UKO MBALI NA MPENZI WAKO ? ZINGATIA HAYA


KARIBU mpenzi msomaji wa Mahaba Exlusive kwa ajili ya mada hii mujarabu inayozungumzia namna bora ya kuweza kudumisha uhusiano wa mbali wa kimapenzi (distance relationship) kwa wapenzi wanaoishi mbalimbali. Ni sehemu ndogo sana ya wapenzi wanaoishi mbalimbali ambao hudumu kwenye uhusiano wao kwa muda mrefu. Hiki kinaonekana kuwa ni  kitendawili kigumu sana kwa wapenzi wengi kuvumiliana kwenye uhusiano bila kusalitiana. Ninapozungumzia umbali ninamaanisha wilaya na wilaya, wilaya na mkoa au mkoa na mkoa au nchi na nchi au bara na bara.
Ninaamini miongoni mwetu ama tumeshuhudia au kusikia au kuona au kuadithiwa kuwa kuna mwanaume au mwanamke ambaye alikuwa na mpenzi, mara mpenzi wake akapata nafasi ya kwenda kusoma mkoa mwingine au nchi nyingine, lakini mwisho wa siku ukasikia wapenzi wale wameachana baada ya mmoja kupata mpenzi mwingine huko aliko.
Inawezekana mpenzi wako alihamishwa kikazi nje ya wilaya uliyopo, lakini mwisho wa siku ukabaini kuwa mwenzio amepata mtu mwingine na mapenzi kwako yameanza kupungua au yamepungua kama siyo kwisha kabisa. Najua wengi huwa mnajiuliza ni nini huwa kinachangia? Zifuatazo ni baadhi ya sababu;
UAMINIFU
Kutokuwa na uaminifu miongoni mwenu, kama wapenzi mtakuwa ni waaminifu katika uhusiano wenu, basi kila unapoingiwa na pepo wa usaliti unakumbuka uzuri wa mpenzi wako, basi unaacha na kujizuia kisha unakuwa umemshinda pepo huyo.
UZALENDO
Kutokuwa mzalendo kwa mpenzi wako. Jaribu kumpenda kwa kuwa ndiye uliyemchagua kuwa naye, kila siku Tanzania inasema watumishi wake wawe wazalendo, siyo wao tu hata mapenzi yanahitaji uzalendo wa hali ya juu. Uzalendo wa kupenda kitu chako, kumpenda mpenzi wako, mkeo, mumeo au mchumba wako. Lazima ujivunie, ujisifie kuwa naye kisha mthamini.
SUBIRA
Wapenzi kutokuwa na subira au uvumilivu; Hili nalo huchangia kwa kiasi kikubwa mapenzi ya mbali kuvunjika. Kama ilivyo subira ya kila mtu kuamini kuwa ipo siku ataondoka kwenye shida na ugumu wa maisha alio nao, basi amini na kuwa na subira au uvumilivu kwa mpenzi wako ili mfikie ndoto zenu.
MAZINGIRA
Jiepushe sana na mazingira ambayo yanaonekana kabisa yanaweza kukusababisha ukaingia kwenye uhusiano usio rasmi tena, pengine kwa mtu ambaye huna ndoto naye. Tatizo la kujiingiza kwenye uhusiano kwa sababu za kimazingira linaweza kukufanya ukajikuta umezama kwenye mahaba na mtu ambaye hana mapenzi na wewe na mwisho wa siku ukajikuta unaumia sana.
MAWASILIANO
Kutokuwa na mawasiliano ya mara kwa mara nayo huchangia sana kuvunjika kwa mapenzi ya mbali au kupoteza ladha, lakini kama mtu anakupenda kwa dhati, anakupenda tu, anaweza kukupigia simu na kukutumia SMS kibao, lakini akawa bado ni tatizo. Chunga sana!
TAMAA
Kama utaishi kwa kutamani vitu usivyokuwa na uwezo navyo ni dhahiri utajikuta unamsaliti mpenzi wako kwa kuwa tu uko mbali na unaona hawezi kukubana wala kukufuatilia. Ingawa ningekushauri ufanye kitu kwa kujiongoza na siyo kwa kuongozwa na tamaa au kwa kuwa mpenzi wako hayuko karibu nawe.
MKUMBO
Acha maisha ya kufuata mkumbo. Kama mwenzako amefanya kitu f’lani, basi eti na wewe unataka ukifanye au ukipate ili uonekane wa kisasa au mjanja. Kumbuka kuwa mwisho wa siku mtamaliza chuo na mengineyo, kila mtu atasambaa, kama uliharibu kwa mpenzi wako, mwenzio hatakuwepo tena na hapo ndipo utakapoanza kumangamanga na dunia. Tafakari, chukua hatua!

Post a Comment

0 Comments