TUNAENDELEA na mada yetu ambayo naamini ukiifuatilia hadi mwisho itakuachia mafunzo makubwa sana. Tunaangalia namna unavyoweza kupandisha thamani ya penzi lako kwa mwenzako.
Wiki iliyopita tuliona namna ambavyo kujirahisha kunaweza kushusha thamani ya penzi. Wepesi wa kutoa penzi na kujiachia na mwanaume ambaye hajakuoa huhatarisha nia ya ndoa.
Ikumbukwe kwamba, si kila mwanaume anafaa kuwa mume na si kila mwanamke ni mke. Utajuaje uliyekutana naye kama ndiye au siye? Ni fumbo. Wengine wanahamia kabisa kwa wanaume au wanakwenda weekend kufua na kufanya usafi wa nyumba. Ni makosa makubwa. Unadhani ataharakishia ndoa ya nini wakati kila kitu anapata?
SIKIA HUU USHAHIDI
Kijana mmoja ambaye hapa nitamtaja kwa jina moja la Jully, alinifuata kunitaka ushauri. Yeye anasema amejikuta amepoteza msisimko kwa mpenzi wake aliyedumu naye kwa miaka minne na anataka kumuacha ili aoane na mwingine.
Jully anasema: “Sikufichi kaka Shaluwa, nilimpenda sana Sarafina lakini sasa nahisi kama sikuwa sahihi kuwa naye. Kwanza ni mwepesi sana…hakunisumbua sana wakati namfuatilia, mbaya zaidi ameshatoa mimba zangu nne, wa nini mwanamke kama huyo?”
Nilipomwuliza kuhusu mwanamke anayetaka kumuoa alisema: “Huyu anaitwa Veronica, nilikuwa naye kabla ya Sarafina. Wakati huo alikuwa Sekondari, amemaliza UD mwaka jana – 2018 (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Ana msimamo hatari!
Ninavyozungumza na wewe hajawahi kunipa penzi na mpaka sasa amenithibitishia kwamba bado ana usichana wake. Kwa nini nisimuoe mwanamke huyu mzuri, anayejitambua na kujitunza? Hawezi kunisumbua kwenye ndoa yangu kama Sarafina.”
WANAWAKE MPO?
Kwa hiyo mmeona kumbe wanaume japo wanawalaghai muwape penzi haohao ni hodari wa kuwasema vibaya na kuwashusha thamani wakati wakiwaza kuhusu ndoa. Ni vizuri wanawake mkaamka na kujitambua na kufahamu thamani mliyonayo.
Acha kudanganyika, penzi si kigezo cha upendo wa dhati. Mbona mambo yako wazi tu! Kama anakupenda atume wazee nyumbani kwenu, taratibu muhimu zifanyike, uolewe kwa heshima na thamani yako ikiendelea kuwa juu. Mwanaume wa aina hiyo ni vigumu kukutesa.
KUWA MJANJA
Kusoma mada hii ni kitu kimoja lakini kuelewa na kubadilika ni kitu kingine. Badili utaratibu wa maisha yako huku ukizingatia kupandisha thamani ya utu wako.
ATHARI ZA KUHARAKISHA FARAGHA
Katika vipengele vilivyopita hapo juu, nimefafanua zaidi matatizo ya moja kwa moja ambayo mtu anaweza kuyapata kwa kuharakisha faragha ambapo nimeeleza kuwa kuna suala la kuchokwa na kuonekana wa kawaida.
Lingine ni kuonekana mwepesi kwenye suala la mapenzi hivyo mwanaume kuwa na mashaka kwamba hata kama akifikia uamuzi wa kukuoa unaweza kuwa mwepesi kutoa penzi kwa wengine kama ulivyofanya kwake. Tuangalie vipengele vinavyofuata.
(i) Hupunguza thamani
Heshima ya penzi ni kwenye ndoa. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kushushwa thamani baada ya kutoa penzi. Wanaume wengi huanza kuwa wasumbufu (kama ni kasumba yao) kwa wapenzi wao baada ya kutoka nao kimapenzi.
Pamoja na kwamba ni tendo la furaha lakini kwa mwanamke linampa unyonge na wakati mwingine huwa mwanzo wa utumwa wa mapenzi kwa kuogopa kuachwa wakati tayari ameshatumika! Hebu jiulize; utatumia/utatumika kwa wangapi? Ukifikiri kwa makini juu ya jibu la swali hili bila shaka utabadilisha mtazamo wako.
(ii) Hupunguza msisimko
Penzi la kienyeji mara nyingi hata wahusika huwa wanajua kabisa kuwa wanakosea. Makosa haya husababisha kupoteza msisimko wa ndani. Ni jambo la kisaikolojia sana na huenda muathirika asigundue tatizo hili kupitia dalili za kitaalamu atakazozionesha.
Mkishaibana huko nje huwa kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza msisimko wa kawaida. Mfano mawasiliano hupungua, hamu ya kuonana inapungua sana n.k
Hapa nisipoteze muda sana, wengi mnafahamu inavyokuwa; mwanaume akishatembea na mwanamke, taratibu ataanza kujiweka pembeni. Kama alikuwa anapiga simu mara nne au tano kwa siku, hupunguza idadi na wakati mwingine hupitisha siku nzima kabisa.
Mbaya zaidi, unaweza kumpigia wewe na bado asipokee, ukituma ujumbe mfupi hatajibu au atachelewa. Kesi nyingi sana nilizokutana nazo za wanawake wanaolalamika wapenzi wao kubadilisha utaratibu wa mawasiliano, baada ya kuwahoji walisema jambo hilo limejitokeza baada ya kuwapa penzi. Usikose wiki ijayo kwenye sehemu ya mwisho ya mada hii, kuna mengi ya msingi zaidi utakayojifunza.
0 Comments