SHOGA USIWE JUU JUU KAMA NYAMA YA BUCHANI


 UNANISHA-NGAA wakati umeshindwa kuyalinda maboga utaweza wapi matikiti maji weyeee! Haloooo eeeehhh wanakwambia kuvimba kwa mchele hakushtui mwiko shoga na ukitaka kujua embe lipo tofauti na papai fika mwishoni kwenye kokwa, upo nyonyo? 

Shoga kuna watu hawana tofauti na chafya, wakikutoka unashukuru unasema asante tena na mikono miwili na kichwa unanyoosha juu! Wengine wanajitia wapo juu juu kama nyama ya buchani kwenye chuma cha kuchongoka wakati ni utumbo wa kibandani tena unauzungukwa na inzi kila anayepita anahisi uchafu, heee heeiyaaa!

Leo nina udambwidambwi umenishika hapa kwenye kooo hadi natamani niwe juu juu kama feni ya panga boi, ukiniwasha tu nazunguka mwenyewe! Wareee reee! Hata niteme mate vipi koo linashindwa kunikauka shoga yangu nikipata meseji za hawa wanawake wenzangu ndiyo kabisaaa natamani dunia isimame nishuke miye nyie muendelee!
Hivi kwa nini hamuishi visa jamani! Mwanamke chapombe na baba naye chapombe mnategemea kuna maisha hapo? Mnategemea watoto watafuata tabia za nani hapo? Halafu bora sasa wangekuwa wanakunywa pombe kawaida, yaani wanakunywa wakiwa nyumbani wanashindwa hadi  kuelewana kila mmoja na lugha yake!

Aliyesema ukubwa wa kitambi hauvunji miguu na siyo kila mwenye mtoto ni mzazi wala hakukosea, mtu mzima na watoto juu lakini kutwa kuendekeza pombe tena wengine za kienyeji! Loooo! Jamani huu mwaka ndiyo kwanza unapita katikati mwisho hatujui utaishije tunatakiwa kubadilika, hivi ukinywa kwa kiasi kuna tatizo?

Utakuta mwanamke tena kapewa ofa tu basi kanywa kalewa kama siyo mke wa mtu au ana watoto wanaomtegemea, akirudi huko ndani ni kugombana mwanzo mwisho au watoto kuzoea hali ilivyo kisha wanahamishia tabia kwao!

Shoga naona koo linanikauka na mate sina, jamani chips hazina ukoko ndiyo maana huwezi kukuta zinageuzwa kiporo japo wanaofanya hivyo ndiyo hao ambao kunywa pombe kwao kupitiliza wameona dili hadi wanasahau kama wana familia.
Hebu ngoja nikung’ate sikio shoga yangu maana mimi na wewe tena kama mtandio na hereni! Mjumbe siku zote hauwawi, badilikeni jamani tena mnatia aibu si kwa majirani tu bali hata kwa familia zenu! Kosa analifanya mama au baba lakini aibu inatembea kila kona anayopita mtoto kama siyo kunyooshewa vidole basi ataambiwa maneno ya kejeli yaliojawa na dharau ndani yake!

Wakati mwingine naongea lakini ndiyo kwanza sijui wengine mmezaliwa kijiji cha wapi ambapo wanawake wenzangu mnashidwa kuelewa zuri na baya, au ndiyo kusema mwalimu wetu ni mmoja! Shuuuutuuuuu! Naandika hadi nahisi mikono inatetema, kwa leo niishie hapa shoga yangu, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu

Post a Comment

0 Comments