UHUSIANO wowote wa mapenzi huwa unakuwa na changamoto kwani hukutanisha watu wawili ambao wamelelewa katika maadili tofauti. Yawezekana mmoja anaweza akawa amekulia kwenye malezi madhubuti, mwingine akawa amelelewa tu ili mradi. Yote kwa yote mnakutana na kuanzisha safari yenu mpya. Safari ya uhusiano ambayo mnatarajia ikue na kuzaa matunda mazuri ya uchumba, ndoa na hata familia. Si kazi rahisi, inahitaji pia neema ya Mungu ili muweze kufika mbali katika uhusiano wenu.
Dunia ya sasa imejaa kila aina ya matatizo. Watu wanaishi kwenye majeraha makubwa ya masuala ya uhusiano. Imefika mahali hata imani tena inakuwa haipo. Mtu haamini tena kama anaweza kuwa na mwenza wake, akamkabidhi moyo wake na akawa salama.
Kelele za wengi kwamba; ‘wanaume sio watu wazuri’. Sio hizo tu, nyingine ni za; ‘wanawake sio watu wa kuwaamini sana.’ Kila mmoja ana kilio chake, hii yote ni kutokana na mioyo ya watu kutotaka kubeba changamoto za uhusiano, kutofuata misingi ya uhusiano.
Kwa kuzingatia hilo, ndio maana nimekuja leo hapa na misingi mizuri ya kuifuata ili wapendanao waweze kuishi vizuri bila kuwa na migogoro ya hapa na pale ambayo huharibu kabisa raha ya uhusiano. Sana sana inapokomaa, mnaishia kuachana maana uvumilivu huwashinda. Ili muweze kuishi vizuri, mnapaswa kwanza kuwa kitu kimoja. Kuwa na malengo yanayofanana katika safari yenu na myaweke mezani katika mazungumzo yenu mapema kabisa kabla ya kuanzisha safari yenu.
Kila mmoja wenu ajue na atangulize hiyo dhamira yenu katika maisha yake. Ajue kwamba lengo la nyinyi kuwa wapendanao ni kudumisha safari yenu, kushirikiana katika kila jambo na kusaidiana ili muweze kufika kule mnakotaka kufika. Kauli zenu ziwe na staha. Kila mmoja wenu anapaswa kujua kwamba mpenzi wake ana thamani gani katika maisha yake hivyo ajue pia moja kati ya vitu ambavyo vitawafanya muishi vizuri ni kuwa na kauli nzuri. Epuka kuongea kauli zenye utata, kauli zenye kuudhi au kauli zenye kejeli.
Mheshimu mwenza wako. Mfanye ajione mwenye thamani na asiwepo hata mmoja wa kujiona ni bora kuliko mwenzake. Mwanamke amheshimu mwanaume wake na vivyo hivyo kwa mwanaume, naye amheshimu mwanamke wake.
Kila mmoja aone kwamba anaishi kwa kumtegemea mwenzake, aone ana mchango katika safari yenu ya mafanikio. Kwa namna yoyote ile, epuka kumpa mawazo mwenzako. Mpe nafasi ya kuzungumza mwenzako sio wewe tu ujione ndio una haki ya kuzungumza, muhimu sana kusikilizana hata kama kinachozungumzwa unahisi hakina maana. Kila mtu asimame kwenye nafasi yake. Mwanamke ajitambue kwamba kipi anapaswa kukifanya kwa mwenza wake na kipi hapaswi kukifanya. Vivyo hivyo kwa mwanaume, asimame kweli kama mwanaume. Ajue wajibu wake kwa mwenza wake.
Peaneni uhuru wa kufanya mambo na muwe tayari kuombana radhi pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo. Mkubali kwamba siku hazifanani, kuna siku mnaweza kujikuta mmetofautiana lugha hivyo muwe tayari kusameheana, kueleweshana mambo kwa kutumia hekima na busara. Epukeni sana kukuza mambo, ukiona mwenzako amepanda sana wewe shuka! Tukutane wiki ijayo
0 Comments