JE, WAJUA KWANINI WANAUME HUONGOZA KWA USALITI WA MAPENZI?


UHUSIANO wa kimapenzi ni jambo gumu sana. Ugumu wake unatokana na ukweli kwamba, mwanaume aliyezaliwa na kulelewa katika mazingira tofauti, anakutana na mwanamke ambaye naye amezaliwa na kukulia katika mazingira mengine.

Wawili hawa wanaanza ukurasa mpya wa maisha, kila mmoja akiwa na historia tofauti kabisa ya huko alikotoka, unategemea itakuwa rahisi kwa wawili hawa kuishi bila misuguano?

Jibu ni HAPANA. Kwa lugha nyepesi, hakuna uhusiano wa kimapenzi ambao hauna changamoto na changamoto kubwa zaidi katika mapenzi ni usaliti.

Nimeshawahi kueleza huko nyuma na naendelea kueleza kwamba hakuna kitu kinachoumiza katika uhusiano wa kimapenzi, kama usaliti.

Ni ukweli kwamba licha ya usaliti kuwa jambo baya katika uhusiano, bado watu wanasalitiana kila kukicha.

Wanandoa wanasalitiana, wachumba wanasalitiana na hata wale ambao wapo kwenye hatua za awali kabisa kuelekea kwenye uchumba, nao wanasalitiana. Si ajabu hata wewe msomaji wangu, siku chache zilizopita umesaliti au umesalitiwa! Ni ukweli mchungu ambao ni lazima tujadiliane kuhusu namna ya kuukomesha.

Utafiti usio rasmi, unaonesha kwamba japokuwa wanawake na wanaume wote wanasaliti, lakini idadi ya wanaume wanaosaliti ni kubwa zaidi kuliko wanawake.

Kabla ya kujua sababu hizo, ni vizuri ieleweke kwamba katika kila usaliti unaotokea, kuna mambo mawili yaliyosababisha; matatizo katika uhusiano wa kimapenzi au matatizo ya mtu binafsi. Kama tunakubaliana katika hilo, hebu kila mmoja ajiulize, kwa nini wanaume wanaongoza kwa usaliti? Kwa nini wanaume wanawasaliti wake zao? Wanawake ambao wanafanya kila kitu kwa ajili yao?

TENDO LA NDOA Sababu kubwa inayofanya wanaume kuchepuka, ni kukidhi tamaa zao za kimwili. Utafiti uliofanywa na mtaalamu wa masuala ya kimapenzi, Dk Tamy Wilson wa nchini Marekani, unaonesha kwamba wanaume ambao wanatimiziwa haja zao za kimwili mara kwa mara bila vikwazo, wana nafasi ndogo ya kusaliti ukilinganisha na wale wanaopata haki ya ndoa kwa ‘mbinde’.

Kwa jinsi miili ya wanaume ilivyoumbwa, kadiri mtu anavyokaa muda mrefu bila kushiriki tendo, ndivyo tamaa za kimwili zinavyoongezeka na kama akishindwa kuwa makini, anaweza hata kutembea na hausigeli wakati ndani anaishi na mke mrembo mwenye sifa zote.

TABIA MBAYA Ukiachana na wale ambao wanasaliti kwa sababu hawana jinsi, lipo kundi lingine la wanaume ambao kihulka wana tabia mbaya tu! Atapewa kila anachokihitaji kwa mkewe, atahudumiwa kimwili, kiakili na kihisia lakini kwa sababu ana tabia ya kupenda kudanganya, kufanya mambo kwa siri na kukosa uaminifu, atasaliti tu.

Watu wa namna hii wanakuwa na matatizo ya kisaikolojia na mara nyingi, huwa hawadumu katika uhusiano hata mwanamke awe mvumilivu kiasi gani.

KUKOSA KUJIAMINI Sababu nyingine inayofanya wanaume wawe na tabia ya kusaliti mara kwa mara, ni kukosa kujiamini. Anaishi na mke au mpenzi mwenye sifa zote nzuri lakini moyoni mwake hajiamini, anahisi ipo siku mwanamke atamkimbia na kwenda kwa wengine, kwa hiyo kukitokea ugomvi kidogo ndani, anakimbilia kutafuta mwanamke wa pembeni akijidanganya kwamba hata mkewe akimkimbia, atakuwepo wa kumfariji.

Yupo tayari hata kumpangia nyumba mchepuko ilimradi tu awe na sehemu ya kukimbilia inapotokea ameachana na mkewe. Itaendelea wiki ijayo.

Post a Comment

0 Comments