UVUMILIVU UNA KIKOMO, HATA KAMA NI VIZURI VIPI BORA UMUACHE

KUNA huu msemo usemao, mvumilivu hula mbivu. Hakuna ambaye ni mgeni wa msemo huu, hukuna asiyejua elimu tunayoipata kutokana na msemo huu. Hakika siku zote mvumilivu mwishowe hula mbivu licha ya kwamba inatahadharishwa kuwa makini sana ili isije ikawa badala ya kula mbivu, tunakula zilizooza. Kwa mfano, katika suala la kusaka mafanikio wapo waliokuwa na uchu wa kufanikiwa lakini kwa kuwa muda wao ulikuwa bado, walijikuta wakiishi maisha yasiyotamanika.

Walijitahidi kuvumilia lakini akilini mwao waliamini ipo siku milango ya neema itafungulia, na kweli leo hii watu hao wanakula ‘bata’. Hili lipo hata katika maisha yetu ya kimapenzi. Uvumilivu una nafasi kubwa sana kiasi kwamba usipokuwa na subira, unaweza kukosa furaha ambayo Mungu amekupangia.

Chukulia kwamba umetokea kumpenda kaka fulani lakini kwa bahati mbaya ukakutana na tabia ambazo hukuzitarajia, unafanyaje katika mazingira haya? Je ni sahihi kumuacha? Hili haliwezi kuwa suala la kukuweka njia panda hata siku moja kama uelewa wako utakuwa mkubwa. Cha kufanya hapa ni kupembua na kujua kama tabia zake ambazo huzipendi zinavumilika ama la!

Ukiona zinavumilika, ni vyema ukakubali kumpa nafasi ukiamini kwamba atabadilika lakini wakati unamvumilia unatakiwa kila wakati kuzungumza naye na kumuweka wazi kwamba unampenda sana kutoka moyoni mwako lakini penzi litaongezeka endapo ataacha kunywa pombe, kuvuta sigara au tabia nyingine ambazo umekuta anazo. Kama kweli atakuwa anakupenda, nina imani atabadilika na siku moja utajipongeza kwa uvumilivu wako ambao umekufanya uishi maisha yaliyotawaliwa na furaha. Kumbuka kumpotezea yaweza kuwa ni kuipoteza bahati yako.

Kama huamini katika hili, jaribu kuchunguza na utabaini wengi ambao sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani, walivumiliana kwa mengi hadi kufikia hatua uhusiano wao ukasimama. Kuwa na subira na wala usiwe ni mtu wa kukata tamaa haraka.

Katika maisha ya sasa, watu wamekuwa hawaeleweki, hakuna unayeweza kuwa na uhakika naye asilimia mia moja kuwa anakupenda kwa dhati, subira yako ndiyo itakufanya ugundue hilo. Usichukulie eti kwa kuwa mara kwa mara unampigia simu hapokei, hajibu sms zako, hakupigii basi hakupendi. Kwa maisha ya sasa kupima kama unapendwa au hupendwi kwa njia hiyo siyo sahihi. Mvumilie mpenzi wako huku ukijaribu mara kwa mara kuzungumza naye, usiwe mwepesi wa kuchukua uamuzi.

Hata hivyo nitoe wito kwamba, tusiutumie vibaya msemo! Uvumilivu una kiwango chake. Usiwe wewe ni mtu wa kulizwa kila siku lakini unashindwa kuchukua uamuzi sahihi eti kwa kuwa tu umeambiwa mvumilivu hula mbivu. Vumilia lakini angalia usije ukala zilizooza badaya ya zilizoiva. Kumbuka si kila mpenzi unayekuwa naye anastahili kuvumiliwa kwa muda mrefu, wengine mapema kabisa wanaonekana hawafai hivyo ni uamuzi sahihi kuwaacha kisha wewe endelea na maisha yako. Niwatakie maandalizi mema ya Sikukuu ya Idd.

Post a Comment

0 Comments