STAA wa filamu Bongo, Kajala Masanja amefichua chimbo jipya la mastaa lililopo katika msitu wa Magoroto uliopo Wilaya ya Muheza, kilomita 37 toka katika Jiji la Tanga. Akizungumza na gazeti hili la Risasi Mchanganyiko, Kajala alisema amekuwa akienda eneo hilo kwa ajili ya kupumzika na kula bata, akashangazwa na mandhari yake ambapo inaelezwa kuwa mastaa kibao wamekuwa wakifika.
“Jamani sasa hivi ni ngumu sana kuona mastaa wanaopenda sehemu tulivu wamekwenda kujiachia kwenye viwanja vya Dar, wengi sasa hivi wanaenda Magoroto, aisee kuna raha. “Kule hata uwe na msongo wa mawazo kiasi gani yanapotea fasta kwa kuwa ni sehemu tulivu mno na mara nyingi siku za mwisho wa wiki naenda kwa ajili ya kupoteza mawazo na kuangalia uzuri wa nchi yangu,” alisema Kajala.
Staa huyo aliongeza kuwa watu wengi ambao ni maarufu wanapenda kwenda kupumzika eneo hilo kwa sababu kuna vitu vingi vya asili kama milima, kijani kibichi, ndege na hali ya hewa safi. “Mimi kuna wakati nilitamani nitafute nyumba maeneo ya kule ili kila wikiendi iwe rahisi kwenda kujiachia, yaani ukijaribu kwenda mara moja utatamani iwe hivyo mara kwa mara,” alisema Kajala.
Baadhi ya mastaa ambao wametajwa kutinga katika chimbo hilo siku za hivi karibuni ni Diamond Platnumz ambaye licha ya kuwahi kutengeneza video katika eneo hilo amekuwa pia akipendelea kufika, DJ Sinyorita, Maua Sama, Ben Pol na wengineo.
Undani kuhusu Marogoto Msitu wa Magoroto uliopo Wilaya ya Muheza una ukubwa wa ekari 591 na ziwa la maji masafi na unatengeneza vipande vya milima ya Usambara ambayo inafahamika kwa uzuri na upekee wa uoto wa asili.
Msitu huo unafahamika zaidi kwa uwepo wa ndege wa kipekee ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Chama cha Uhifadhi Wanyamapori wanahusika katika uhifadhi wa misitu hiyo nchini. Mogoroto ni kivutio cha utalii siyo Muheza pekee bali kwa mtu yoyote mwenye nia ya kutembelea eneo hilo kutokana na hali yake ya hewa kuwa nzuri huku ikiambatana na mandhari nzuri ya chini ya milima.
0 Comments