JE, NI SAWA MWANAMKE KUMZIDI UMRI MPENZI WAKE

BILA shaka msomaji wangu umzima buheri wa afya. Karibu tena kwenye kona yetu hii tunapopeana elimu na maarifa kuhusu suala zima la uhusiano wa kimapenzi. Leo nataka kuzungumza na wanawake ambao wapo kwenye uhusiano na wanaume ambao kiumri ni wadogo kwao.

Imezoeleka kwamba katika uhusiano wowote wa kimapenzi, mwanaume anapaswa kuwa mkubwa kuliko mwanamke, ikitokea mwanamke amemzidi umri mwanaume, basi ataitwa majina yote yasiyofaa, wapo watakaomuita anatoka na ‘serengeti boy’, wengine watasema ‘anambemenda’ na maneno mengine ambayo hayapendezi.

Inawezekana uhusiano wa aina hii ni mgeni katika mila na desturi za Waafrika lakini utafiti wa kimapenzi unaeleza kwamba, umri si kikwazo katika mapenzi. Kuna msemo wa Kiingereza usemao ‘age is nothing but numbers’ ukiwa na maana kwamba katika mapenzi, umri si chochote bali ni namba tu.

Kama mmependana kwa dhati, tofauti ya umri haiwezi kuwa tatizo kwenu, hata watu wa nje wakizungumza vipi hawawezi kuliathiri penzi lenu kwa sababu mnapendana kwa dhati. Hata hivyo, zipo changamoto ambazo mwanamke unapoamua kuingia kwenye uhusiano na mwanaume ambaye ni mdogo kwako kiumri ni lazima uwe tayari kukumbana nazo.

1.HESHIMA Katika mila za Kiafrika, imezoeleka kwamba mdogo ndiye
anayepaswa kumheshimu mkubwa kuliko ambavyo mkubwa anamheshimu mdogo. Kwamba mdogo ndiye anayepaswa kuanza kumuamkia mkubwa wake, anatakiwa kumsikiliza kwa kila anachomwambia na kuwa na adabu anapokuwa mbele yake.

Hata hivyo, katika mapenzi huwa ni tofauti, mwanaume ameumbwa kuwa kichwa, hata kama ni mdogo, hulka ya kimaumbile, atataka kuheshimiwa, kusikilizwa na kupewa kipaumbele kwa sababu tu ni mwanaume. Na wewe kama mwanamke, jukumu lako la kwanza ni kumsikiliza na kutii anachokwambia. Sasa jiulize, utakuwa tayari kuyafanya hayo kwa mtu uliyemzidi umri? Kama jibu ni ndiyo, basi hilo haliwezi kuwa tatizo katika uhusiano wenu, mtaishi kwa amani, upendo na uaminifu wa hali ya juu.

2. VIKWAZO VYA NDUGU Ipo wazi kwamba ndugu wa mwanaume, hasa mama na
dada zake (mawifi) wanapenda kumuona ndugu yao akiingia katika uhusiano na mwanamke ambaye ni mdogo kwake. Wengi wanaamini kwamba ili mwanaume awe na mamlaka kamili, ni lazima amuoe mwanamke mdogo kwake.

Ikitokea kwamba wewe mwanamke ni mkubwa, maneno na vikwazo vitakuwa vingi sana. Itaonekana kama unataka kumfanya ndugu yao ‘mume bwege’, kwamba hata ukikosea atashindwa kukuwajibisha kwa sababu umemzidi umri.

Jiulize kama utakuwa tayari kukabiliana na kashfa, matusi na vituko utakavyokumbana navyo kwa sababu ni lazima vitatokea tu. Kama unadhani roho yako ni nyepesi, ni bora ukafikiria uamuzi mwingine lakini kama umekubali kujitoa sadaka, simamia penzi lako na hakika mtafika mbali licha ya vikwazo hivyo. Itaendelea wiki ijayo. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

Post a Comment

0 Comments