UNAMSAIDIAJE MWENZA WAKO KUBADILIKA??

DUNIA ya sasa kumpata mtu mwenye mapenzi ya dhati, mwenye moyo wenye huruma, anayejali na ambaye ana hofu ya Mungu kidogo huwa ni ngumu. Wengi ni matapeli, wengi si waaminifu. Mtu anakuwa na wewe lakini anakuwa na wengine wengi tu. Haheshimu hisia zako labda pengine wewe umejitoa kwa moyo wako wote, unaamini upo kwenye mikono salama kumbe wapi bwana unaibiwa.

Hii inauma sana, watu wa aina hii ni hatari na hawafai kabisa kwenye ustawi wa mapenzi. Ukimgundua mapema mtu wa aina hii ni vyema kumuonesha mlango wa kutokea. Mara kadhaa nimekuwa nikisema, usikubali kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye huna imani naye, kama mtu unaona anafanya mambo ambayo yanakufanya usimuamini ni hatari kuendelea naye.

MAMBO YA KUZINGATIA

Unapokuwa unaanzisha uhusiano unapaswa kuwa makini sana katika suala zima la tabia njema, upendo, wa dhati, mwaminifu na hofu ya Mungu.

Hivyo vitu viwe mwongozo kwako katika kusaka mwenza sahihi wa maisha. Lakini pamoja na hayo yote, inatupasa pia tutambue kuwa tunapaswa kujua kuhusu suala la kumbadilisha mwenzako ambaye unakutana naye. Ukiwa na moyo mwepesi wa kukata tamaa haraka, unaweza kuwa bingwa wa kubadilisha wapenzi.

Leo utakuwa na huyu kwa sababu umeona ana sifa hii, mnavyozidi kuishi unagundua ana kasoro fulani basi unamuacha na kuhamia kwa mwingine. Huko unakohamia nako unakuta naye ana sifa fulani lakini kwa upande mwingine ana tatizo fulani. Matokeo yake utajikuta wewe kila siku unayumba tu kwenye uhusiano, hautulii. Unakuwa bingwa wa kuchagua sana lakini

Na Joseph Shaluwa

mwisho wa siku unakuta hakuna aliyekamilika. Kila mtu unayeanzisha naye uhusiano anakuwa na kasoro yake.

JIFUNZE UVUMILIVU

Ndugu zangu, haya mambo ya tabia huwa kila mtu ana zake. Hii inatokana na malezi. Mnakutana ukubwani, kila mtu amelelewa kivyake hivyo unaweza kukuta mwenzako alikuwa na uhuru wa kufanya mambo ya ajabu sana katika safari yake ya kukua.

Anaweza kuwa na tabia za ajabu sana ambazo kimsingi inakuwa ngumu sana kumbadilisha. Mathalan kuna watu wamekulia kwenye familia ambazo kutwa baba anampiga sana mama unafikiri hali hiyo itakuwa inampa picha gani? Au mtu amekulia kwenye familia ambayo baba, mama wote walevi. Naye anapata uhuru wa kufanya kila aina ya uhuni anaotaka bila kuwa na uangalizi wowote kutoka kwa wazazi. Mtu wa aina hiyo unapokutana naye kwa vyovyote lazima ukutane na ukinzani fulani katika maisha yenu.

JIFUNZE KUMBADILISHA

Lakini kama nilivyotangulia awali kusema kwamba, hakuna aliyekamilika hivyo jukumu la kumbadilisha mwenza wako bado unaweza kulibeba kama kweli unamuona anafaa kuwa wako. Jaribu kupima kwanza huyo mtu anafaa kuwa mwenza wako?

MASWALI MUHIMU

Jiulize ana malengo na wewe? Ana nia njema na wewe? Anaweza kubadilika? Maswali hayo matatu muhimu yatoshe kukuongoza katika kufikia maamuzi. Ukishaona ana malengo, ana nia njema na anaweza kubadilika katika jambo fulani basi libebe hilo jukumu.

AMINI ATABADILIKA

Usikate tamaa, ichukulie tabia fulani ya mwenza wako kama changamoto katika uhusiano wako ukiamini kwamba ipo siku moja atabadilika. Ninayo mifano mingi sana ya watu ambao wamebadilishwa mambo mengi na wenza wao, mtu alikuwa mhuni, mkorofi na mwenye tabia chafu kwelikweli lakini anapokutana na mtu mzuri, mtu mwenye malengo na dira nzuri, mwenyewe anabadilika.

PIMA UZITO WA TABIA

Muhimu ni kuwa makini na uzito wa tabia husika tangu mapema, jitahidi kumvumilia mwenza wako kwa kupima yale mazuri mengi aliyonayo na machache mabaya. Yale machache mpe muda, mfundishe abadilike bila kujua anafundishwa.

Post a Comment

0 Comments