UKIMPENDA KWA MALI NA PESA ZAKE, HAKIKA NDOA UTAIJUTIA!


WAKATI fulani huwa najiuliza kwa nini tunakuwa na wapenzi, kwa nini mapenzi yakawepo? Kwa nini tunaoa ama kuolewa? Kwa nini baadhi ya watu huamua kujinyonga baada ya kuachwa na wapenzi wao? Kwa nini mapenzi yamekuwa sehemu ya maisha yetu?  Kwa nini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Huwa najiuliza maswali mengi yenye kwa nini, yakihusisha mapenzi. Kwa ujumla kama nilivyo na maswali mengi, majibu pia yamekuwa mengi.
Kwa vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mapenzi hayo, hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni MTUMWA WA MAPENZI! Kama ndivyo, kwa nini uwe mtumwa?
Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi!
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia maisha yako na huyo mwandani wako! Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe!
Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake!
Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu!
Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla. Hii ina maana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, na lazima utamkaribisha!
DHANA YA KUJIFUNZA KUPENDA!
Baadhi ya wasichana wakito-ngozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo. Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo.
“Pesa anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitajitahidi kumpenda taratibu,” baadhi ya wasichana huwaza hivi. Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa.
MATATIZO YANAYOWEZA KUIBUKA
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati ambalo ndio msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.
Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, siku lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo, na kama ana hasira, anaweza kukua.
ZINGATIA HILI
Kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza likaharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa. Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo.

Post a Comment

0 Comments