NI Jumatatu nyingine tunakutana kwenye eneo letu la kupeana elimu ya uhusiano. Ulimwengu huu ni mzuri kama utampata mtu sahihi. Mtu ambaye mnapendana kwa dhati na hakuna hata mmoja wenu ambaye anamsumbua au kumyanyasa mwenzake. Kizazi cha sasa kimetawaliwa na ugomvi, usaliti, tamaa na kila aina ya mambo mabaya. Bahati mbaya sana hata wale walioko kwenye ndoa, wapo ambao wanatamani kutoka kutokana na matatizo au changamoto wanazokutana nazo. Inafika mahali watu wanapoteza kabisa ile hamu ya ndoa maana wanawake kwa wanaume wanasaliti. Wameifanya staili ya kutoka nje ya ndoa kwamba ni jambo la kawaida. Mwanamke anaridhika kabisa mumewe amsaliti, lakini asijue.
Vivyo hivyo kwa mwanaume, naye anakuambia hakuna mwanamke wa kwako peke yako. Anaamini mwanamke ni kiumbe dhaifu, ni kiumbe ambaye kushawishika kwa mambo madogo ni jambo la kawaida kabisa hivyo muda wowote anaweza kudanganywa na akaingia mkenge. Ndugu zangu, akili zetu tunavyozirahisisha kuwaza haya tunakosea sana. Tunahalalisha upuuzi usiokuwa na maana wala afya katika ustawi wa uhusiano wetu na hata kizazi cha baadaye. Kurahisisha haya mambo ya uhusiano kwa jinsi tunavyofanya ndiyo maana tunashuhudia ndoa nyingi za sasa zikivunjika.
Mioyo yetu tumeifanya imekuwa miyepesi sana kukubaliana na suala la kuachana kuliko kitu kingine chochote kwa sababu hatujali, tunaona maisha yapo tu bila kujua tunajishushia heshima na kuharibu hata kizazi kinachokuja maana kitaona suala la kuchepuka ni halali, nao wataliiga.
Unashindwaje wewe kuishi na mtu ambaye mtazeeka pamoja? Mbona wazazi wetu waliweza, sisi tunakwama wapi? Ninachokiona mimi ni suala zima la kufanya mambo yaende kihuni, kufanya uhuni na kuwarithisha watoto wetu uhuni.
Ndiyo maana leo nimekuja na mada hii kama inavyojieleza, mnapokuwa kwenye hatua ya awali ni vizuri sana mkalielewa hili somo. Mapenzi ni hisia, zinapokuwa zinaenda sawa hakika mtaishi vizuri sana, lakini mambo yanapokuwa tofauti, mtateseka. Unaweza kuwa na dhamira njema kabisa ya kufanya maisha na huyo mwenza wako, lakini mwisho wa siku ukajikuta unapoteza muda kama yule mtu wako hamuendani. Siku zote wewe ambaye unakuwa unamhitaji zaidi mwenzako huwa unakuwa na matumaini kwamba ipo siku atabadilika.
Mwenzako atakufanyia vituko vya kila aina kiasi ambacho katika hali ya kawaida ni ngumu kuvumilia, lakini wewe upo unavumilia. Sasa basi, kwa nini kujipa presha ya muda mrefu mkiwa kwenye hatua ya awali?
Umeshaona kabisa kwamba huyu mtu hatuendani, ameshaonesha kabisa hana mpango na wewe wa nini kumng’ang’ania? Unataka kuwa na mtu wa kulia, kuumizwa moyo miaka yako yote? Nimekuwa nikieleza sana kuhusu jambo hili, fanya kila linalowezekana, lakini ifike wakati ufanye uamuzi mgumu.
Kama unaona vituko vimekuwa vingi, manyanyaso, dharau na mambo mengine mengi ya maudhi, basi amua kutoka kwenye uhusiano huo. Sijasema usiwe mvumilivu, la hasha, kuwa mvumilivu kwa kiasi cha kutosha, lakini unapoona matatizo yamekuwa makubwa zaidi kuliko furaha katika hatua za mwanzoni, jiondoe.
Kila unalofanya mwenzako analiona baya, anakujibu vibaya au anakuonesha kabisa kwamba hakutaki wewe wa nini? Huyo hamuiendani, yawezekana alikutamani kwa muda sasa hamu yake imeisha hivyo hana mpango na wewe.
Kataa utumwa wa mapenzi mapema ukiwa kwenye hatua za awali. Yupo mtu kwa ajili yako ambaye mtakuja kukutana na mtaendana, mtafurahia maisha ya uhusiano bila kuangalia ni lini na wapi ila wakati wako upo
0 Comments