Tatizo la Kuchokana Kwenye Mapenzi

NI Ijumaa nyingine nzuri ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia. Hatuna cha kumlipa zaidi ya kushukuru kwa kusema ‘ASANTE’! Wiki iliyopita nilianza mada hii ambayo lengo lake ni kutafuta tiba ya tatizo hilo ambalo limezitikisa kapo nyingi. Tuliangalia vipengele mbalimbali kama namna ya kufanya mazungumzo na tabia za kila mmoja zinavyoweza kuchangia tatizo hili.

MAPENZI
Ni muhimu sana kwa wanandoa ili kuyaimarisha mapenzi yao yasiote mvi, kutamkiana hisia zao za kupendana bila utangulizi wowote. Kwa mwanaume au mwanamke kumwambia mwenzake NAKUPENDA, kuna athari nzuri katika nafsi kuliko hata ungemletea zawadi ya kitu cha gharama.

ZAWADI
Zawadi ni njia nzuri ya kudhihirisha mapenzi yako na nafasi ya mwenzako katika maisha yako na zawadi ambayo mtu huitoa kwa mwenzake bila utangulizi au mnasaba maalum, huleta athari njema na huimarisha mapenzi.

Na katika zoezi hili la kupeana zawadi, ni vema kila mmoja akaelewa anachokipenda mwengine ili zawadi iwe na athari inayotarajiwa na iwe ni zawadi maalum kwa mlengwa, isiwe zawadi ambayo mtoaji naye atafaidika na zawadi hiyo.

Kwa mfano, si vema kwa mwanaume kumletea mwanamke zawadi ya sufuria, microwave, pazia au dinner set. Hii haitaitwa zawadi, lakini ni juu yake kumletea manukato ayapendayo, hereni, bangili, mkufu au pete ya dhahabu na vitu ambavyo ni maalum kwa matumizi yake binafsi. Hali kadhalika kwa mwanamke kumzawadia mwanaume, achunge vigezo hivyo.

VYAKULA
Inaweza kushangaza kuwa ni vipi wapenzi wataalikana chakula wakati wenyewe ni lazima wale pamoja? Ni vema ikaeleweka kuwa, kubadili mazingira na kufanya vitu mahsusi kwa kushtukizana, huwafanya wapenzi kutozoeana na kuchokana, kwani maisha yenye mtindo na mtiririko mmoja kila siku, humfanya mtu kuyachoka.

Ni vema wanandoa na hasa mwanamke kuwa mbunifu katika kuyapaka rangi mpya maisha yao kwa kubuni vitu vitakavyotia ladha mpya katika nyumba, njia mojawapo ni hiyo ya kumualika chakula maalum mumewe peke yake na hata kama itamlazimu kununua au kuagiza aina tofauti ya chakula, basi afanye hivyo na ampe mwaliko mumewe wa kutokosa kuhudhuria katika mnasaba huo.

Aidha, mwanaume naye anaweza kumualika mkewe kwenye hoteli ya heshima kwa ajili ya mlo wa mchana au usiku na kupata nafasi ya kujikumbusha mambo mazuri yaliyopita.

NYUMBA
Wanawake wengi huwalalamikia wanaume wao kwa kutopenda kukaa nyumbani na badala yake, kumaliza muda wao kwenye migahawa na kwa marafiki zao.

Mke mwerevu huwa anafanya kila juhudi za kumnasa mumewe apende kukaa nyumbani wakati wa nafasi yake kwa kumbadilishia mazingira ya nyumba, kwani mazingira ya nyumba yanapokuwa ni yaleyale tangu ndoa ilipofungwa hadi wanakuwa na watoto watatu, kochi lipo palepale kama kisiki cha mti, saa ya ukutani tangu imetundikwa mpaka imeshikana na ukuta, mapazia yaleyale na kama yanabadilishwa, basi rangi ni zilezile, hali hii humfukuza mwanaume ndani ya nyumba na kumfanya arudi kuja kulala tu na huu ndiyo mwanzo wa kuchokana na kuichoka nyumba.

USAFI WA MWILI
Miongoni mwa mambo yanayokera kwa wapenzi ni uchafu wa mmoja wao. Uchafu ni sifa isiyovumilika hususan kwa mwanamke. Baadhi ya wanawake hudhani kuwa, manukato na vipodozi ndivyo usafi.

Utakuta anapitisha siku bila kuoga kikamilifu, bali anapitishapitisha maji na sabuni tu katika maeneo fulani kisha kujijaza manukato, losheni na mafuta mengine, bila kuelewa kuwa, anapokuwa karibu zaidi na mumewe, harufu ya asili hujitokeza na kuleta mchanganyiko wa harufu mbaya.

Hali kama hii si rahisi kwa mwanaume mstaarabu kuizungumzia kwa mpenzi wake, atakaa nayo na atavumilia, lakini mwisho wake ni kumchoka mwanamke wake. Wanaume nao hudhani kuwa, kwao wanaume ndiyo wamepewa kibali cha kuwa wachafu.

Kwa mfano, wanaume wengi huona ni jambo la kawaida kunuka jasho na wengine wana matatizo sugu ya kunuka miguu. Huu ni uchafu ambao hauvumiliki kwa mwanamke msafi.

Baadhi ya wanaume hawana vionjo katika mavazi yao na jinsi wanavyojiweka, jambo ambalo linaweza kumsababishia mwanamke maudhi na hata kujihisi aibu kunasibishwa na mpenzi wake huyo.

IBADA
Nguzo muhimu na mhimili wa maisha ya ndoa ni kumcha Mungu au Allah. Sala za usiku humkaribisha mja karibu zaidi na Mungu, hivyo wapenzi kuhimizana kufanya ibada hii pamoja, huwazidishia imani na mapenzi baina yao na kulifanya penzi lao kuwa imara zaidi kila kukicha.
Kwa leo ninaishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Post a Comment

0 Comments