HEYAHEYA, acha nicheke miye kwani sidaiwi na mtu, navuta hewa ya bure ya nini kujibana, najiachia nitakavyo. Kama hewa ingekuwa inauzwa kama luku mbona wengi tungepumua kwa mahesabu kila muda unaangalia kama mita imeanza kuisha! Hee heeeiyaaaa! Ushaanza kusema nina maneno mengi kama vile nimebemendwa, aiiih! Jamani mbona hivyo? Kwani kucheka ni kwa wenye meno tu na siye wenye mapengo tusicheke? Tuvumiliane basi mate yakiwarukia muone kama pafyumu, upo nyonyo?
Ushaanza maswali yako eti mate ya ugoro hayavumiliki? Jamani ina maana mbwia ugoro hatoi denda? Mmh! Hayo si yangu tuendelee na yetu. Jamani mashostito wangu mbona mwaka huu wangu, nani alikuambia kisasi cha kitu hulipwa kwa kitu? Au mmesahau akupigae shavu la kushoto mgeuzie na la kulia? Basi mwanakwetu, juzi nimefuatwa wanguwangu na binti mmoja ambaye anajua shughuli yangu, alinimwagia machozi shuu, nikamuuliza una nini? Si akanimwagia ya chumbani, mwaaa mwari likanishuka.
Moja alilolisema ni mumewe kukosa uaminifu ndani ya ndoa yao, pili kushindwa kupatiwa penzi kamili. Aliendelea kusema kuwa mume wake pamoja na kuwa naye mbali na kukutana kwa muda mchache bado amekuwa hakidhi haja zake na kufikia hatua ya kila siku kuwa katika mateso, siku chache anazokuwa yupo nyumbani amekuwa akimuacha njiani.
Wazo lake kubwa lilikuwa ni kutafuta mtu wa pembeni ili awe akimsaidia pale mume wake anapokuwa nje kwa kipindi cha mwezi mmoja mpaka miwili. Kwa upande wake aliona ule ndiyo ulikuwa utatuzi wa tatizo lake, lakini uamuzi ulikuwa mgumu na kuomba ushauri kabla hajachukua uamuzi huo mzito. Mmh! Mtoto wa kike ameyamwaga hadharani kwa kuwa mtu huyo wa kumtibu maradhi yake alishampata lakini alitegemea majibu yangu. Haya, mmemsikia jinsi mtoto wa kike anavyoteseka.
Nikamshauri asiwe mwepesi wa kutoa uamuzi bila kuangalia hasara zake, kwani ni kubwa kuliko faida. Nikamwambia tui la nazi kamwe haliwezi kutengeneza chai yaani mwanamke unapoikosa haki yako ndani katu huwezi kuitafuta nje ya ndoa.
Unapotokewa na tatizo la mwenzio kutokukufikisha au mpenzi wako kuwa mtu wa kusafiri kila wakati, mwari wee nakuomba uwe mvumilivu na kulilinda penzi lako, najua unakuwa kwenye hali mbaya lakini ustahimilivu ni jambo la msingi sana.
Siku zote unapokuwa kwenye wakati kama huo, jiepushe na mawazo ya kufikiria mapenzi au kuangalia picha za kikubwa ambazo zinaweza kukupa kishawishi cha mapenzi. Mawazo ya mtu huelekea pale anapoyaelekeza, pia moyo una haki ya kutamani lakini wewe ndiye unayetakiwa kuuzuia. Hakika ukiuendekeza moyo utakupeleka kubaya.
Kitu kingine acha kuwa bubu na mdomo umeugandisha kama gundi ya mbao unashindwa kumweleza ukweli mwenzako kuwa siku hizi hushibi, unataka ushibishwe lini kwa mfano! Unatakiwa kuwa mkweli kwa mwenzako, kumueleza jinsi unavyoteseka kwa yeye kukuacha njia panda ili mtafute ufumbuzi wa tatizo lako. Kwa leo ni hayo, tukutane tena wiki ijayo!
Ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu!
0 Comments