UKIKOSEA NAMNA YA KUANZISHA UHUSIANO, IMEKULA KWAKO!



BROTHERS and sisters tunakutana tena kwenye ukurasa wetu ambao tunajadiliana kuhusu uhusiano. Naamini kila unaposoma hapa, kuna kitu unajifunza.  Leo nataka tujadili kuhusu namna ambavyo watu wengi hufanya makosa wakati wa mwanzo wanapoanzisha uhusiano, mwisho wanakuja kugombana na kuvunja uhusiano katika wakati ambao mmoja wao anakuwa na matarajio makubwa kwenye penzi hilo.
Kabla ya kwenda mbali, tutajifunza kitu kupitia kisa kifuatacho kutoka kwa msomaji mmoja aliyenitaka ushauri.
KUTOKA KWA MSOMAJI
“Kaka Shaluwa naomba msaada wako, mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 30. Nina mpenzi wangu ambaye nimekuwa naye kwa muda mrefu, hadi kufikia sasa nimeshika ujauzito wake. “Lakini nimelazimika kurudi kijijini kwetu huku Tanga, kutokana na kupata matatizo ya kiafya. Lakini tangu nimemweleza huyo bwana kuhusu ujauzito, amekuwa haeleweki, pia hapokei simu zangu siku hizi nikimpigia. Naomba ushauri wako.”
Hayo ndiyo aliyonieleza msomaji wetu huyo. Baada ya maelezo yake, nilimwuliza maswali kadhaa. Majibu ya maswali yangu ndiyo yaliyozalisha mada hii, maana niligundua kitu kimoja tu, toka kwake. Walianza uhusiano wao vibaya.
UHUSIANO NA  MUME WA MTU
Katika mazungumzo yetu, alisema mwanaume huyo ni mume wa mtu. Nikamwuliza alikuja kugundua hilo baadaye au alifahamu tangu mwanzo wa uhusiano wao, akasema alimwambia mwanzo na waliridhia.
Nikamwuliza walikubaliana kuzaa kwenye uhusiano wao au imetokea kwa bahati mbaya, akasema ni bahati mbaya! Lakini anadai walikubaliana angemuoa mke wa pili, kwa sababu dini ya jamaa yake huyo inaruhusu hilo. Nilizungumza naye mengi, ambayo naamini kama akiyafuata yanaweza kupunguza tatizo lake, maana kwa namna mambo alivyonieleza siyo ya kumaliza, bali kupunguza tu.
TATIZO NI MWANZO
Marafiki ni muhimu sana kuwa makini na mwanzo. Unapokutana na mtu leo hii kuanzisha naye uhusiano, lazima umjue vizuri. Lazima umchunguze vya kutosha. Ni nani, anatokea wapi, alihusiana na nani nk. Lakini lazima kujua hali yake ya uhusiano ya wakati unaanzisha naye mapenzi. Ujue nia yake kwako ni nini na uwe tayari na mtakayokubaliana.
Siyo sahihi kuwa na uhusiano na mtu ambaye ana ndoa yake, lakini ikiwa umeona ni sahihi, ujue kuwa unaanzisha uhusiano ambao hakuna matunda hapo baadaye. Ujue haiwezekani kuingia kweye ndoa kwa sababu mwenzako ameshaoa/kuolewa. Uwe na uhakika kuwa umeingia kwenye uhusiano ambao wewe unakwenda kuwa msindikizaji mpaka mwisho.
KUHUSU DINI
Lazima ujue dini ya mwenzako na muwe radhi pamoja. Haishauriwi kuendeleza uhusiano hadi unafikia mahali umekomaa, mnapaswa kuanza kufikiria kuhusu ndoa, ndiyo mnakuja kuibua suala la dini.
Hayo ni mambo ya kuyajadili mapema kabisa. Inashauriwa kuwa na imani moja ya dini. Lakini inawezekana mkazungumza na mkakubaliana mmoja kufuata imani ya mwenzake. Suala hili lisiwe la mwisho kujadiliwa.
HISTORIA
Mwulize mwenzako vizuri na awe mkweli kwako kuhusu historia yake ya uhusiano huko nyuma. Nawe pia unapaswa kuwa wazi kwa mwenzako kuhusu mapito yako.
Inawezekana una watoto au mtoto kabla ya kukutana naye. Mweleze ukweli, kadhalika naye akueleze ukweli kuhusu hilo. Ukweli utakufanya uamue kunyoa au kusuka. Itakuwa jambo la kushangaza, unaingia kwenye uhusiano na mtu kiasi cha kufikiria kufunga ndoa, halafu unakuja kugundua kuwa mwenzako ana watoto aliozaa na wengine kabla ya kukutana na wewe.
Au labda wewe una watoto, umekaa kimya, inafikia mmekaribia kufunga ndoa, ndiyo unakuja kueleza kuwa una mtoto au watoto. Siyo sahihi. Hapo mnaweza kuibua ugomvi ambao mwisho wake hauwezi kuwa mzuri.
Uhusiano wenye afya ni ule unaotawaliwa na ukweli. Simama katika ukweli kwa kumweleza mwenzako ukweli tangu mwanzo wa uhusiano wenu. Nyote mkifanya hivyo, mtajenga uhusiano mzuri wenye afya. Nasisitiza, zingatieni sana kuwa na mwanzo mzuri!
Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Post a Comment

0 Comments