LULU DIVA: HAKUNA WA KUDIDIMIZA NDOTO ZAKO

“Hata hapa nilipofika namshukuru Mungu kwa sababu sikutarajia, sikuweza kuendelea na masomo baada ya kumaliza kidato cha nne lakini nilipambana kufikia ndoto zangu.”

Hivyo ndivyo msanii wa muziki wa kizazi kipya, Lulu Diva alivyoanza kuelezea historia ya maisha yake mbele ya vijana waliokuwa kwenye mdahalo wa namna usawa wa kijinsia unavyoweza kuchochea maendeleo.

Mdahalo huo ulioandaliwa na Shirika la Plan International ulilenga kuwajengea vijana hasa wa kike uwezo wa kujiamini, kujitambua na kufikia ndoto zao kimaisha.

Kabla ya kuimba, Diva alitumia nafasi hiyo kuwaambia wasichana wanaweza kufika akisimulia historia yake kwa ufupi ili kuwapa moyo hasa wasichana waliokata tamaa katika ndoto zao.

Wasanii wengine waliopamba mdahalo huo ni Elias Barnaba, Kala Jeremiah na mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

“Kipaji changu kilionekana zamani na sikukata tamaa licha ya changamoto kadhaa, niliamua kufanya nilichosikia moyoni na sasa nasimama mbele yenu kuwapa historia,” anasema Diva huku akipigiwa makofi.

Anasema aliamini siku moja atapata tuzo za kimataifa na atakuwa kati ya wasanii wakubwa Tanzania ndoto ambazo leo hii anaziishi.

Historia yake ndiyo inayomfanya asimame mbele ya vijana wenzake hasa watoto wa kike kuwaambia chochote kinawezekana.

Anasema ili kuwainua wengine, anatarajia kuanzisha taasisi yake kwa ajili ya kutetea na kuwasaidia wasichana wa kazi wanaonyanyaswa.

Anadai kuwa baadhi ya wasichana hufanyishwa kazi ngumu na kulipwa ujira mdogo kinyume na sheria.

“Wasichana wengi wamepoteza ndoto zao na kuamua kufanya kazi za ndani wakiamini zitawasaidia kimaisha lakini wakiwa kazini hukutana na ukatili wa kijinsia, lazima tuwasaidie,” anasema kwa kujiamini na kuongeza;

“Nataka kupitia shirika langu nitakaloanzisha sauti za wasichana hawa zisikike na waanze kuheshimiwa kwa kazi kubwa wanayoifanya,” anasema Diva.

Anaeleza kuwa ni ajabu kuona wasichana wanaotegemewa kulea watoto na kulinda nyumba wanafanyiwa ukatili wa kijinsia na mabosi wao wakati ndio wanaobeba dhamana ya nyumba zao.

“Kipaji cha muziki ukikitumia vizuri unaweza kufika mbali cha msingi ni kuwa na malengo, nina malengo,” anasema.

Wakati Diva akizungumzia mkakati wake wa kuanzisha taasisi, Kala Jeremiah anasema wasanii wana nafasi kubwa ya kuwa kioo cha jamii kwa kuwafanya vijana hasa mabinti kufikia malengo yao.

Huku akitoa mfano wa Jokate Mwegelo alivyopigana kufikia ndoto zake, Kala anasema wasichana wakiamua wanaweza kufanya vizuri.

“Jokate wakati ule alinipatia jina la Kala Jeremiah, mwanadada huyu amepambana sana na ni ‘role model’ kwa mabinti wengi wanaotaka kufikia ndoto zao,” anasema Kala.

Barnabas kwa upande wake alisema aliamua kuimba wimbo usawa wa kijinsia akiitaka jamii kuwaheshimu wasichana ili wafikie ndoto zao kwa sababu bado ni kikwazo.

Awali Mkurugenzi mkazi wa Plan International Gwyneth Wong alisema kila mwanajamii wakiwamo wasanii wanapaswa kupiga vita ukatili wa kijinsia ikiwamo ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni.

Post a Comment

0 Comments