yake, Isabel dos Santos, ambaye pia ni binti wa dos Santos na ni mwanamke tajiri kuliko wote barani Afrika.
Isabel amekuwa akipuuza wito kadhaa kutoka kwa wachunguzi nchini Angola wanaochunguza malipo yaliyofanywa wakati binti huyo alipokuwa kiongozi wa kampuni kubwa ya serikali ya mafuta, Sonangol.
Binti huyo anaweza kukamatwa wakati atakaporejea Angola.
Kaka yake, Jose Filomeno dos Santos pia amezuiwa kuondoka Angola na aliwekwa mahabusu kwa miezi sita kutokana na tuhuma za rushwa.
Jose Eduardo dos Santos alikuwa rais wa Angola kwa miaka 38 hadi mwaka 2017.

Post a Comment

0 Comments