JINSI YA KUZUIA KUWA NA WIVU KATIKA MAPENZI

 WIVU ni hisia za ajabu, hususani katika uhusiano wa kimapenzi. Ukiuruhusu wivu kushamiri ndani yako, unaweza kuwa na nguvu yenye madhara makubwa kwako na kwa wengine. Hata hivyo, kwa upande mwema, wivu ni hisia za kawaida kabisa na kwamba kuna mikakati ya kimsingi ambayo unaweza kuitumia kuudhibiti. Mikakati hiyo inaweza kuchukuliwa kwa kupitia hatua tano zifuatazo:

Hatua ya kwanza. Piga moyo konde kwa kutuliza hisia zako unapoona wivu unakukamata. Jaribu kutambua mzizi wa hisia hizo. Wivu katika hali halisi ni woga wa kumpoteza mtu au kitu fulani. Wivu huenda sambamba na hasira kwamba mtu fulani amevamia eneo au mali yako.

Hatua ya Pili

Yazungumzie na watu wengine mazingira ambayo yanakuchochea uwe na wivu. Iwapo unaweza kumweleza mtu mwingine hisia zako katika hali ya utulivu na bila ya kuwa na msimamo wa lawama, unaweza kupata afueni na kukwepa lawama iwapo zitatokea baadaye. Kumbuka unapoelezea hali hiyo anza kwa kusema neno “Mimi” badala ya “Wewe” ili kuonyesha kwamba nadharia iko katika hisia na majibu yako na si hisia au matendo yanayofanywa na mtu ambaye unafikiri anataka kukunyima raha.

Hatua ya Tatu

Fikiria ni nini hasa lengo la wivu wako. Mara nyingi, watu hutumia hisia zao za wivu katika kutaka kutoa vipaumbele kwenye masuala yanayohusu maisha na uhusiano wao. Hivyo, jiulize ni kwa nini unahisi kuna tishio katika mazingira yanayokukabili.

Kufanya hivyo kutakusaidia kuchukua hatua njema na za busara katika kuelewa ni nini kilicho muhimu kwako. Kwa mfano ukigundua mume anataka kukuacha, anakusaliti kwa sababu ya ukorofi wako, chukua hatua ya kuondoa ukorofi huo, ili woga wa kuachwa uondoke. Timiza majukumu yako katika uhusiano wako, usiwe mtu wa kumfikiria mwingine na kuacha kujifikiria mwenyewe!

Hatua ya Nne

Ni muhimu kuzitambua fikra na maneno yanayokuja akilini kwako ambayo yanaweza kuchochea hisia za wivu moyoni mwako. Watu wanaojiona ni wa hali ya chini na wanaoamini kwamba watu wengine wanawatenga, mara nyingi hujikuta katika dimbwi la wivu. Fanya juu-chini utambue fikra zinazokutuma kuwa na hisia za wivu, na badala yake fikra hizo zifute

na kupanda fikra za kujiamini.

Iwapo una marafiki au familia ambayo inachochea hisia hizo mbaya, basi ni heri kwenda kutafuta marafiki ambao watakuunga mkono katika hali ya kujiamini. Hebu jiulize kama mwanaume alikuchagua wewe miongoni mwa wanawake milioni 50, kwa nini usijione mshindi kwake na kujipa nafasi ya kudumu? Unaweza kujiamini, punguza wivu jenga uhusiano wako wa kimapenzi.

Hatua ya Tano

Jipe muda wa kukomaa na kujifunza yale yote yanayotokana na wivu. Huwezi kujenga moyo wa kujiamini katika muda mfupi. Ni lazima kwanza ujisafishe roho na hisia zako, ufanye mazungumzo mbalimbali na watu wengine ili kupata ujuzi wa kukabiliana na wivu ambao ukizidi huweza kuwa kero ndani ya nyumba na hatimaye kuvunja penzi lako.

Post a Comment

0 Comments