Katika maisha yetu ya kila siku neno fursa si geni sana masikioni mwetu. Neno hili watu wengi hulichukulia kama la kawaida sana lakini kiukweli kama utaweza kujua maana yake na kufanyia kazi lazima utaona mabadiliko makubwa katika maisha yako. Fursa nyingi hapa duniani zinakuwa haziko wazi au kwa maneno mengine zinakuwa zimejificha sana. Leo hii nataka nikushirikishe njia ambazo unaweza kuzitumia ili kuona fursa mbalimbali katika eneo lako.
Tambua fursa ikoje
Ili uweze kuona fursa katika maisha lazima ujue kwanza fursa ni nini na inafananaje. Kwa mfano unaweza ukawa unatafuta kitu fulani lakini kwenye akili yako lazima ujenge picha ya kile kitu unachokitaka. Kwa kufanya hivi inakuwa rahisi kwa mtu kujua ni nini hasa anakitaka na atumie mbinu gani na muda gani ili aweze kufanikisha.
Kuwa na njia mbalimbali za kukamilisha malengo.
Kuna msemo usemao usiweke mayai yote kwenye kapu moja. Kama unataka kuwa na fursa nyingi ,anza kufanya vitu vidogovidogo vingi na angalia ni kipi kinakuwa kikubwa. Kama kila kitu kitakuwa na mpango mmoja na hamna mipango mingine B,C,D au E basi utakuwa hatarini sana na pengine mpango A unaweza usifanikiwe.
Usidharau fursa ndogondogo
Watu wengi waliofanikiwa hapa duniani walianza kufanyia kazi fursa ndogondogo zilizojitokeza machoni mwao. Kwa kuanza na fursa ndogo inakifanya upate akili ya kupambana na kuona fursa kubwa. Unaweza ukawa na fursa ndogondogo tatu kwa wakati mmoja lakini mojawapo ndo ikakufaidisha na zile nyingine zikawa zimekuongezea maarifa ya kupambana.
Kuwa tayari
Ili uweze kuona fursa na kuinyakua lazima uwe na utayari wa kuipokea pindi inapojitokeza.
0 Comments