NIPE, NIKUPE NDIO UTAMU WA PENZI

NI IJUMAA nyingine tulivu kabisa mpenzi msomaji tunakutana tena kwenye uwanja wetu maridhawa kabisa kupeana elimu ya uhusiano baada ya juzi na jana kusherehekea Sikukuu ya Idd. Mapenzi ‘yana-run’ dunia hivyo si vibaya kila siku tukaendelea kuyajadili na kupeana mbinu mbalimbali ambazo zinasaidia katika maisha yetu ya kila siku.

Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita tulijifunza mengi. Wengi sana mlinitumia ujumbe mfupi wa maandishi kuonesha mmeguswa kuguswa na mada iliyopita. Basi moja kwa moja twende katika mada yetu ya leo. Mapenzi ni makubaliano ya watu wawili. Kushirikiana katika shida na raha. Mwanaume amshirikishe mwanamke kwa kila kitu, vivyo hivyo kwa mwanamke. Naye anapaswa kumshirikisha mwanaume kila kitu. Hapo ndipo maana nzima ya mapenzi inapokamilika.

Kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa mwenzake. Ikitokea mmoja wenu hawajibiki kwa mwenzake, penzi huanza kuingia dosari. Yule ambaye mwenzake hamuwajibikii, hawezi kufurahia penzi. Atahitaji na yeye kutendewa wema, kutendewa mazuri, kupendwa kama yeye anavyompenda mwenzake, lakini mwenzake anajifanya kiziwi.

Atahitaji kuona mwenzake anamjali kama yeye anavyomjali. Si kwamba ni malipizi, lakini kila mtu anahitaji faraja. Anahitaji kufarijiwa na mtu wake. Unafikiri usipomfariji wewe kama mpenzi wake, atafarijiwa na nani? Lazima kila mmoja wenu alitafakari hilo kwa upana wake.

Kutokana na tabia, makuzi ya kila mmoja, si rahisi sana wapendanao kukutana na wote wakawa na hulka moja. Kwamba wote wakapendana, wakaheshimiana sawasawa. Lakini kupishana huko isiwe kigezo cha kumuacha mwenzako. Tenga muda wa mazungumzo. Mueleze kwamba kuna kitu anakifanya hakipo sawa. Kwamba mnapaswa kujaliana, kuthaminiana, kuheshimiana na kwa kila hali. Haiwezekani wewe kila siku uwe mtu wa kumpigia mwenzako simu, kumuuliza umeamkaje au umeshindaje, yeye hata siku moja hakuulizi.

Salamu kama hiyo inaweza kuwa kitu kidogo, lakini ina maana kubwa sana. Ikifanywa na upande mmoja kila siku, utafikia wakati utachoka. Naye anaweza kunyamaza kimya. Anaona haiwezekani kila siku yeye tu ndiye awe anajali, mwenzake hana habari, yupoyupo tu. Haiwezekani mwenzako kila unapoumwa wewe, anakuwa bize kukujulia hali, anakufariji kila wakati, lakini wewe ukisikia mwenzako anaumwa, huna habari. Unaendelea tu na shughuli zako. Tatizo hili wanalo zaidi wanaume.

Wanaume wakiwa wanaumwa, wanawake wanakuwa wanawajali, lakini wakiumwa wanawake, hawarudishi upendo kama ule waliokuwa wakitendewa na wanawake. Wanasahau kabisa kwamba wanawake nao wanahitaji faraja kama wanavyofarijiwa wao. Si wanaume peke yao, wapo pia wanawake ambao wanapenda kuwadekea wanaume. Wanataka kubembelezwa wao tu, wanafikiri wanaume hawahitaji kubembelezwa. Wanakosea, hakuna mtu asiyehitaji kubembelezwa.

Unapaswa kutambua kwamba ukibembelezwa na wewe bembeleza kwa wakati. Kama kuna tabia fulani hupendi kufanyiwa wewe kutokana na sababu zako, basi vilevile na wewe usije kumfanyia mwenzako. Unapaswa kumsoma mwenzako, kujua ni kitu gani anapenda kufanyiwa, mfanyie kwelikweli. Zidisha kipimo katika kitu ambacho mwenzako anakipenda. Usimbanie maana wewe ndiyo furaha yake. Usipompa wewe hawezi kuipata sehemu nyingine na hata akiipata litakuwa ni tatizo kwako na mtaanza kugombana.

Usitoe mwanya huo kwani kupendana ni maridhiano. Mnapaswa kukubaliana katika mambo ambayo mnaona hayako sawa. Kama umeona tabia ambayo si nzuri kwa mwenzako, mueleze ili naye akupe hoja zake na mwisho wa siku mfikie muafaka.

Hata mnapokuwa faragha, raha ya tendo ni kila mmoja kumhudumia mwenzake. Isiwe wewe tu kila siku ndiyo unataka uanzwe, siku nyingine anza wewe. Kuwa bize kama mwenzako anavyokuwa ‘bize’, usimtegee kwani na yeye atainjoi kama na wewe utakuwa bize. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

Post a Comment

0 Comments