WATU wanateseka sana kwenye mahusiano kwa kuipoteza amani ya moyo. Wanaishi kwenye maugomvi, wanapoteza kabisa muelekeo kutokana na visa mbalimbali wanavyopitia kwenye mahusiano. Unakuta mtu anaumia sababu yupo na mtu ambaye pengine anampenda sana, anaogopa kuchukua uamuzi wowote mbaya akifikiria kwamba moyo wake utateseka. Hapo ndipo kwenye kiini cha mada yangu ya leo. Migogoro katika mahusiano huwa ni jambo ambalo linarudisha nyuma sana. Kunapokuwa na migogoro kwenye mahusiano hamuwezi kusonga mbele, hata mafanikio ya kimaisha hamuwezi kuyapata sababu muda wa kufikiria vitu vya mafanikio haupo.
Wakati ambao pengine mlipaswa kufurahi ili akili yenu iweze kupanga mambo, nyinyi mnaukosa huo utulivu. Kila mmoja wenu anakuwa amemkasirikia mwenzake, anawaza namna ya kujinasua kwenye migogoro hiyo anashindwa. Kushindwa kujinasua kwenye migogoro hii mara nyingi huwa kunatokana na kila mmoja kushikilia hoja yake na kujiona yupo sahihi na mwenzake ndiye mwenye makosa. Hivyo, hakuna ambaye anakuwa tayari kujishusha na kumuomba radhi mwenzake.
Kila mmoja ni jeuri, anajiona yupo sahihi na matokeo yake sasa mnaweza kuishi wiki, mwezi au hata miezi; nyinyi ni watu wa kurumbana tu. Yaani watu mnaishi nyumba moja lakini hakuna mwenye muda na mwenzake. Ndugu zangu hii ni hatari sana sababu kwenye maisha siku zote wapendanao wanatakiwa kuwa na muelekeo mmoja ili waweze kusonga mbele.
Hata kama si kimafanikio kwa maana ya kifedha lakini kiakili na kimwili. Ndio maana nasema kwamba amani ya moyo ni muhimu sana katika maisha yetu, wanadamu tunapaswa kuitafuta kwa gharama yoyote. Unapoona imetoweka, kuwa wa kwanza kuitafuta. Vivyo hivyo kwa mwenzako, akiona haipo naye aitafute haraka.
Hili ni kama darasa, fundishaneni umuhimu wa somo hili hususan kipindi ambacho mnakuwa kwenye wakati mzuri. Ule wakati ambao mnaishi vizuri, mnafurahia mahusiano yenu muutumie pia kuelekezana juu ya jambo hili.
Ili inapotokea mmepishana kauli kidogo, kila mmoja wenu ajue namna ya kuihangaikia amani ya moyo. Amani ya moyo ni jukumu lenu wote kuitafuta, msiwe watu wa kuipoteza kwa namna yoyote ile. Iwe kipaumbele chenu maana isipokuwa tu, hamtafika mbali zaidi ya kuishia kuumizana kama si kuachana.
Ikiwa upo na mtu kwenye uhusiano halafu akawa hatambui umuhimu wa amani ya moyo, basi tegemea kupata maumivu makali. Ya nini kuteseka? Ya nini kupata maumivu maishani mwako? Utaishi kwenye mateso mpaka lini?
Hakikisha tu kwa gharama yoyote unahakikisha umetimiza wajibu wako kwa mwenzi wako, kuitafuta amani ya moyo pindi inapokuwa imetoweka. Na ukiona umetimiza jukumu hilo kikamilifu halafu ukaona mwenzako hajali, siku zote nasisitiza ni vyema kujiweka pembeni.
Dunia ipo huru hii, huna sababu ya kuteseka na mtu ambaye hajui thamani ya maumivu yako. Wewe unalia tu usiku na mchana mwenzako anacheka, anaendelea na ratiba zake za maisha kama kawaida. Wewe huli, unakonda wakati mwenzako anakula kisawasawa na kunenepa zaidi.
Achana naye. Jiweke pembeni kwa muda kumpima na akitambua thamani yako atarudi. Asiporudi mshukuru Mungu, hakuwa wako. Wa kwako yupo na akitokea utashangaa kuona mambo yanavyowaendea vizuri.
Zingatia sana amani ya moyo hususan mnapokuwa kwenye hatua za awali za mahusiano. Mkiruhusu muendelee na mahusiano huku mkiwa hamna amani ya moyo, ni hatari sana huko muendako!
Instagram&Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.
0 Comments