MABINTI WANAOFANANA KUTOKA KATIKA FAMILIA TOFAUTI WANAVYOTIKISA KENYA

Mabinti pacha wa Kakamega nchini Kenya, Sharon na Mellon wanadaiwa kutenganishwa tangu mwaka 1999 baada ya kuzaliwa katika Hospitali Kuu ya Kakamega nchini humo. Picha na Mtandao 

Dar es Salaam. Mabinti, Sharon na Melon (19), wamekuwa gumzo nchini Kenya kutokana na kufanana kwa kila kitu kama walivyo pacha, lakini wao ni kutoka kwa baba na mama tofauti.

Ajabu ni kwamba, hata wazazi wao hakuna anayejua nini kilitokea hadi ikawa hivyo.

Mabinti hao, mmoja akiwa anaishi Kakagema na mwingine Nairobi, kwa mara ya kwanza walikutana kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook ambapo Melon alipata ujumbe wa mtu wanayefanana akimuomba urafiki.

“Nilipoona mtu anayefanana na mimi akiniomba urafiki nilishtuka, ila nikamkubalia na kuanza kumhoji maswali yeye ni nani akaniambia anaitwa Sharon na yeye akaniuliza mimi ni nani, kwa nini tunafanana,” anasema Melon.

Tangu hapo, mawasiliano kati yao yalianza hadi familia zao zikakutana na sasa kila mmoja anahitaji kujua hatima yake huku Sharon akionekana kuwa kwenye wakati mgumu zaidi.

“Mimi na Melon tunafanana kila kitu kuanzia kuzungumza, kutembea hadi kucheka kwetu mpaka uwezo wa kufikiri, yaani kuna wakati tunawaza vitu vinavyofanana,” anasema Sharon.

Rosemary Onyango ambaye ni mama wa Melon, anasema miaka 19 iliyopita alikwenda kujifungua akiwa na hali mbaya, akafanyiwa upasuaji, hivyo hajui kama alijifungua watoto wawili au watatu.

Anasema, baada ya kujifungua na kuamka kutoka usingizini aliambiwa amepata watoto wawili, mmoja akiwa na afya aliyekabidhiwa baada ya siku mbili huku mwingine akiwa kwenye uangalizi wa madaktari ndani ya chumba cha kunyonyeshea watoto. “Mtoto wangu mmoja alikaa huko kwa wiki tatu, nilikuwa naenda kumnyonyesha na kumuacha, alikuwa anasumbuliwa na tatizo la kupumua, sasa sijui mtu alitumia upenyo huo kubadilisha au nilipata watoto watatu mwingine akapewa mama mwingine,” anasema.

Akihojiwa na kituo cha Redio Jambo, Richard, baba wa Melon alielezea jinsi alivyoshtuka baada ya kukutana na Sharon akimfananisha na binti yake aliyekuwa amemuacha nyumbani Nairobi.

Anasema, “nilienda Kakamega nikamuona binti ambaye alifanana kabisa na mwanangu nikamuita Melon, akanishangaa na kunijibu kwamba yeye haitwi hivyo nikamshangaa inakuwaje mwanangu hanijui, nikampigia simu mama yake kumuuliza.”

“Mama (mkewe) akaniambia kwamba mtoto yupo nyumbani Nairobi na muda huo amekwenda kanisani, nikamwambia haiwezekani Melon nimemuona huku Kakamega, tukabishana na hata kufikia kugombana.”

Baada ya kufuatilia kwa muda mrefu na kuonana na mama yake Sharon, Richard alibaini kuwa mwanaye alizaliwa siku moja na Melon, na wote walizaliwa katika hospitali moja.

Richard anaeleza kuwa mkewe alijifungua kwa upasuaji na aliambiwa amepata watoto pacha wasiofanana ambao ni Melon na Melvis, na hawakuwahi kuhisi kama alikuwepo mtoto mwingine.

‘Pacha’ hao wako njiapanda ambapo Sharon anasema hataishi kwa amani kama ataishi katika familia tofauti na ile ya Melon. “Siwezi kuwa na amani kama nitakuwa na familia nyingine halafu wazazi wangu wapo sehemu nyingine, na vilevile itakuwa ngumu kwangu kuiacha familia niliyokaa nayo kwa miaka 19 nikiamini kwamba mimi ndiyo mtoto pekee wa kike. Kwa hiyo ikibainika Melon ni ndugu yangu nitachagua kuwa na familia zote mbili,” anasema.

Kilio kikubwa cha Melon ni kwa Hospitali Kuu ya Kakamega ambako ndiko walikozaliwa, akisema imewakosea na kuwasababisha walelewe kwenye familia tofauti.

Anasema, “kwa miaka 19 tumeumia na kuteseka wakati kuna ukweli unaohusu maisha yetu, kama ni kweli wametufanyia hivi maana yake wametukosea na ikitokea sisi siyo ndugu tutaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.”

Post a Comment

0 Comments