Zijue sababu za mimba kuharibika


MIMBA yenye wiki 28 au chini ya hapo uharibika au kutoka, hali hii kitaalamu inajulikana kama ‘miscarriage’ na kwa kawaida mtoto aliye tumboni katika umri huu, hataweza kuishi nje ya tumbo la mama.  Zaidi ya asilimia 80 ya mimba uharibika katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito na baada ya miezi hiyo kupita, uwezekano wa mimba kuharibika hupungua. Miaka ya hivi karibuni baadhi ya wanawake wamekuwa wakipata changamoto ya kuharibika kwa mimba mara kwa mara, hali inayosababisha baadhi yao kukosa matumaini ya kupata watoto. Zipo sababu zinazochangia mimba kuharibika, matumizi ya pombe, sigara na hewa chafu kuwa miongoni mwa vyanzo.
Sababu zipo nyingi kulingana na umri wa mimba husika. Mimba imegawanyika katika vipindi vitatu. Miezi mitatu ya mwanzo ambayo mtoto hujishikiza, miezi mitatu ya katikati na ile mitatu ya mwishoni kukamilisha miezi tisa.
Kila kipindi kina sababu zake, huku sababu kubwa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo zipo zaidi ya tatu za kitaalamu ambazo husababisha mimba kuharibika.
Sababu hizo ni pamoja na homoni kutokuwa sawa, suala hilo husababisha mimba kutoendelea kukua vizuri na mambo mengi yanaweza kutokea ikiwemo mimba kutoka. Homoni zinaposhindwa kuwa sawa, husababisha mizizi inayoshikilia mimba tumboni kutojengeka vizuri ambayo ndiyo huzalisha kondo.
Vinasaba ni suala lingine ambalo ni kisababishi kikubwa cha mimba kutoka, hasa tatizo hili huwa sababu kubwa ya kutoka kwa ujauzito au kuharibika na vinasaba vinaweza kuwa vya mama au baba. Sababu nyingine ni matumizi ya dawa kali bila ya ushauri wa daktari hasa dawa za antibayotiki zinazotibu malaria mimba ikiwa changa.
Kipindi cha pili cha ujauzito huwa ni kuanzia umri wa mimba ya miezi mitatu mpaka sita, mimba huhitaji kizazi kiwe na uwezo wa kuibeba bila kutetereka. Katika kipindi hiki mimba huanza kukua na hivyo huhitaji kizazi imara ambacho kitaweza kuibeba, wakati huu shingo ya kizazi inabidi iwe imekaza na kama imelegea, mimba itaporomoka na wakati huu wajawazito wengi mimba hutoka bila kusikia uchungu wowote.
Katika kipindi hicho, maambukizi pia huchangia mimba nyingi kuharibika; ikiwa magonjwa ya zinaa na iwapo mama atakuwa na tatizo la kisukari au malaria kali.
Kipindi cha mwezi wa sita mpaka tisa ni kipindi cha mwisho cha ujauzito ambapo, kuna mambo kadhaa pia huchangia mimba kutoka, ikiwa tatizo la shinikizo la damu au presha, magonjwa sugu ya mfumo wa mkojo (U.T.I) na matumizi holela ya dawa.
Lakini pia hewa chafu ina uwezo mkubwa wa kuchangia kutoka kwa ujauzito.
Matatizo ya maumbile ya mtoto tumboni (genetic abnormalities) pia yanaweza kuwa sababu.
UCHUNGUZI NA VIPIMO
Pale unapopata dalili hizi, wahi kumuona mtaalamu wa afya haraka. Hii itasaidia kuokoa maisha ya mtoto na ya mama. Mtaalamu wa afya atakufanyia uchunguzi wa tumbo na via vya uzazi; ikijumuisha kutazama tumbo, uke na shingo ya uzazi kama imefunga au la.
MATIBABU
Matibabu hutolewa kutokana na hali ya mimba ilivyo. Mimba inaweza kuwa imeharibika na kutoka (complete abortion), lakini bado ipo kwenye mji wa uzazi.
Kama mimba imeharibika na kutoka, basi mama atapewa dawa za kutumia ili kuzuia maambukizi ya vijidudu vya bakteria (antibiotics) na za kuongeza damu hasa kama alitokwa na damu nyingi.
Kama mimba imeharibika lakini bado haijatoka yote, basi mji wa uzazi utahitaji kusafishwa. Kuna njia mbili ambazo hutumika kusafisha mji wa uzazi, nazo ni; kuusafisha kwa kuvuta (Manual Vacuum Aspiration). Njia hii hutumika pale ambapo mimba ina chini ya wiki 12.
Njia nyingine ni kusafisha mfuko wa uzazi kwa kuukwangua (Dilatation and Curretage). Njia hii hutumika kama mimba ni kubwa zaidi ya wiki 12. Shingo ya uzazi hutanuliwa na kisha curreter huingizwa ambayo hukwangua mji wa uzazi na kuondoa masalia ya mimba au mimba iliyobaki.
Baada kusafishwa utapewa dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria na dawa za kuongeza damu ikibidi.
USHAURI
Unaweza ukaendelea kupata maumivu kwa siku kadhaa, lakini yatakuwa yanapungua polepole. Damu inaweza ikaendelea kutoka kidogo kwa muda wa wiki moja, ikizidi muone daktari.
Ili kupata mimba tena, tunashauri kusubiri kwa muda usiopungua miezi mitatu kabla ya kupata mimba nyingine, ili kuruhusu viungo vipone vizuri na kuwa tayari kutunga mimba nyingine.
Na Dk. Marise Richard

Post a Comment

0 Comments