KUNA wakati inatokea kwenye uhusiano, mmoja wao (hasa mwanamke) akadhauriwa na mpenzi wake na kuonekana wa kawaida tu. Athari kubwa zaidi katika kuonekana wa kawaida au kudharauliwa ni kuachana wakati wowote – kwa ghafla.
Mara nyingi tendo la kuachana kwa wenzi wa aina hii huwa hakuna sababu kubwa sana. Jambo dogo tu linaweza kukatisha uhusiano lakini kumbe ndani kuna siri nyingine kubwa zaidi; kushuka thamani.
Marafiki zangu, wakati uhusiano unapofikia kwenye hatua hii huwa ni hatari sana na uamuzi wa kuachana hupewa nafasi kubwa zaidi kwa pande zote. Habari mbaya zaidi ni kwamba, hata kama wahusika watakuwa wana ndoa, huwa si kigezo kikubwa sana kwao, badala yake hufikiria kuachana kama ndiyo kitulizo cha mioyo yao.
HEBU TUJIFUNZE
Nazungumzia kuhusu thamani. Ni somo linalohitaji utulivu mkubwa wa akili na utayari wa ubongo. Ninaposema kushuka thamani namaanisha kupungua kwa umuhimu au kupotea kabisa. Kubwa ambalo utakuwa umebaki nalo (labda) ni kukutana kwa ajili ya mapenzi tu. Hawezi kukushirikisha katika mambo yake kwa sababu huna thamani kwake.
Kwa bahati mbaya ni kwamba, ukishushwa thamani, mara nyingi unaweza usigundue hilo hivyo kuendelea na maisha kama kawaida katika mtindo ambao kumbe tayari mwenzako ameshakubadilisha daraja.
UTAJUAJE KUWA UMESHUSHWA THAMANI?
Ninachohitaji kuzungumza nanyi marafiki zangu ni namna ya kujipandisha thamani ili mpenzi wako asikuchoke wala kukushusha au kukuona wa kawaida. Kila wakati akuone wa muhimu na akufanye namba moja katika maisha yake. Kabla sijafika hapo nataka kwanza mfahamu dalili atakazozionyesha mwenzako zinazoashiria kuwa amekushusha thamani yako kwake.
(i) Mawasiliano hupungua
Hapa inategemea na kasi ya mawasiliano mliyokuwa nayo mwanzo lakini kwa kiwango chochote kile huanza kupungua. Kama alikuwa na kawaida ya kuwasiliana nawe mara kwa mara akikueleza mambo mbalimbali – hata madogo tu, kuhusu mwenendo wa siku yake, ataacha.
(ii) Msiri kupitiliza
Kulingana na kiwango cha uhusiano wenu, ataanza kuwa msiri kwa baadhi ya mambo yake. Hata kama anafanya jambo fulani zuri kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye, hatakuambia. Unaweza kushtukia tu kusikia kwa watu kuwa mwenzako ameagiza gari au amenunua kiwanja mahali na pengine ameshaanza ujenzi bila kukujulisha.
(iii) Hukupuuza
Kama awali alikuwa na kawaida ya kukusikiliza, sasa ataanza kukupuuza. Unaweza kumwambia jambo lenye manufaa makubwa kwenu lakini asilichukulie umakini. Hii ni dalili kwamba wewe huna thamani kwake.
SIFA ZAIDI…
Kama umeshushwa thamani unakuwa kwenye hatari ya kuachwa. Hata kama mwenzako alikuwa ameshafikiria suala la kuingia kwenye ndoa lakini kwa sababu ameshakushusha thamani ndoa inaweza kuyeyuka.
Ukiwa kwenye ndoa ni hatari zaidi maana mwenzako hukuchukulia wa kawaida – mazoea huzidi na hapo ndipo uhitaji wa kuwa na mwingine wa pembeni unapoanza. Haoni cha muhimu tena kwako, ndiyo maana wazo hilo huvamia ubongo wake kwa kasi.
Itafikia hatua, kama upo ndani ya ndoa, mwenzako atagoma kuongozana na wewe na kama ikitokea hivyo mkikutana na rafiki zake njiani hatakutambulisha. Hisia kwamba hamuendani humwingia.
UNAFANYAJE SASA?
Kubwa unalotakiwa kufahamu rafiki yangu mpendwa, suala la kupanda au kushuka thamani lipo mikononi mwako. Yapo mambo ambayo ukiyazingatia, mwenzako hawezi kukuchoka na kufikia hatua ya kukushusha thamani.
Tayari tumeshaona athari zake lakini hapa sasa nataka kukupa mbinu ambazo ukiwa nazo makini basi itakuwa rahisi kwako kubaki namba moja na mtu muhimu zaidi (ndiyo inavyotakiwa kuwa) kwa mpenzi wako maana ni haki yako.
0 Comments