NA CHRISTIAN BWAYA
UMEWAHI kujaribu kutafuta mwafaka na mtu ukiwa kwenye hali ya hasira? Fikiria kuna kitu amefanya umekasirika na unajisikia msukumo wa kuzungumza kuondoa tofauti zenu. Unadhani mtaelewana? Ingawa najua inategemea na maumbile na hulka yako, lakini uwezekano wa kuelewana ni finyu.
Hasira inaweza kukufanya ukawa mtu mwingine. Ufahamu wako unabadilika. Hufikiri tena kwa utulivu. Unakosa uwezo wa kuvaa viatu vya mwenzako. Katika mazingira kama haya, wahenga walisema hasira hasara.
Unajiuliza kwanini hasira ilete hasara? Kwanini ni vigumu kutenda haki ukiwa kwenye hali ya hasira? Kimaumbile hasira ni silaha inayotuwezesha kupambana tunapokuwa kwenye nyakati za dharura tunazolazimika kujihami. Hasira inakuwezesha kufanya uamuzi usio wa kawaida unapojitetea. Uamuzi ambao laiti ungekuwa kwenye hali ya kawaida, usingefikiri kuufanya, unaweza kuyafanya ukiwa na hasira.
Hasira husisimua ule uthubutu unaoishi ndani ya mtu. Ukikasirika vya kutosha, kwa mfano, hutoogopa tena. Mwili wako unasisimka, unajwa mhemko, unahema kwa kasi, mzunguko wa damu unaongezeka, kukuandaa kupambana. Ukishakasirika unakuwa huna kizuizi cha kufanya chochote kinachokwaza maslahi yako. Ukiwa na hasira, unakuwa na mhemko wa kulinda heshima, usalama na hadhi yako kwa gharama yoyote.
Hujali tena. Usipojizuia unaweza kusema maneno ambayo kwa hali ya kawaida usingethubutu kuyasema. Unaweza kutumia nguvu kupambana.
Ikifikia hapa tunasema hasira inakufanya ushindwe kuudhibiti ule ubinafsi unaoishi ndani yako. Unaweza kulopoka, kusimanga, hata kutukana kwa sababu unachokifikiria ni wewe na kile unachokitaka. Maumivu ya mwenzako, kudhalilika kwa mwenzako na namna nyingine za kisasi.
Bahati mbaya, katika mazingira haya ya hasira, ni vigumu kuwajibika. Hata kama kwa kiasi fulani unaweza kuwa umechangia hali ya kutokuelewana, ukishakasirika, fahamu zako zinakuelekeza kupambana.
Huwezi tena kufikiri namna gani na wewe uwajibike kwa makosa yako. Huwezi tena kufikiri amani kati yenu. Huna tena muda wa kufikiri mahitaji ya mwenzako. Katika mazingira kama haya ni vigumu kupata suluhu inayotegemea uwezo wa nyie wawili kwenda nje ya heshima zenu binafsi.
Katika utafiti mmoja, wanasaikolojia walichunguza tofauti ya ugomvi wa watu waliokuwa wamepandwa hasira na wale waliokuwa na kiwango cha chini cha hasira. Kiwango chao cha hasira kilipimwa kwa vifaa maalumu.
Washiriki wa utafiti huo waliwekewa mazingira yaliyopandisha hasira zao na kuwagombanisha na kisha walitazamwa namna walivyojaribu kutatua tofauti zao.
Matokeo yalionesha kuwa katika mazingira ambayo wanandoa walikuwa wametibuka na hasira, ilikuwa kawaida kwao kufokeana, kurushiana maneno, kushambuliana na matokeo yake hawakuweza kuelewana na kumaliza tofauti zao kwa urahisi.
Ingawa kuna nyakati ilionekana kuwa wanandoa hawa waliopandwa jazba waliweza kumaliza tofauti zao, sababu kubwa ilikuwa ama mmoja kuamua kukata tamaa kwa kunyamaza au wote wawili kuamua kujiondoa kwenye mazungumzo yaliyokuza tofauti zao.
Tofauti ilionekana pale ambapo wanandoa hawa walipopunguza hasira. Kwa mfano, baada ya kujiridhisha kuwa wote pamoja au mmoja wapo amekasirika, mtafiti angeweza kumwita mmoja wapo na kufanya naye mazungumzo mengine kwa muda fulani na kisha kumruhusu akaungane na mwenzake. Matokeo yalionesha kuwa mwanandoa huyu alipokutana na mwenzake baadae hasira zilipokuwa zimepoa, tofauti ilikuwa bayana.
Mazungumzo yalifanyika kwa utulivu zaidi, walisikilizana kuliko kushambulia, hawakufoka na kukemea, ukilinganisha na pale wanapokuwa wanagombana wakiwa kwenye kilele cha hasira.
Pia hata pale ambapo ilikuwa vigumu wanandoa hawa kuondoa tofauti zao, bado waliweza kuzungumza kwa namna inayoonesha ukomavu na uelewa wa hisia za mwingine. Tafsiri ya utafiti huu inaakisi kile tunachokifahamu sote.
Kwamba unapozungumza na mwenzako katika hali ambayo wote wawili hamjapandwa na hasira, uwezekano ni mkubwa mtaelewana kwa urahisi kuliko kuzungumza mnapokuwa mmekasirika.
Utafiti huu unatufundisha nini? Kwanza, usifanye majadiliano na mtu aliyekasirika. Kama tulivyodokeza hapo awali, katika hali ya hasira huwezi kufikiri sawa sawa. Hasira zina tabia ya kuhemsha mwili wako kwa namna inayokuandaa kujitetea.
Ikiwa lengo lako ni kufanya mazungumzo yenye amani yanayolenga kupata suluhu, ni vizuri kukwepa vishawishi vya kutoa maelezo kwa mtu mwenye hasira.
Lakini pili, subiri urudi kwenye hali ya kawaida kabla ya kufanya mazungumzo na mwenzako. Jizuie kuzungumza, kwa kuvuta pumzi, ondoka eneo husika, nenda mahali utulie na kulia ikiwa mazingira yanaruhusu. Ukishajiridhisha kuwa mhemko wa hasira umepoa, nenda mtafute mwenzako mzungumze. Uwezekano wa kuelewana utakuwa mkubwa zaidi.
0 Comments