MGENI Jadi Kadika, Mbunge Viti Maalumu (CUF) ameiomba serikali iunde kamati maalumu ya kufuatilia mtandao wa watu wanaofanyisha watoto wa kike baishara ya ngono. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Kadika ametoa ombi hilo leo tarehe 25 Juni 2019 bungeni jijini Dodoma, wakati akihoji mpango wa serikali katika kudhibiti biashara hiyo inayodhalilisha watoto wa kike nchini.
Kadika amesema, kuna ongezeko kubwa la watoto wa kike kufanyishwa biashara ya ngono, na kuitaka serikali kuikomesha biashara hiyo kwa kuwachukulia hatua wanao husika na mtandao huo.
“Kuna wanawake wanawadhalilisha watoto, wanawatoa vijijini kuwapeleka mjini kuwafanyisha biashara ya ukahaba na ni kundi kubwa tu, kwa hivyo serikali ina mkakati gani wa kuunda kamati maalum ya kufuatilia watu hawa.
“Wanapopatikana wapewe adhabu ya kutosha ili iwe fundisho kwa wengineo ili suala hili la kudhalilisha watoto liondoke,”amesema Kadika.
Akijibu swali hilo, Dk. Faustine Ndugulile, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema serikali inatambua changamoto hiyo na kwamba, inatekeleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike, ikiwemo kuanzisha kamati za ulinzi za wanawake na watoto.
“Tuna sera ya maendeleo ya mtoto, tuna sheria ya mtoto ambazo zimeanisha haki za msingi za mtoto ikiwa pamoja mtoto ana haki ya kutunzwa, kuendelezwa na kutofanyishwakazi nzito. Ziko wazi na pale mzazi au mlezi anapokiuka hatua za kisheria huchukuliwa,” amesema Dk. Ndugulile na kuongeza:
“Niombe jamii na wabunge kusemea haya na tutaendelea kuchukua hatua pale tunapobaini. Suala la watoto kufanyishwa kazi ya kingono, katika mpango mkakati wa serikali katika kutokomeza matendo ya ukatili wa kijindia dhidi ya wanawake wa watoto tumeelekeza kuanzisha kamati za ulinzi za wanawake na watoto tutaendelea kuziimarisha.”
Wakati huo huo, Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga amehoji mpango wa serikali katika kutokomeza ongezeko la watoto wa mitaani, huku akiishauri kuhamasisha jamii kutumia uzazi wa mpango ikiwemo matumizi ya mipira ‘Kondomu’ kwa ajili ya kudhibiti mimba zisizotarajiwa.
“Uwepo wa kundi kubwa la watoto wazururaji kunasabaishwa na wazazi kutofuata njia bora ya uzazi wa mpango isiyo na madhara yoyote, na ni matumizi ya mpira wa kike na kiume.
Kwa sasa katika jamii yetu kumekuwa na tatizo kubwa la watu kutotumia mipira hiyo licha ya watengenezaji kuweka vionjo mbalimbali katika dhana hii , mfano ndizi chocolate na kupeleka si tu kuwa na watoto w amitaani bal ongezeko kubw a la magonjwa ya zinaa na Ukimwi,” amesema Mlinga.
Akijibu swali hilo, Dk. Ndugulile amewataka wananchi kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuondoa changamoto ya watoto wa mitaani.
“Moja ya kisababishi kinachopelekea watoto wa mitaani ni wazazi kutojiandaa kupata watoto, labda jingine watu kupata ujauzito katika umri mdogo pasipo kuwepo uwezo wa kulea. Serikali inahamasisha uzazi wa wa mpango, kuna matumizi ya dawa na matumizi ya mipira,” amesema Dk. Ndugulile na kuongeza.
“Rai yangu kwa jamii kabla hatujaingia katika suala la kupata watoto ni vizuri tukajitafakari katika suala la malezi na matunzo ya watoto.”
0 Comments