AMANI ya kweli katika uhusiano katu haiwezi kupatikana ikiwa wahusika hawajafahamu wanatakiwa kuishi katika mtindo upi wa maisha. Kila mmoja anatakiwa kufahamu kuwa katika mahusiano na fulani si tiketi ya moja kwa moja ya kuwa na furaha na amani.
Kwani wangapi wako katika mapenzi na bado kila siku wanalia na wanateseka kwa upweke? Kwani wangapi wako katika mapenzi na badala ya kupeana raha na amani, wao wanapeana shida na mateso? Unajua tatizo ni nini? Shida kubwa ni mfumo wa maisha ambao wameuchagua.
Ili amani na furaha iweze kutamalaki kwa wahusika ni muhimu wakajua kuwa urafiki baina yao ni kitu muhimu sana. Yaani badala tu ya wahusika kujiona ni wapenzi ila pia ni manufaa sana kila mmoja akamwona mwenzake kama rafiki pia.
Urafiki una faida kubwa katika mapenzi. Moja kati ya faida kubwa ni kuwa kila mmoja hatakuwa na uwezo wa kumchoka mwenzake kiurahisi kutokana na mtindo wa maisha ya urafiki ulivyo.
Watu wakiwa wanajiona wapenzi zaidi kuliko hata kuwa marafiki, ni wazi muda mwingi watakapokuwa wakikutana watakuwa wanazungumzia mahusiano yao labda na matatizo yao. Hali hii ikizidi, mmoja kati ya wahusika ama wote wanaweza kujikuta wanaboreka na hali hii. Hii ni kutokana na asili ya binadamu akiona kitu ama kukisikia mara nyingi ubongo wake hukikariri na kuona hakina umuhimu sana.
Ila kama wakiwa marafiki wapenzi si kila muda wanaweza kuzungumzia mapenzi tu, hapana. Kutakuwa na muda wakutaniana, kubishana kiasi katika hali ya kufurahisha na hata wakati mwingine kuanzisha mada zinazoweza kuwachemsha wote wawili. Hali hii ina faida sana kwa wapenzi.
Hali hii inawajenga na inafanya watamani kila muda kuonana kwa sababu kati yao kuna mengi ya kufanya na si kuzungumzia mapenzi na migogoro yao tu, ila pia rafiki mpenzi faida yake nyingine ni kila mmoja kuwa huru na mwenzake.
Mahusiano mengi yamekosa amani na furaha kwa sababu wahusika hawaambiani ukweli. Na hawaambiani ukweli kwa sababu ya mtindo wa maisha ambao wamechagua kuishi.
Mmoja anaweza kuwa hafurahishwi na aina ya vitu anavyofanya ama anavyoongea mwingine ila kutokana na mtindo wao wa kuishi kama wapenzi zaidi na si kama marafiki unakuta anaogopa kumwambia mwenzake abadilike kwa sababu anahofia kumkera. Hii ni sumu mbaya katika mapenzi.
Kwa sababu wakati mmoja anahofia kumkera mwenzake kwa sababu ya kauli atakayomwambia yeye atakuwa anakereka na kwa sababu binadamu si kiumbe aliyeumbwa kwa ajili ya shida basi anaweza kujikuta baadaye akifanya uamuzi wa kijinga zaidi na kuhatarisha hali ya usalama katika uhusiano wao.
Wewe na mpenzi wako ni marafiki ama ni wapenzi tu? Amani na furaha katika mahusiano si kitu cha bahati mbaya ila ni kitu kinachotokea kutokana na aina ya mfumo wa maisha wahusika wanaoishi.
Nimewahi kupata kesi ya mwanamke akilalamika kuwa mume wake hakidhi haja yake ya kimwili vizuri. Nilipomhoji kama amewahi kukaa na mume wake na kuzungumzia suala hilo alisema kuwa anaogopa kumkera kwa maana wanaheshimiana sana.
Nilishtuka. Kwani kuheshimiana kunaingiliana vipi na kuambiana ukweli unaojenga? Kama yeye mke wake anashindwa kumwambia mume wake kuwa hamkidhi haja yake ya kimwili mume atajirekebisha vipi na matokeo ya kutomwambia yatakuwa nini?
Wengi wanateseka katika mapenzi si kwa sababu wamepangiwa hivyo hapana, ila inakuwa hivyo kwa sababu ya mtindo wao wa kimaisha.
Katika tathmini ya kina niliyofanya juu ya faida na hasara ya kuwa katika mahusiano yenye ladha ya urafiki ni kuwa kuna faida tupu ya mtindo huu wa mahusiano kuliko kuwa katika mahusiano yenye harufu ya mapenzi pekee.
Maisha ya kiuhusiano ili yaweze kuleta hamasa ni lazima wahusika wafurahi wakiwa pamoja na watamaniane kila muda, bahati mbaya hali hii haiwezi kutokea abadani kama furaha yao inategemea tu katika mazungumzo ya kimapenzi au katika mkutano wao wa faragha pekee.
Watu wengi wanashindwa kuwa wabunifu kwa wapenzi wao kwa sababu hakuna urafiki ndani yao. Kama kungekuwa na urafiki wangeweza kuambiana mambo mengi bila kuhofia kukwazana kwa sababu wanakuwa na mazoea halisi na si yale yanayozaliwa kutokana na msukumo wa mahusiano pekee.
Wale wanaofurahia mapenzi kiuhalisia ni wale walioko katika furaha halisi ya urafiki wa mapenzi. Hii imegawanyika katika pande mbili.
Wapo wale walioanza kuwa marafiki kwanza kisha wakawa wapenzi baadaye. Faida ya hawa ni kuwa waliweza kuwajua wenzao mapema na kuwasoma kabla ya kuingia katika mapenzi. Faida yake hili ni kuwa wahusika wanakuwa wametambua upungufu na matatizo yao hivyo hata wakiingia katika mahusiano kunakuwa hakuna kipya cha kuogofya miongoni mwao.
Mahusiano ya namna hii huleta amani na furaha sana kwa sababu mengi ya kila mmoja yanakuwa yanatambulika na wahusika wote. Hivyo ile tabai yako ya uchafu, wivu na kauchoyo mhusika anakuwa anakajua hivyo anapokuwa na wewe katika mahusiano anajua ni mtindo gani wa maisha utafaa katika kuleta mabadiliko ya tabia yako.
Ila hali hii haileti uhakika wa moja kwa moja kuwa wahusika hawatakosana. Hapana. Urafiki na mapenzi kuna tofauti yake. Hivyo kuna mengi mapya tegemea kuyaona wakati mkiwa katika mapenzi ambayo hamjayaona katika urafiki wa kawaida japo haitakuwa shida sana kushughulika nayo kutokana na mtindo wa urafiki uliopo kati yenu.
Pia urafiki katika mapenzi unaweza kuzaliwa wahusika wakiwa tayari katika mahusiano. Yaani baada ya kuwa pamoja wakaamua kuwa waishi mtindo wa kiurafiki, yaani wataniane, wazungumzie mambo tofauti na mapezi yao na kila mmoja awe huru kumjua vizuri mwenzake na kuendana naye kutokana na namna alivyo.
Chanzo Bingwa
0 Comments