NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku, mada ambayo ningependa tuijadili ni kama inavyojieleza hapo juu.
Upo usemi kwamba kosea mambo yote lakini usikosee mtu wa kuingia naye kwenye ndoa. Bahati mbaya ni kwamba, wengi wanafanya makosa makubwa katika uamuzi wa nani wa kuanzisha naye uhusiano wa kudumu na ndiyo maana maumivu ya mapenzi yanazidi kuwa makubwa kila kukicha.
Nimewahi kulieleza hili siku za nyuma kwamba watu wengi wanakosea kwa kujiwekea matarajio makubwa ndani ya vichwa vyao kabla ya kuingia kwenye uhusiano na mtu.
Ukimuuliza mwanamke yeyote anatamani kuingia katika ndoa na mwanaume wa aina gani, atakujibu mwanaume mwenye mvuto, ‘handsome’, mwenye ‘six pack’, mwenye kazi inayoeleweka, mwenye fedha na sifa nyingine
kedekede! Wakati huohuo, huyu anayeweka vigezo hivi unakuta kiuhalisia ni mtu wa kawaida kabisa na anaishi maisha ya kawaida kabisa.
Mtu wa namna hii, kwa sababu tayari ameshajiwekea matarajio makubwa ndani ya kichwa chake, ambayo hayaendani na hali halisi, ataendelea kupishana na watu ambao alitakiwa kuwapa nafasi, siku zitaenda, akija kushtuka umri umeenda na mwisho anaamua kudondokea kwa yeyote atakayejitokeza.
Mwanaume naye ukimuuliza anatamani kuingia katika ndoa na mwanamke wa aina gani, atakujibu mwanamke mrembo, mzuri wa sura na umbo, ‘aliyefungashia’, anayetokea kwenye familia inayojiweza kiuchumi, mwenye kazi na sifa nyingine kedekede. Lakini utashangaa huyu anayeweka viwango hivi kichwani mwake, hana kazi yoyote zaidi ya maana zaidi ya kubangaiza na kushinda kijiweni akicheza drafti kutwa nzima.
Jambo ambalo unatakiwa kulitambua, ni makosa makubwa ‘kumjaji’ mtu kwa mwonekano wake wa nje. Sifa za nje za mtu zisikudanganye, unaweza kudanganyika na urembo au utanashati wa nje ukakurupuka kuingia kwenye ndoa lakini kumbe ndani ni mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo! Kwa hiyo jambo la kwanza, kabla ya kuamua nani unataka awe wako wa milele, ni vizuri kwanza kupata muda wa kutosha wa kumchunguza mwenendo wake. Isiwe tu kwa sababu umetongozwa na mwanaume ambaye ulikuwa unamuota maishani mwako ukaingia kichwakichwa ukiamini umeshapata mume sahihi.
Au isiwe kwa sababu umefanikiwa kumnasa mwanamke uliyekuwa unamuwaza kwenye kichwa chako, basi ukaingia kichwakichwa na kutangaza ndoa, fanya makosa yote lakini usikosee mtu wa kuingia naye kwenye ndoa. Ukishakuwa unayatazama mambo kwa jicho la tatu kama hivi, utagundua kwamba kumbe vigezo ulivyojiwekea kichwani mwako havina maana yoyote.
Utagundua kwamba kumbe mkeo mtarajiwa ni yule dada uliyekuwa unamchukulia poa siku zote kwa sababu hana sura nzuri au hajafungashia kama ulivyokuwa unajidanganya lakini ana tabia nzuri, anajiheshimu, anajituma, mpole na sifa nyingine kibao ambazo kimsingi ndizo anazotakiwa kuwa nazo mke.
Kama wewe ni mwanamke, utagundua kwamba yule jamaa ambaye alikuwa ‘anakufukuzia’ kwa muda mrefu lakini ukawa unampuuzia kwa sababu amechoka kimaisha, anahangaika na vibarua na vikazi vidogovidogo vya kumpatia ridhiki, hana mvuto kama uliokuwa unaufikiria mwanzo, ndiyo hasa anayefaa kuwa mumeo.
Sifa za mwanaume anayepaswa kuwa mumeo, ni tofauti kabisa na zile wanawake wengi wanazozifikiria ndani ya vichwa vyao, na sifa za wanawake ‘wife materials’ ni tofauti kabisa na zile wanaume wengi wanazozifikiria, na kibaya zaidi sifa hizi huwa hazionekani kwa urahisi kwa nje mpaka utakapoamua kumfuatilia mhusika. Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii.
0 Comments