SHANGAZI NISAIDIE, NINA MWANAMKE ANA WIVU HADI ANAKERA

Habari za kazi, pole na majukumu. Naomba ushauri labda utanisaidia kuwa na amani, mke wangu amezidi kunionea wivu hadi nakosa raha.

Nikiwa kazini anasema nipo na wanawake zangu, nikiwa na washikaji anasema wananitafutia wanawake. Hataki hata niimbe nyimbo zenye majina ya kike anasema ninawataja wanawake zangu kijanja.

Nifanyeje?

Hilo donda umelilea tangu likiwa changa sasa limekuwa dinda ndugu linakunukia mwenyewe, mwanamke ana wivu wa aina hiyo na bado hujachukua hatua za kuhakikisha unaukomesha.

Usiruhusu hali hiyo kwenye familia yako utakosa raha, hutakuwa na marafiki na atakufanya ujione mkosaji kila siku.

Kuanzia leo akikueleza kuwa upo na wanawake zao mjibu ndiyo, acha kujitetea kwa vitu ambavyo hujafanya, kama umeshatumia muda mwingi kumuelewesha haelewi ipo siku atawatukana watu unaofanya nao kazi ukiendelea kumlea.

Mueleze kabisa kuanzia sasa hutaki kusikia wivu usiokuwa na sababu. Akitaka akufuatilie ili aone hicho anachokifikiria. Kemea hii tabia kama unaamini anakushutumu kwa mambo usiyoyafanya.

Ndoa ni furaha katika maisha na ni faraja kwa familia, kwa maisha hayo mnayoishi hizi maana zote zitapotea, atakufarakanisha na watu. Usiruhusu hali hiyo.

Kila tunalojadili anamwambia mama yake

Mke wangu ananikera kiasi nashindwa la kufanya.

Kila ninachozungumza naye anakwenda kumwambia mama yake na kumtaka ushauri akikataliwa huko ujue hicho kitu hakitafanyika na atasema hata mama yake alisema hakifai.

Nifanye Anti au nimuache?

Masikini umeoa msungo!

Usijali dawa yake ni kumueleza bayana kama tabia hiyo inakukera. Usimwambie peke yake mwite shangazi yake au bibi yake kama wapo uwashirikishe katika hilo ili wamuelimishe maana ya kuwa na kifua cha mbele na nyuma.

Anahitaji kuelekezwa kwa nini nyumba ina kuta nne, ulipomuoa walisahau kumwambia.

Kumuacha siyo suluhisho washirikishe watu wengine kulimaliza, mtume bibi yako, msimamizi wenu wa ndoa, somo yenu akazungumze na mama yake pia na amkanye kuingilia mipango ya mwanaye na mumewe.

Post a Comment

0 Comments