WATAALAMU WATAJA SABABU KUU ZA MIMBA KUHARIBIKA

Mimba yenye wiki 28 au chini ya hapo huharibika au kutoka, hali hii kitaalamu inajulikana kama ‘miscarriage’ na kwa kawaida mtoto aliye tumboni katika umri huu hataweza kuishi nje ya tumbo la mama.

Zaidi ya asilimia 80 ya mimba huharibika katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito na baada ya miezi hiyo kupita, uwezekano wa mimba kuharibika hupungua.

Miaka ya hivi karibuni baadhi ya wanawake wamekuwa wakipata changamoto ya kuharibika kwa mimba mara kwa mara, hali inayosababisha baadhi yao kukosa matumaini ya kupata watoto.

Wataalamu wa afya wameweka wazi sababu zinazochangia mimba kuharibika, huku wakitaja matumizi ya pombe, sigara na hewa chafu kuwa miongoni mwa vyanzo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Colman Living anasema sababu zipo nyingi kulingana na umri wa mimba husika.

Anasema mimba imegawanyika katika vipindi vitatu, miezi mitatu ya mwanzo ambayo mtoto hujishikiza, miezi mitatu ya katikati na ile mitatu ya mwishoni kukamilisha miezi tisa.

Dk Colman anasema kila kipindi kina sababu zake, huku akitaja sababu kubwa kuwepo katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza.

“Uharibikaji wa mimba tunahesabu katika vipindi vitatu vilivyogawanyika kwa miezi tisa ya ujauzito. Kila kipindi kina sababu zake,” anasema Dk Colman.

Pia, anasema katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo kuna sababu zaidi ya tatu ambazo husababisha mimba kuharibika.

Anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na homoni kutokuwa sawa suala hilo husababisha mimba kutoendelea kukua vizuri na mambo mengi yanaweza kutokea ikiwemo mimba kutoka.

“Homoni zinaposhindwa kuwa sawa husababisha mizizi kutojengeka vizuri ambayo ndiyo huzalisha kondo.”

Anasema vinasaba ni suala jingine ambalo ni kisababishi kikubwa cha mimba kutoka, “hasa tatizo hili huwa sababu kubwa ya kutoka kwa ujauzito au kuharibika na vinasaba vinaweza kuwa vya mama au baba.”

Dk Colman anataja sababu nyingine kuwa ni matumizi ya dawa kali bila ushauri wa daktari hasa dawa za antibiotiki, zinazotibu malaria katika umri huo wa mimba changa.

Anataja kipindi cha pili cha ujauzito kuwa ni kuanzia umri wa mimba ya miezi mitatu mpaka sita, mimba huhitaji kizazi kiwe na uwezo wa kuibeba bila kutetereka.

“Katika kipindi hiki mimba huanza kukua na hivyo huhitaji kizazi imara ambacho kitaweza kuibeba, wakati huu shingo ya kizazi inabidi iwe imekaza na kama imelegea mimba itaporomoka na wakati huu walio wengi mimba hutoka bila kusikia uchungu wowote,” anasema Dk Colman.

Anasema katika kipindi hicho maambukizi pia huchangia mimba nyingi kuharibika ikiwamo magonjwa ya zinaa na iwapo mama atakuwa na tatizo la kisukari au malaria kali.

Dk Colman anataja kipindi cha mwezi wa sita mpaka tisa kwamba ni kipindi cha mwisho cha ujauzito ambapo kuna mambo kadhaa pia huchangia mimba kutoka ikiwemo tatizo la shinikizo la damu au presha, magonjwa sugu ya mfumo wa mkojo (U.T.I) na matumizi ya holela ya dawa.

Wakati akitaja sababu hizo, Dk Colman anasema hewa chafu pia ina uwezo mkubwa wa kuchangia kutoka kwa ujauzito.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Japeth Shao anasema matatizo ya maumbile ya mtoto tumboni (genetic abnormalities) pia yanaweza kuwa sababu.

Post a Comment

0 Comments