
UNAPOZUN-GUMZIA suala la maumivu ya mapenzi, japokuwa huumiza sana hasa kama ulikuwa na mapenzi ya dhati na mwenzi wako na baadaye akaaamua kukugeuka, siyo suala geni hapa duniani. Unapolia leo kwa sababu ya mapenzi, elewa kwamba mamilioni ya watu wanalia kama wewe ingawa tunatofautiana namna ya kukabiliana na maumivu. Lakini cha kujiuliza ni je, mpenzi wako akikuumiza sana, ni sahihi kujiapiza kwamba hutapenda tena?
Ni sahihi kusema kwamba siku hizi hakuna mapenzi ya ukweli kwa sababu tu amekuumiza? Ni sahihi kusema wanaume wote wako hivyohivyo au wanawake wote ndivyo walivyo?
Ukweli ni kwamba, unapovunjika moyo haimaanishi kwamba huo ndiyo mwisho wako wa kupenda. Unapojiapiza kwamba hutapenda tena au hutamwamini mtu tena, ni makosa makubwa kwa sababu kama uliyekuwa naye ameshindwa kuiona thamani ya penzi lako, yupo ambaye atakuthamini na kukuheshimu. Kuna usemi maarufu kwamba mlango mmoja unapojifunga, mwingine huwa unafunguka muda huohuo lakini wengi wetu hupoteza muda mrefu kuutazama ule uliojifunga badala ya kuufuata ule uliofunguka.

Ukishaukubali ukweli, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupona majeraha ndani ya moyo wako na nakuhakikishia, hata kama ulimpenda vipi huyo uliyekuwa naye, kama amefikia hatua ya kukuumiza na kuuvunja moyo wako, hakuwa riziki yako, endelea kumuomba Mungu kwa sababu yupo ambaye ndiye haswa aliyepangwa kuwa wako.


0 Comments