JE, WAJUA UTAMU WA MCHEPUKO??

Na THOMAS MATIKO

UNAWEZA kusema kuwa mchepuko umeondokea kuwa kama vile ni mtindo wa kawaida sana ijapo sio sawa.

Kikweli mchepuko huumiza nafsi ya aliyeathiriwa, lakini hata zaidi, huwa ni msumari moto kwenye kidonda, pale mhusika anachepuka akiwa kwenye ndoa na cha kuzidisha, akaishia kuchumbiana na mchepuko wake, ndoa yake ikiwa bado haijavunjika.

Ni visanga ambavyo hutokea kila leo na hata nao maceleb wamejikuta kwenye hali hii.

Hawa ni baadhi tu ya mastaa wa burudani walioishia kuchumbia michepuko yao wakati wakiwa wangali kwenye ndoa.

Elizabeth Taylor

Alipata umaarufu mkubwa sana katika miaka ya 50 hadi 60 kutokana na uigizaji wake.

Hata baada ya kustaafu uigizaji, umaarufu wake haukuwahi kupungua hata siku moja.

Taylor alikuwa mwigizaji Mwingereza aliyefanikiwa kung’aa sana Hollywood licha ya kwamba alikuwa akitokea familia ya kitajiri. Maisha yake aliyakulia sana Marekani ilikohamia familia yake 1939 na kujenga boma mjini Los Angeles.

Ukiachana na umaarufu wake wa usanii, maisha ya kibinafsi ya Taylor yalikuwa ya kuvutia kwa wengi waliomfuatilia. Hadi anapofariki dunia 2011 akiwa na umri wa miaka 79, staa huyu aliacha rekodi ya kuolewa mara saba.

Siku kumi tu baada ya kutalikiwa na mume wake wa nne Eddie Fisher (1959-64), Elizabeth alimwoa mchepuko wake Richard Burton. Burton na Elizabeth walidaiwa kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa kipindi kirefu sana hata alipokuwa kwenye ndoa na Fisher. Ilidaiwa kuwa alimvisha pete ya uchumba akiwa angali hajatengana rasmi na Fisher.

Burton na Elizabeth walianza mahusiano yao kipindi wote wakiwa katika ndoa.

Swizz Beatz

Produsa huyu maarufu wa Hip hop ndiye mume wake staa wa RnB Alicia Keys. Ndoa yao imedumu kwa miaka tisa sasa. Kabla hawajaoana Beatz alikuwa kwenye ndoa na staa mwingine mwanamuziki Mashonda.

Wakati Beatz akianza uhusiano na Keys, alikuwa kwenye ndoa na Mashonda ambaye alianza uhusiano naye 1998. Mashonda na Beatz walitangaza kuvunjika kwa uhusiano wao 2008 ila hawakuwa wametalikiana. Kipindi hichi cha utengano ndicho Beatz alianza kutoka na Keys.

Talaka ilipoidhinishwa Mei 2010, mwezi uo huo Beatz alitangaza kumchumbia Keys na hata kuongezea kwamba alikuwa tayari kampachika mimba.

Julia Roberts

Nyota huyu wa Hollywood alimkufia mume wa mtu Danny Moder kipindi akiwa kwenye ndoa na mkewe Vera Steimberg.

Julia alitaka sana kuwa na Danny, ikiwa sababu moja iliyopelekea kuvunjika kwa ndoa hiyo. Danny na Vera wakiwa wametengana, inadaiwa Roberts aliamua kumlipa mwenzake Dola400,000 ili aharakishe utaratibu wa talaka. Miezi kadhaa baada ya kutalikiana, Julia alifunga ndoa na Danny.

Jennifer Lopez

J-Lo tayari kachumbiwa na Alex Rodriguez ambaye huenda akawa mume wake wa tano. Miezi michache tu baada ya kutangaza kutengana na mume wake wa pili Chris Judd huku wakiwa wanasubiria talaka, J-Lo alianza kuonekana na mwigizaji Ben Affleck kwenye hafla mbalimbali alizomtambulisha kama mpenzi wake mpya.

Hata kabla ya talaka, J-Lo na Affleck walitangaza kuchumbiana. Inasemekana mchepuko wa kimya kimya kati ya J-Lo na Affleck ndio ulisababisha ndoa yake na Judd kupata kutu.

Mariah Carey

Kipindi akichumbiwa na bilionea wa Australia James Parker mwaka 2018, talaka za wawili hao zilikuwa bado hazijatoka.

Uamuzi wa talaka ya ndoa kati ya Mariah na mumewe wa zamani Nick Cannon ulikuwa bado ukisubiriwa sawia na talaka yake James kwa mkewe wa pili Erica.

Mariah Carey. Picha/ Hisani

Post a Comment

0 Comments