JINSI YA KUMTAMBUA MWANAUME ULIYENAE KAMA NI TAPELI WA MAPENZI

Inawezekana upo katika uhusiano na tapeli wa mapenzi bila kujua, hiyo ni sumu na unachotakiwa kufanya sasa ni kuanza kumchunguza mpenzi wako mapema isije kuwa upo kwenye foleni!

Hakuna kitu kibaya kama kuwa katika foleni ya wapenzi kwa mpenzi mmoja, tena mbaya zaidi awe ni yule ambaye moyo wako umempenda kwa dhati.

Kumbuka, kuwa katika uhusiano na mtu ambaye haeleweki ni sawa na kukaribisha matatizo katika maisha yako, huna sababu ya kuishi kwa wasiwasi ukiwa hujui mpenzi wako anakuchukulia vipi.

Wapenzi

Anza kumuwekea mitego mapema. Lakini katika mitego yako achana na simu yake kabisa, huna sababu ya kuchunguza simu yake lakini kama ni msaliti utajua tu, unafikiri atajificha mpaka lini?

Atafanya mambo yake gizani mpaka lini? Kuna siku utagundua na kumuacha aendelee na umalaya wake kama ameona ndiyo maisha. Usikubali kabisa kuwa katika penzi la kiutumwa, penzi la kisaliti, kuwa na mtu ambaye anakuchanganya wa kazi gani zaidi ya kukupotezea muda na kukukaribishia machozi?

UTAMJUAJE MPENZI LAGHAI?

Hapa ndipo kwenye kazi, kwa bahati mbaya sana kama ikitokea ukampenda mtu sana hata kama akifanya mabaya kiasi gani unaweza usiyaone, kama wewe ni wa aina hii unapaswa kubadilika kifikra. Mwone wa kawaida, fanya uchunguzi wako polepole na kama ukiona moja kati ya mambo yafuatayo, ujue kuna kitu.

(a) Hataki ujulikane na rafiki zake

Hii ni kati ya alama walizonazo matapeli wa mapenzi, ni mtu wa kufanya mambo kwa upekee sana. Kila dakika hakaukiwi na neno nakupenda sana, lakini moyoni mwake hakuna alama hata moja ya mapenzi kwako.

Ni vigumu kumtambua mtu wa aina hii lakini chunguza kuhusu hili, hapendi kabisa kukukutanisha na rafiki zake na hata mkikutana nao kwa bahati mbaya basi hatakutambulisha na kama akikutambulisha hatakutambulisha kama mpenzi wake rasmi. Ataishia kusema ninyi ni marafiki mlioshibana!

Tangu lini mpenzi akatambulishwa kama rafiki? Mtu anapomtambulisha mpenzi wake humtambulisha kwa kujisikia furaha moyoni kwamba anamtambulisha mpenzi wake lakini inakuwaje kwako akutambulishe kama rafiki?

Baadaye utakapomuuliza hawezi kuwa na jibu la maana, atabaki kukuambia hata kama akikutambulisha kama rafiki jamaa ataelewa kuwa ni mpenzi wake, hii inaingia akilini kweli?

Hakuna ukweli kama huo ndugu zangu! Huo ni ulaghai na anaogopa kukutambulisha kama mpenzi maana tayari ameshaonwa akiwa na wapenzi wengine. Sasa kama ndivyo, atatambulisha wangapi? Aseme wewe ni nani? Chukua hatua usikubali kupotezewa muda wako.

(b) Msiri kupitiliza

Hii ni alama nyingine waliyonayo wanaume wa aina ninayoielezea katika mada hii. Siku zote mambo yake ni kwa siri kubwa, kama mna ahadi ya kukutana, hataki muongozane, atakuambia mkutane moja kwa moja sehemu husika. Hata muda wa kuondoka atafanya kila njia ili kila mmoja aondoke mwenyewe na kama mkiondoka pamoja basi ujue ni usiku na hakuna atakayewaona.

Ikitokea akakubali kuongozana na wewe, hatapenda muongozane pamoja. Atalazimisha utangulie mbele yeye afuate nyuma, kwa nini? Kwa sababu anaogopa kujulikana kuwa yeye ni mpenzi wako na kama anaogopa anakupenda kweli? Mapenzi gani hayo yanafanywa kwa siri? Anakupotezea muda huyo.

(c) Hapendi ndugu wafahamiane

Mpenzi wa aina hii ni mjanja sana, kwanza kabisa atajifanya mtu mwenye ‘ubize’ sana, yote hii ni kukwepa kuwajua ndugu zako au wewe kuwajua ndugu zake! Wakati mwingine anakuwa hapendi ndugu zako na wake wakutane wakijua wazi kuwa nyie mna uhusiano, hili ni tatizo.

Hakuna uhusiano wenye heri na malengo ya kuishi pamoja siku zijazo ukawa wa kificho cha kiasi hicho. Kama ana nia na wewe basi atahakikisha anawafahamu baadhi ya ndugu zako na wewe unawafahamu baadhi ya ndugu zake, hayo ndiyo mapenzi ya kweli.

Mapenzi hayaishii kwa nyie wawili pekee bali hata kwa ndugu zenu. Mnapojuana inakuwa rahisi kusaidiana hata katika mambo mengine ya kawaida.

Post a Comment

0 Comments