Na SHANGAZI
SHIKAMOO shangazi! Nimempa moyo wangu wote mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu sasa. Hata hivyo, nimekuwa nikishuku kuhusu iwapo ananipenda kwa dhati. Juzi niliamua kuthibitisha nikamtumia SMS kumwambia tuachane kwa sababu nimepata mwingine. Alinipigia simu ghafla huku akilia na kutaka kujua sababu yangu kumuacha ndipo nikamwambia ulikuwa mzaha tu. Ni wiki mbili sasa tangu siku hiyo na amekatiza mawasiliano, sijui anafikiria nini. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Ninashangaa umekuwa katika uhusiano huo kwa miaka mitatu na kufikia sasa hujaamini iwapo mwenzako anakupenda kwa dhati ingawa hujaelezea sababu ya kumshuku. Pili, ulitumia mzaha mbaya kupima mapenzi yako kwake. Bila shaka matamshi yako na yalimuumiza sana moyoni na labda haamini ulikuwa mzaha. Jambo la kufanya ni kumtafuta ili kumhakikishia kuwa huo kweli ulikuwa mzaha kisha umuombe msamaha.
Dadake mpenzi amenichanganya!
Kwako shangazi. Nina msichana mpenzi wangu lakini kuna dada yake ambaye ananipenda. Mimi pia amenivutia kwani ana maumbile na tabia nzuri kushinda mpenzi wangu. Nishauri.
Kupitia SMS
Iwapo unataka uhusiano wa maisha, huu ndio wakati wa kuamua na itabidi uwe makini. Kama kweli unampenda zaidi dada ya mpenzi wako na unaamini anatosha kuwa wako, basi mwambie ukweli mpenzi wako.
Nahofia ‘EX’ wake atavuruga harusi
Hujambo shangazi? Nilimuoa mke wangu akiwa na mtoto kutokana na ndoa ya awali na tumepata watoto wengine wawili. Tumeamua kuhalalisha ndoa yetu kwa kufanya harusi lakini nahofia huenda aliyekuwa mumewe akavuruga harusi yetu. Nishauri.
Kupitia SMS
Muda ambao umekuwa na mke wako ni mrefu iwapo tayari mmepata watoto wawili. Kama aliyekuwa mume wake hajauliza chochote kufikia sasa, sidhani anaweza kuwa na nia wala sababu nzuri ya kuingilia mipango yenu. Ninaamini kuwa yeye pia ameamua kuendelea na maisha yake. Endeleeni na mipango yenu.
Kimya chaniumiza moyoni, nifanyeje?
Hujambo shangazi? Tadhali ninahitaji ushauri wako. Ninaumia sana moyoni kwa sababu mwanamke mpenzi wangu ametoweka ghafla katika maisha yangu. Hataki kabisa nimuone wala kumpigia simu. Nilimkosea na ninataka kumuona ili nimuombe msamaha. Nimefanya hivyo kupitia SMS lakini amenyamaza tu. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Ingawa hujaelezea jinsi ulivyomkosea mpenzi wako, ni muhimu kwamba umeungama na kujuta. Nijuavyo ni kwamba makosa ni kawaida kwa binadamu. Umeonyesha mapenzi yako kwake kwa kumuomba msamaha. Inawezekana kwamba bado ana hasira kwa hivyo ninakushauri umpe muda. Kama kweli anakupenda atakutafuta.
Alinisaliti na rafiki na wala hakujutia
Shikamoo shangazi! Tafadhali nahitaji ushauri wako ili kutuliza maumivu niliyo nayo moyoni kuhusu mapenzi. Mwezi mmoja umepita sasa tangu siku niliyomfumania chumbani mwake na mwanamke rafiki yangu mkubwa. Niliondoka ghafla na baadaye akanitumia SMS kuniambia aliamua kumchukua rafiki yangu eti kwa kuwa ni mrembo kunishinda. Matamshi yake hayo yalinikata maini, nikahisi kama maisha yangu yamefika ukingoni. Kwangu maisha hayana maana tena na sijui hali itakuwa hivyo hadi lini.
Kupitia SMS
Ni hali ya kutisha na pia ya kuumiza moyo kwa watu wawili ambao umewathamini kwa maisha yako kukusaliti namna hiyo. Ninaelewa kuwa haitakuwa rahisi kwako kukabiliana na hali hiyo. Ninachoweza kukwambia ni kuwa maisha yako hayafai kumtegemea mtu yeyote yule kwa sababu binadamu ni kiumbe asiyeaminika. Hali yako hiyo itakuwa ya muda, bora tu ukubali kuwa sasa huna mpenzi, rafiki yako amepindua serikali yako. Ni kwa njia hiyo pia ambapo utaweza kupenda tena.
0 Comments