Simulizi Ya Maisha; Asante Kwa Kunitesa Frank -Sehemu ya 39



ASANTE KWA KUNITESA FRANK
MTUNZI:  TIMOTHY PETER MSUYA “KIRAKA”
+255 763 305 605
SEHEMU YA THELATHINI NA TISA
__________________________
Waambie hivi…
Wanaoamua kuwa wakweli na nafsi zao hawatumii nguvu kubwa kuishi. Mara zote wanajua namna nzuri ya kuituliza mioyo yao na kujipa nafasi ya kukubali yale ambayo wanajua wazi kuwa hawawezi kuyabadili katika maisha yao. Wanaopenda kuwa waongo, wako tayari hata kujidanganya wao wenyewe kuwa wana uwezo katika kila jambo. Hii wakati wote inawasababishia kuishi kwa wasiwasi, hofu na zaidi sana uchungu wa kushindwa yale ambayo walikuwa na uhakika kuwa wanayaweza.
Hii ni sehemu ya thelathini na tisa
_________________________
Akiwa na mawazo tele juu ya hali yake, sasa wazo la kutafuta mganga wa jadi atakayeweza kumsaidia kutokana na tatizo lile likamjia kwa kasi. Aliamini wazi kuwa alikuwa akichezewa na wasiopenda mafanikio yake. Lile hakusita kumshirikisha Imelda ambaye naye akamsisitiza kuwa, huenda kweli walikuwa wameshikiwa nyota zao na wale wake wakubwa, kwani hata yeye pia alikuwa akihisi kuwa mke mwenzake ndiye aliyekuwa na gundu kwa kuwa, amemchawia nayeye kupata mtoto mwenye ulemavu, labda kwa kuwa mtoto wake naye alikuwa mlemavu. Wazo la kumpata mganga mzuri atakayewasaidia katika vita ile likawa ndilo pekee vichwani mwao. Harakati za kumtafuta zikaanza mara moja!!
Maskini ni bora wangekaa chini na kuibuka na njia sahihi zaidi!! Kwa pamoja, wakaianza safari fupi sana ya kuyamaliza maisha yao!!
***************
Malamba, Muheza, Tanga
Giza lilikuwa limetanda sehemu kubwa ya kijiji cha malamba, wilayani Muheza mkoani Tanga. Kwa mkazi yeyote wa eneo lile, isingekuwa rahisi kutishwa na ile milio ya ajabu ajabu kutoka kwa wadudu na ndege wapendao kulia usiku, lakini kwa Kidawa, kila mlio ulikuja na aina ya mshtuko kwa upande wake. Alikuwa na Shemahonge, mganga aliyeelekezwa kwake na mojawapo ya marafiki zake waishio jijini Dar es Salaam, na kwa msaada wa mtandao wa marafiki zake ambao wengine alikuwa amewafahamu kupitia mitandao ya kijamii tu, akajikuta akifika kwa mzee yule maarufu. Walikubaliana na swahiba wake Imelda kuwa, yeye atangulie kwa mganga yule kwa kuwa yeye alikuwa na mtoto mchanga bado, na ikiwezekana atakaporudi ampe mrejesho juu ya mganga yule
Kidawa akawa tayari kwa mzee Shemahonge, baada ya maandalizi ya miezi mitatu!
Zoezi la tiba likaanza rasmi. Usiku huu wa kiza kinene, Kidawa alikuwa amekalia mfano wa chungu kilichokuwa na mdomo mpana kiasi ambamo ndani yake kulikuwa na maji yaliyokuwa na moto kiasi huku akiwa hajui ni nini kilikuwa kikiyapa moto maji yale kwani kwa zaidi ya dakika arubaini haya kuwa na dalili yoyote ya kupoa. Baada ya manyanga na manuva kadhaa ya mzee yule, sauti ya kutisha ikatoka katika kinywa chake, huku sasa akiwa anazungumza lugha zisizoeleweka na kuruka huku na kule. Kutokana na macho yake sasa kuwa yameshalizoea giza, aligundua pia kuwa, kama ilivyokuwa kwake, mzee yule pia alikuwa yuko uchi wa mnyama, huku maumbile yake makubwa yakiwa yanaruka ovyo kila alipokuwa akiruka ruka na kucheza machezo yake katikati ya kiza kile.
Alionekana wazi kukereka na hali ile, lakini akajikumbusha kuwa mtaka cha uvunguni sharti ainame. Akajilazimisha kuendelea kuangalia video ile ya kuchekesha.
“Ni kweli Kidawa. Naliona tumbo lako la uzazi likiwa linafanya kazi sawasawa. Na tayari limeshapokea mimba sita ingawa zote zinatoka mapema tu.. Tawireeeee” hatimaye Shemahonge alizungumza kwa Kiswahili
“Tawire babu” Alijibu Kidawa huku sasa moyo ukimtulia kwa kuwa alikuwa amepata mganga sahihi.
“Rrrrrrrrr… Robookaaaa, taaaaaariiiiiiik… Raaaaaarikkk.. Ooooooo Roooobokaaaa… Sasa utapata ujauzito, na huu wa sasa hautatoka kamwe. Nitakupa dawa, na utarudi kwako. Utahesabu siku ishirini na saba ukiwa unaitumia dawa hii kwa kunywa kila siku usiku. Kisha siku ya ishirini na nane utafanya safari kurudi hapa Malamba, na utafika hapa siku ya ishirini na tisa mchana. Usiku wa kuamkia siku ya thelathini nitaiita mizimu itakayoingia ndani yako kulishika vema tumbo lako ili usije ukapoteza ujauzito.. Raaaaaaboookaaaaa.. Tawire!”
Akapewa masharti mengine machache kisha akarejea Dar es Salaam kuanza rasmi ile tiba. Alimwelezea rafikiye juu ya mganga yule. Hali ya Nicas sasa ilikuwa wazi kabisa kuwa alikuwa na tatizo. Tayari walikuwa wameshaanza tiba na kuahidiwa kuwa mtoto wao angepona ingawa asingeweza kabisa kuondokana moja kwa moja na ile hali ya mtindio wa ubongo! Imelda akaazimia wazi kuwa, ni lazima angekwenda kumwona mzee Shemahonge ili amuwekee sawa mambo yake.
Akawa anangoja mafanikio ya Kidawa ili yamvutie na yeye zaidi!
******************
Ulikuwa sasa ni mwezi wa nne wa ujauzito wa Kidawa! Tofauti na mimba zingine, mimba hii ilikuwa ikiendelea vema kabisa na mpaka wakati huu kila alipokwenda kupima, kila kitu kilionekana kuwa swadakta kabisa. Hii ikaongeza pia ile hamu ya Imelda kwenda kumwona Shemahonge, sasa akiamini kabisa kuwa hali ile ya mwanae kuwa na tatizo ilisababishwa na Jamila kwa kuwa alikuwa akitembea na mumewe. Safari ikapangwa na akawasili Malamba, huku sasa wakati huu akiwa ameambatana na Kidawa ambaye sasa alikuwa mwenyeji.
Walikaribishwa kwa mbwembwe nyingi na msaidizi wa Shemahonge na wakapangiwa wakati wa kuonana na mzee yule. Saa nne kasorobo hivi za asubuhi, wakaingia kwa Shemahonge, naye bila ajizi akaeleza wazi nia ya safari yao ile baada ya yale makeke yake kwa muda mfupi tu. Lakini jambo moja likawa tofauti kabisa na matarajio yao.
“Hauko sawa hata kidogo. Mtoto huyu hajalogwa wala kudhurika kutokana na matatizo yenu ya mahusiano. Huyu ni lango. Mtoto huyu ni mlango wa kuingilia sehemu, na panaonekana wazi kuwa na hatari kubwa sana kwangu na hata kwenu kuanza kufuatilia mambo ya mtoto huyu. Tafadhali sana naomba muondoke upesi” Alisema Shemahonge huku mawimbi ya hofu yakizidi kujijenga katika sura yake iliyokuwa na hali fulani ya kuogofya kutokana na weusi usio wa kawaida.
“Babu hapana. Mi nna uhakika ni mke mwenzangu. Tafadhali tusaidie. Hilo lango sijui nini si ulifunge tu jamani?” Imelda ambaye sasa alikuwa ameamua kuiweka taaluma yake ya sheria kando na kuamua kuyapigania maisha na afya ya mwanae ingawa kwa njia isiyoendana kabisa na taaluma yake ya sheria alimsihi Shemahonge.
“Unanipa wakati mgumu sana. Sawa. Acha niwasiliane na mizimu yangu. Saa nne usiku mtarejea tena hapa kwaajili ya kwenda kujaribu bahati yenu. Mtanijia na mayai manne, nazi ambayo haijakomaa pamoja na kitambaa chekundu” Alimaliza mzee yule na kuwaamuru kuondoka mara moja.
*****************
Kama ambavyo walikuwa wameamriwa asubuhi iliyotangulia, muda ule ule walioambiwa uliwakuta wakiwa katika ua wa mzee Shemahonge ambaye toka mchana hakuwa ametoka ndani wala kuwahudumuia wateja wengine. Safari ya kuelekea katika kilinge cha kuagulia cha mzee yule kikaanza.
Hali ilikuwa tete! Wakati tu shughuli ile inaanza rasmi, mawingi mazito mazito yalianza kujitokeza kama vile kulikuwa na dalili ya mvua kunyesha kwa wingi. Ilikuwa ajabu zaidi kwa Shemahonge kwani, ile haikuwa miezi ya mvua katika kijiji kile na mkoa mzima wa Tanga. Haraka akaanza manyanga yake huku akionekana wazi kuwa mwenye ama hasira ama hofu kubwa. Upepo mkali ukaanza kuvuma huku radi zikianza kulichora anga lile.
Shemahonge aliyachukua mayai yale yaliyoletwa na kina Imelda na kuyanenea maneno Fulani kisha akayanfunga katika kitambaa kile na kuyapasulia miguuni mwa Nicas alliyekuwa ameshikiliwa na mama yake huku miguu yake ikiwa imegusa ardhi iliyopoa, huku akiichukua na ile nazi na kuipasulia miguuni mwa Imelda. Kidawa alibaki mbali akiwa anatazama tu kwa wasiwasi mkubwa.
Ngurumo kubwa ikatanda eneo lote kwa kama dakika mbili au tatu hivi, kisha upepo mkali ukazuka pale alipokuwa Shemahonge. Upepo ule ukaambatana na yowe kubwa kutoka kwa Shemahonge, yowe lililokuwa na kila aina ya uchungu na majuto makubwa… Kisha….. Mwanga mkali ukalijaza eneo lile kama vile kulikuwan na tochi kubwa iliyokuwa ikimulika pale.
Utulivu ukarejea kama awali… Lakini……
Ah!! Mungu wangu!!!
Shemahonge alikuwa amejilaza pembeni ya Jamila akiwa kimya kabisa. Hakukuwa na dalili zozote za uhai kwa mzee yule. Pale alipokuwa amesimama awali palikuwa na mtu mpya kabisa. Mtu ambaye, hakuwa mgeni machoni pa Kidawa. Alikuwa mzee aliokuwa na upara mpana na midevu mingi iliyokuwa imesambaa vibaya, huku pamoja na baridi kali iliyokuwa imetanda usiku ule, bado zee lile lilikuwa kifua wazi, huku tumbo lake kubwa liking’aa kutokana na jasho lililokuwa likimtiririka. Kumbukumbu zikamrudia Kidawa na kukumbuka kuwa aliwahi kumwona mzee huyu zaidi ya siku ile. Alikuwa ni mtu wa karibu na kina Ndimbo.
Alikuwa mzee Okafo!
Bila kusema nao, akainama na kuokota kile kitambaa kilichovunjiwa mayai na kukifunga fundo lingine huku akioneka wazi kuwa na ghadhabu zisizo za kawaida. Akawatazama kwa mara ya mwisho na kisha akageuka na kuanza kuondoka bila kusema neno lolote. Kwa Kidawa na Imelda, hali ilikuwa tete. Huku wakiwa wamechanganyikiwa vibaya, wakajizoazoa na kuanza kutoka mbio huku Imelda akiwa amembeba mtoto wake kwa umakini mkubwa. Usiku ule wa hofu ukapita na mapema kabisa asubuhi, wakaianza safari chungu ya kurejea Tanga na kisha Dar es Salaam huku kila mmoja akiwa kimya kabisa. Hakuna aliyekuwa na hamu ya kuzungumza na mwenzake na walipotazamana, kila mmoja alikwepesha macho kuonesha wazi dalili za waziwazi za majuto!
Safari ya kwa Shemahonge ikawa imemalizika kwa hofu kubwa, huku wakiwa na uhakika kabisa kuwa, hata maisha ya Shemahonge yamefikia mwisho!
******************
Taarifa za Ndimbo kuhusu ujauzito wa Kidawa kupitisha miezi mitano salama ndiko kulikoharibu kila kitu! Kidawa akaanza kuchunguzwa mara moja. Ndimbo akasahau kuwa, idadi ya sadaka ambazo alikuwa akidaiwa hazikuwa zimefikia kiasi kile ambacho ndicho lilikuwa deni halisi. Kwa Okafo, uchunguzi ukaanza ingawa kila walipojaribu kumfikia Kidawa ilikuwa inashindikana. Ni kama alikuwa na nguvu ya ziada ambayo kwao ilikuwa inawazidi mara kwa mara. Lakini siku hii baada ya Nicas, ambaye alikuwa ni mtoto wa Frank aliyezaa na Imelda, kisha akamweka kuwa aina ya kafara ambayo tofauti na mwanae wa kwanza aliyemtoa sadaka, yule angekuwa ni mlemavu wa akili kwa maisha yake yote ili awe mlango wa mafanikio kwa Frank, kupelekwa kwa mganga, ikawa ni njia ya yeye kufika mara moja eneo la tukio.
Haraka akafika kupambana na Shemahonge, ambaye hata hivyo kutokana na wepesi wake, alifanikiwa kumzidi nguvu na kummaliza kwa haraka tofauti kabisa na maandalizi makubwa aliyokuwa ameyafanya. Ndipo sasa akagundua jambo zito ambalo lilikuwa ni jibu kw swali alilokuwa akijiuliza kila siku juu ya Kidawa. Mimba ile ya Kidawa ilikuwa ya Shemahonge, na alimwingilia bila kuwepo kwa uelewa wa Kidawa, na kutokana na Kidawa kujiaminisha kuwa mtoto yule alikuwa ni wa Ndimbo, asingeweza kuendelea kuishi akiwa anaaminika kuwa ni mtoto wa Ndimbo. Hii ingekuwa hatari kubwa kwao na mizimu yao. Ilikuwa wazi kuwa, kwa kosa walilolifanya, Imelda na Kidawa walipaswa kupotezwa mara moja kwani pia kubaki kwao hai kungehatarisha siri kadhaa.
Wote wawili wakawekwa katika orodha ya wanaopaswa kufa!
Ah.. maskini usilolijua!!
**************
Tuungane wakati ujao!

Post a Comment

0 Comments