JINSI YA KUEPUKA MIMBA ZISIZOTARAJIWA

WANAWAKE wengi hawajui kuhesabu mzunguko wao wa hedhi na namna unavyoweza kutumika katika kuleta au kutoleta ujauzito. Hata hivyo, ili mfumo wa hedhi uwe na maana kuna uhusiano na hali ya mfumo wa maisha ya mhusika, vyakula anavyokula na shughuli nyingine za kawaida. Hedhi unaweza kuigawa katika mafungu matatu ambayo ni mzunguko mfupi (siku 21), mzunguko wa kati au kawaida (siku 28) na mzunguko mrefu wenye siku 35.

Kwa hapa mzunguko huanzia pale mwanamke anapoanza kupata damu za hedhi. Mbali na mizunguko hiyo ambayo haibadilikibadiliki, wapo wanawake wanaopata mizunguko ambayo haipo katika kundi hilo kwa maana ya kuanzia siku 22, 23, 24, 25, 26, 27, 29, 30, 31, 32, 33 na 34. Mwanamke anayepata mzunguko chini ya siku 21 na zaidi ya siku 35 anachukuliwa kwamba ana tatizo la hedhi. Kutokana na utofauti wa mizunguko kwa kila mwanamke, uanguliwaji wa yai ambao ndio kitu muhimu sana cha kuangalia suala zima la mimba, pia hutofautiana.

Ili mwanamke aweze kujua siku zake sahihi za hatari ni lazima ajue anaangua yai siku gani au siku ya ngapi kutokana na urefu wa mzunguko wake. Mzunguko rahisi kufuatilia ni ule usiobadilikabadilika. Wapo wanawake ambao wao tangu wanaanza kupata hedhi siku zake hazibadilikibadiliki na wapo wale ambao wao kila mwezi tarehe hubadilika.

Wimbi kubwa la wanawake wamejikita kwenye chati inayozunguka mitandaoni inayoonesha jinsi ya kuhesabu siku za hatari na kujua mzunguko wao lakini chati hiyo haimfai kila mwanamke. Chati hizo nyingi ni zile za mzunguko wa siku 28 ambao wengi wapo kwenye mzunguko huo, lakini hata hivyo haimaanishi kila mwanamke atumie chati hiyo.

Kupevuka kwa yai ni nini? Kupevuka kwa yai ni pale yai moja au zaidi yanapoachiwa kutoka kwenye moja ya mfuko wa mayai (ovary) na hii hutokea mwishoni mwa muda ambao mwanamke ana uwezo wa kupata mimba katikati ya mzunguko wake wa hedhi.

Kila mwezi, kati ya mayai 15 hadi 20 huzalishwa ndani ya mfuko wa mayai ya mwanamke. Yai lililopevuka hutolewa na kusukumwa kwenye mirija ya uzazi (fallopian tubes) inayounganisha na tumbo la uzazi. Mifuko ya uzazi sio kwamba inapokezana kutoa yai kila mwezi. Hili hutokea bila mpangilio maalumu.

Ili kupata ujauzito kwa njia ya kawaida, yai na mbegu kutoka kwa mwanaume lazima vikutane kwenye mirija ya uzazi. Yai la mwanamke haliwezi kuwa hai kwa zaidi ya saa 24 baada ya kuwa kwenye upevushaji, kwa hiyo kukutana kwa yai na mbegu lazima kutokee ndani ya muda huo.

Kwa upande mwingine, mbegu za mwanaume huweza kuwa hai hadi kufikia siku saba. Mbegu zitaishi kwa raha tu kwenye uke, mfuko wa mimba, au kwenye mirija ya uzazi kwa muda wote huo. Hii inamaanisha, sio lazima mwanamke ahesabu muda sahihi kabisa ikiwa yai limepevushwa kupata ujauzito. Kiuhalisia kila mwanamke ana jumla ya siku sita kwenye mzunguko wake wa hedhi ambazo anaweza akashika mimba.

Kwa hiyo kama akifanya tendo la ndoa katika kipindi hiki, yai lake lililopevuka tayari linaweza likakutana na mbegu yenye afya ya mwanaume na kupevushwa na kutungwa mimba.

Upevushaji mara nyingi hutokea kati ya siku ya 12 hadi 14 kabla ya hedhi nyingine kuanza.

Hii ni wastani tu wa makadirio, hivyo inaweza ikawa ni siku chache kabla au baada. Kwa mfano, tuseme mwanamke ana mzunguko wa kawaida wa hedhi wa siku 28.

Post a Comment

0 Comments