HAMISSA: UREMBO WANGU NJE, JIKONI HUNIWEZI

Nwakati mwingine mzuri wa wewe mpenzi msomaji kupata nafasi nyingine tena ya kujua maisha halisi wanayoishi mastaa mbalimbali kupitia safu yako hii ya ‘MY STYLE’. Hiki ndicho kiwanja cha mastaa kufunguka kwa undani kuhusiana na staili zao za maisha na gharama za matumizi yao. Najua huwa unaenjoy vya kutosha kwenye kona hii ya kipekee kwenye magazeti Bongo.

Unataka kujua leo tunaye nani? Jibu ni rahisi tu, tupo na mwanamitindo na mwanamuziki Hamisa Mobetto ambaye kwa sasa ameanza kusumbua kwenye muziki, akitesa na kibao cha Bosi ambacho hadi juzi Alhamisi jioni kilikuwa kinatrend namba mbili katika mtandao wa Kijamii wa Youtube. Hamisa ni mzazi mwenzake na mwanamuziki wa Bongo Fleva, anayetamba ndani na nje ya nchi, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’. Huyu hapa anafunga kwa undani.

MY STYLE: Msomaji angependa kufahamu wewe ni mtu wa aina gani?

HAMISA: Mimi ni mtu ambaye kwanza ninapenda sana watu, na pia ninafurahi kuona kila anayenizunguka ana furaha na wakati wote huwa napenda sana amani.

MY STYLE: Nini ambacho kinafanya maisha yako uyaone yako sawa kwa kila kitu?

HAMISA: Ni watoto wangu (Fantansy – aliyezaa na Majizo na Dylan – aliyezaa na Diamond) na mama yangu mzazi. Kiukweli hao wanafanya kila kitu changu kiende sawa kabisa.

MY STYLE: Maisha yako ukiwa ndani ya nyumba unayoishi yakoje?

HAMISA: Mimi nikiwa nyumbani napenda sana kuwa jikoni, napenda kupika sana. Mara nyingi napenda kujifunza vitu mbalimbali kwa hiyo naweza kukaa jikoni muda mrefu kuliko hata kukaa meza ya kujipamba.

MY STYLE: Kwa nini hupendi kufuga kucha za mikono yako kama wengine?

HAMISA: Kwanza kabisa mimi ni mtoto wa Kiislamu na mara kwa mara naenda kuswali, urembo wangu hauko kwenye mikono.

MY STYLE: Unapenda kwenda kwenye mitoko sehemu gani?

HAMISA: Mara nyingi sana mimi sio mtokaji, labda kuwe na sehemu maalumu inayonitaka niende na si vinginevyo.

MY STYLE: Umezaa watoto wawili lakini unaonekana kama hujawahi kuzaa nini siri ya urembo wako?

HAMISA: Siri kubwa ni kujipenda, kingine kuchukulia kila kitu kinachotokea kwenye maisha kama changamoto inayokufanya kusonga mbele. Hakuna siri zaidi ya hiyo.

MY STYLE: Kwenye mitoko yako ya kila siku unaweza kuteketeza shilingi ngapi?

HAMISA: Inategemea wapi nakwenda kwa sababu mitoko yangu mingi huwa navaa nguo ambazo zimetengenezwa kwenye kampuni yangu ya Mobetto Style lakini siku moja moja kuteketeza milioni na nusu kwenye mtoko mmoja sio mbaya.

MY STYLE: Chakula gani unapendelea zaidi?

HAMISA: Napendelea chakula cha Kitanzania chochote kilichopikwa vizuri kabisa huku maharage yakiongoza.

MY STYLE: Kwa upande wa watoto wawili ulionao, wanatosha kwako au una mpango wa kuongeza wengine?

HAMISA: Mimi nina mpango wa kuzaa sana, hata watoto saba kwa sababu kwenye familia yetu tupo wachache sana.

MY STYLE: Kwenye simu yako, namba ya nani ina umuhimu zaidi, hata kichwani mwako umeikariri?

HAMISA: Ni ya mama yangu – si ya mtu mwingine yeyote yule.

MY STYLE: Unapochukia, kitu cha kwanza huwa unafanya nini?

HAMISA: Huwa naondoka eneo la tukio maana sipendi kabisa ugomvi.

MY STYLE: Unapenda kuolewa na mwanaume wa aina gani?

HAMISA: Mwanaume mkweli na mwenye mapenzi ya dhati.

MY STYLE: Nashukuru sana kwa ushirikiano wako Hamisa.

HAMISA: Asante nawe pia, karibu tena wakati mwingine.

MY STYLE: Asante

Post a Comment

0 Comments