UNAJUA MAANA YA KUTA NNE ZA CHUMBA KATIKA

Hakuna ubishi kwamba hisia za mapenzi hasa pale unapompata mtu sahihi, huufurahisha na kuuburudisha sana moyo. Lakini wakati huohuo, hakuna ubishi kwamba maumivu ya mapenzi, hasa pale unapoumizwa na yule unayempenda kwa dhati, huwa huwezi kufananisha na chochote. Waswahili wanasema sikitiko la mahaba lashinda msiba! Furaha au maumivu ya mapenzi, hutokea ndani ya moyo na huhifadhiwa na kuta nne za chumba, mahali ambako wewe na mwenzi wako huwa wapenzi mnakutana.

Kama ni kufurahi mpaka ukataja majina ya mababu zako kwa sababu ya kukolea kwenye dimbwi la mapenzi, haya hufanyikia ndani ya kuta nne za chumba. Kama ni kulia mpaka kusaga meno na kujiapiza maneno yote unayoyajua kwenye dunia hii, haya pia hufanyikia ndani ya kuta nne za chumba. Mwanamama Celine Dion, mkali wa kutunga nyimbo za mahaba, amewahi kuimba wimbo mmoja mzuri sana akisema ‘If walls could talk’ akimaanisha kama ‘kuta za chumba zinaweza kuzungumza’.

Naam, bila shaka kama kuta nne za chumba zitazungumza, basi tutasikia ambayo hatukuyatarajia, kama kuta nne za chumba zitageuka vioo, basi tutaona ambayo hatukutegemea kuyaona, lakini kwa nini hatuyaoni? Ni kwa sababu kuta nne za chumba kazi yake ni kuhifadhi yale mambo yanayofanyika ndani yake. Hapo ndipo uhuru wa faragha ya mtu na mpenzi wake unapopatikana, hapo ndipo mtu anapoweza kutembea bila kuwa na nguo hata moja mwilini mbele ya mwenzi wake na bado akawa huru kabisa.

Sasa kutokana na kukosa uelewa kuhusu maana ya kuta nne za chumba, watu wengi wamekuwa wakifanya makosa makubwa ambayo huziumiza mno nyoyo za wale wanaowapenda, kwa kutoa siri za kile wanachokifanya na wenzi wao wawapo faragha, siri zilizofichwa na kuta nne za chumba. Umekuwa ni mchezo wa kawaida siku hizi kuwasikia wanaume wakijadiliana kwenye vijiwe vyao, kuhusu mambo ya siri ya wanawake. Utamsikia mwanaume bila haya anakwambia ‘Fatuma hakuna kitu kabisa, yaani akiwa kitandani ni sifuri au ni gogo kabisa’.

Huyu ni mtu ambaye Fatuma alimuamini na kumpenda na kuamua kumpa penzi lake, mwisho anaishia kumuanika hadharani. Siri ambazo zilipaswa kutunzwa na kuta nne za chumba sasa zinamwagwa hadharani. Siku hizi imekuwa kawaida pia kuwasikia wanawake wakihadithiana mambo ya chumbani na wenzi wao.

Utasikia ‘Juma hana lolote, dakika sifuri tu chalii!’ Haya ni makosa makubwa sana wanayoyafanya wanandoa na miongoni mwa mambo yanayoweza kuvuruga kabisa uhusiano, ni kumsema vibaya mwenzi wako kuhusu mambo ya faragha kisha maneno hayo yakamfikia kwa sababu maneno huwa na tabia ya kuzunguka na mwisho humfikia mhusika. Unapaswa kupevuka kiakili, siri za chumbani na mwenzi wako hazipaswi kutoka nje ya kuta nne za chumba, hata iweje.

Hata akukasirishe vipi, hata akuumize vipi, hutakiwi kabisa kutoa siri za mwenzi wako hasa zile zinazohusu mambo ya faragha. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Post a Comment

0 Comments