NI matumaini yangu mpenzi msomaji wa safu hii, utakuwa kwenye hali nzuri na tayari kusoma kile ambacho nimekuandalia Jumatatu hii.
Mahusiano ya kimapenzi siku zote yana nafasi kubwa sana katika maisha yetu. Yanapokwenda vizuri, furaha ya moyo inapopatikana, basi mtaishi miaka nenda rudi bila mikwaruzano na hata ikitokea, mnaimeza ndani kwa ndani. Mapenzi yana changamoto zake, wengi wamejikuta yakiwashinda kwa sababu ya kutosoma alama za nyakati. Wanashindwa kuelewa kwamba wapo kwenye nafasi gani na kujikuta wakiishi tu kimazoea bila kujua wanafanana tabia au la.
Ndugu zangu, japo ni vigumu kuujua moyo wa mtu, lakini hakikisha pindi unapoanzisha uhusiano na mtu, awe kweli ni mtu ambaye mnafanana. Mnaivana kitabia, mnashibana vya kutosha na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza mbele yenu.
Hakikisha uliyenaye anakupenda kwa dhati kutoka moyoni kabla ya kuzama penzini. Japo watu wanabadilika, lakini angalau, jiridhishe kwa jinsi unavyoweza kiasi cha akili yako kuweza kung’amua kwamba kweli uliyenaye anakupenda kwa dhati au kuna msukumo mwingine.
Anayekupenda kwa dhati utamjua tu kwamba huyu ananipenda kweli au ananizingua. Anayekupenda kwa dhati atakujali, atakuthamini na hayupo tayari kukupoteza. Anayekupenda kwa dhati hawezi kukuingiza kwenye matatizo na badala yake atakuwa mlinzi wako muda wote. Kila mara atahakikisha anaitafuta furaha yako kwa gharama yoyote ile.
Hatapenda kukukorofisha na kukusababishia maumivu ya moyo. Atakupa faraja wakati wote. Wakati wa matatizo yako, ataguswa nayo kama vile ambavyo yamekugusa wewe. Huyo ndiye mtu ambaye mtakuwa mmefanana na kweli mnaweza kuruka safari moja.
Kinyume cha mtu mnayefanana, ni mtu ambaye hamfanani. Ukiishi na mtu ambaye hamfanani tabia na mienendo yenu, basi jua wazi kwamba msingi wenu wa maisha ya uhusiano hauwezi kuwa imara. Ni lazima tu utatetereka na hata kuanguka kabisa.
Hii ndiyo maana tunashuhudia ndoa nyingi sana za sasa hazidumu. Watu wengi wanaingia kwenye ndoa kutokana tu na tamaa mbalimbali. Mwanamke anataka tu kuitwa bibi harusi na mke wa mtu au mwanaume naye anataka tu kuitwa bwana harusi au mume wa mtu.
Hawafanani, hawana upendo wa dhati kati yao. Yawezekana pia watu wakaoana kwa tamaa za fedha, siku fedha hizo zikiyeyuka tu, basi na ndoa inayeyuka. Mifano ipo mingi, najua hata wewe au jirani yako, yawezekana utakuwa umeshuhudia au kuhadithiwa kitu cha namna hiyo.
Mwenye mapenzi ya dhati hawezi kukimbia pindi mambo yanapokuwa magumu kwenye maisha ya uhusiano. Atasimama na wewe hadi dakika za mwisho, kama alivyosimama wakati mlipokuwa kwenye nyakati nzuri.
Ni jukumu lako kuchagua kuishi na mtu ambaye anafanana na wewe au la. Kama hamfanani, muepuke mapema kabla safari yenu ya uhusiano haijafika mbali. Endapo ikitokea tayari mmeshafika mbali, tafuta watu wazima au viongozi wa dini wanaweza kukusaidia na si kufanya maamuzi kwa kutumia akili yako pekee.
Madhara ya kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hamfanani ni mengi sana. Chunga sana, usiishi na mtu ambaye hamfanani, muepuke. Watu wanaoana wakiwa hawafanani, matokeo yake huwa wanaweza kusalitiana, kugombana au hata kuuana.
Kwa nini mfikie huko? Chukueni hatua stahiki katika muda muafaka!
0 Comments