Tabia ya mtu mzima inachangiwa kwa kiasi kikubwa na malezi ya utotoni mwake. Wanasaikolojia za watoto wanaeleza kuwa binadamu anajifunza vitu vingi sana katika kipindi cha utotoni kati ya mwaka 1 mpaka miaka 7 pengine kuliko kipindi kingine katika maisha yake hivyo kufanya malezi ya watoto kuwa jambo muhimu sana la kuzingatiwa na wazazi au walezi.
Mamabo anayojifunza katika kipindi hiki ndiyo yanayomtengeneza kuwa vile ambavyo anakuwa katika utu uzima wake. Hivyo basi hiki ni kipindi muhimu sana katika malezi na ukuaji wa mtoto.
Katika kipindi hiki mtoto anajifunza kwa haraka sana. Ni wakati ambao anajifunza kipi ni kizuri na kipi ni kibaya kutokana na jinsi walezi na jamii anayoishi inatafsiri na kufanya.
Inashauriwa katika kipindi hiki watoto kuwa pamoja na wazazi wao kama mazingira yake ni mazuri na yanachangia kujifunza kuzuri kwa mtoto.
Familia ambayo ina upendo na amani inamfundisha mtoto kuwa hivyo. Mtoto anajifunza kupenda kwa sababu anaona upendo katika familia yake,anajifunza kupenda amani na kutengeneza amani kama anaona wazazi wake au ndugu katika familia wanafanya hivyo.
Kinyume chake ni kuwa kama familia inakosa amani na upendo kati yao basi vivyo hivyo inamfundisha mtoto mambo mabaya. Mtoto anajifunza kutopenda au kutojua kupenda na hivyo kumjenga vibaya. Familia za aina hii zinajenga mazingira mabaya kwa mtoto wao.
Familia zilizotengana wakati mwingine zinaleta uafadhali kwa upande mmoja wa kumfanya mtoto asione maisha yasiyo na upendo toka kwa wazazi wake; japo kwa upande mwingine kuna madhara kwa mtoto kwani hatajua umuhimu wa kuwa na mwenza wa maisha.
Watoto wengi ambao wamelelewa na mzazi mmoja au wazazi wakiwa mbalimbali wanapata shida kuishi na wenza katika maisha yao ya ukubwani.
Kwa ujumla ni muhimu sana kwa wazazi kupanga na kutekeleza aina ya malezi ya watoto ambayo yatawafanya wawe na maadili na tabia njema wakiwa watu wazima.
Tabia ya Kuomba.
Kumfundisha mtoto kuomba pale anapohitaji kitu inamfundisha kuwa mnyenyekevu kwa watu wengine hasa anapohitaji msaada.
Inamfundisha pia kuwa kupata kitu kisichokuwa chako inahitaji hiari toka kwa mmiliki. Mtoto ambaye hajui kuomba na kupewa anajengwa katika hatari ya kuwa mnyang’anyi na mbakaji siku za mbele.
Lakini pia kwa kuwa unapoomba kuna matokeo mawili,kukubaliwa au kukataliwa. Mtoto anajifunza hayo na anakuwa tayari kukubali hapana kama mojawapo ya majibu. Mtoto ambaye hajui kukataliwa kila anapoomba ni hatari pia.
Tabia ya Kulilia Vitu.
Tabia hii ni mbaya na ni lazima kwa wazazi kutoiendekeza kwani ina madhara makubwa kwa watoto na hatimaye hata wakiwa watu wazima.
Mtoto anayelilia vitu ni yule ambaye kwanza hajui kuomba na hata akiomba hajui kuwa kuna matokeo mawili,yaani “ndiyo” na “hapana”.
Watoto wanatakiwa kujua kuwa kuna wakati si kila kitu kinapatikana na katika hali hiyo kunahitajika uvumilivu. Kwani hii ndiyo hali halisi ya maisha kwa walio wengi duniani. Lakini pia mtoto anafundishwa kuwa si kila kitu ni kizuri kwake. Mtoto anaweza akalilia bia kama anamwona mama au baba anakunywa, ni vyema akaambiwa na akaelewa kuwa bia hairuhusiwi kwa watoto na hivyo hatapewa.
Kama mtoto yuko katika umri ambao anaweza akaambiwa na akaelewa sababu basi ni vizuri akaambiwa.
Hapana ni muhimu sana kwa mtoto,neno hili linatengeneza mipaka ya mahitaji ya binadamu mtoto. Inasaidia kujenga adabu katika maisha ya utu uzima. Anajenga tabia ya kujizuia vile ambavyo anajua si vyema kwake. Aidha kwa kujifundisha mwenyewe au kwa kuambiwa na wazazi wake au walezi na walimu toka akiwa mtoto.
Tabia ya Kusemea.
Utasikia mtoto anamwabia mama yake baada ya kuadhibiwa “Nitakusemea kwa Baba akirudi”.Hii ni tabia mbaya kwa mtoto. Kwasababu inamtengenezea kuamini kuwa hakutendewa haki na mama yake au mtu mwingine yeyote. Hii ina maana hata kama alifanya kosa hakiri kuwa ni kosa na hivyo ni ngumu kujirekebisha. Falsafa ya madiliko ya tabia inasema kuwa “Kukiri kosa ni nusu ya safari ya kujirekebisha”.
Tabia hii ikemewe kwa mtoto. Mtoto akija kwangu na kesi kama hii huwa namuuliza kwanini alifanyiwa hivyo alivyofanyiwa?. Jaribu kuuliza swali hilo kwa mtoto kila anapoleta kesi ya hivi na sikia majibu yake. Akikuambia sababu,ambayo mara nyingi inakuwa kosa lake mweleze kuwa hilo ni kosa na asirudie tena.
Hapo unampa mafunzo mawili,kwanza umemweleza kuwa amekosa kwa mara nyingine na hivyo kumfanya aamini na kukiri kosa na hivyo kujenga mazingira mazuri kuelekea kujirekebisha. Pili unamfundisha kuwa si kila anapoaadhibiwa anaonewa na akimbilie kuomba msaada.
Pia inamsaidia kujifunza kuwa aliyemwazibu alikuwa sahihi na inamsaidia kumheshimu na kumsikiliza siku za mbele.
Tabia ya Kumpongeza Mtoto na Kumuadhibu.
Pongezi ni muhimu katika kujenga tabia nzuri ya mtoto na hata akiwa mtu mzima kama ambavyo ni muhimu katika kuadhibu.
Mtoto anajifunza kuwa akifanya kitu vizuri au akifanya vitu vizuri anapata zawadi na kinyume chake anaadhibiwa. Hii ni kweli hata katika utu uzima.
Japo pongezi isizidi mipaka na kumuharibu mtoto (soma jinsi pongezi zinvyoharibu watoto) ni vyema mtoto akajua kuwa kunamatokeo chanya na hasi kwenye kila anachokifanya na pale anaposhindwa kufikia malengo basi aongeze bidii zaidi na atafanikiwa.
Pongezi inaweza ikawa ni makofi tu au maneno ya kumtia moyo kama “Hakika wewe ni mtoto mzuri, ninajivunia”. Pongezi zinamfanya mtoto kupenda kufanya vitu vizuri tena siku nyingine.
Adhabu ni muhimu pia,hasa pale ambapo mtoto ameelezwa mara kadhaa na haoneshi mabadiliko yoyote. Adhabu ni kitu hasi chenye nia ya kukuongoza katika njia chanya.
Maisha ya binadamu yanaongozwa na sheria,sheria ziko kila mahali,nyumbani,kazini,barabarani na sehemu nyingine nyingi kwa madhumuni ya kuleta utaratibu fulani wa kuishi. Adhabu inamjenga mtoto kufahamu kuwa kunasheia na ni budi kuzifuata vinginevyo utaingia matatani.
Tabia ya Uchoyo,Ulafi na Ubinfsi.
Unajua mafisadi na majambazi wanatengenezwa wapi? Ni katika familia zetu. Tunamuona mtoto hataki kula na wenzake na ananyang’anya wenzake kile walichonacho hata kama hana kazi navyo na tunakaa kimya. Unategemea nini mtoto huyu akiwa waziri au raisi wa nchi?
Wazazi wanatakiwa kukemea tabia za uchoyo na ulafi kwa watoto. Mfundishe mtoto kucheza,kula na kupeana vitu na wenzake. Mjengee moyo wa kutoa na kuwa na kiasi kwani hivi vina mchango mkubwa katika kumjenga kuwa mtu mzima mwenye haiba.
Kuna msemo kuwa “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo” na hii ni kweli kama ambavyo tumejadili hapo juu. Tusiwalee watoto kwa hisia peke yake,tuweke na misingi mingine itakayotuongoza kuwajenga kuwa watu wazima wenye tabia nzuri.
Mapenzi ya kupitiliza ambayo yanatulevya kiasi kuwa tunachelea kuwakanya watoto wetu itatuletea matokeo mabaya na hatimaye kulaumiwa na kujilaumu wenyewe. Waswahili wanasema “Mchelea mwana kulia hulia yeye” nyingine inasema “ukimchekea nyani,utavuna mabua”.
0 Comments