Faida zitokanazo na kufanya mapenzi salama

Kujamiana (ama tendo la ndoa) ni moja ya mambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Ni ukweli usiofichika kwamba wengi wetu tungependa kuwa na mwenza ambaye mnaridhishana katika tendo la ndoa. Si hivyo tu, bali tendo hili huleta maelewano katika uhusiano wowote ule. Lakini, kuna faida zozote za kiafya za kufanya tendo hili? Ndiyo! Zipo faida kadhaa zinazotokana na kujamiana. Katika makala hii, mwandishi wako Dk. Khamis Hassan anajaribu kutueleza faida za kujamiana kiafya kama ambavyo imewahi kuonekana katika tafiti kadhaa zilizofanyika sehemu mbalimbali duniani.

1. Hulinda mwili dhidi ya magonjwa ya moyo
Wanawake ambao hufika kilele (orgasm) angalau mara mbili kwa wiki kila wanapojamiana, wana uwezekano mdogo sana (30% tu) wa kupata maradhi ya moyo tofauti na wale wasiofikia kilele. Hii ni kwa vile homoni ya endorphin inayotolewa wakati wa kujamiana hupunguza msongo wa mawazo na hivyo kumuepusha mtu na magonjwa wa moyo. Aidha kujamiana angalau mara tatu kwa wiki, husaidia kupunguza uwezekano wa kupata shambulio la moyo (heart attack) na kiharusi.

Uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo wakati wa kufanya mapenzi ni mdogo sana, ni asilimia 1 tu ya vifo vyote vinavyotokana na mshtuko wa moyo ndivyo uhusishwa na kujamiana. Aidha, sababu nyingine inayoongeza uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo ni kuwa na uhusiano nje ya ndoa ambapo huchangia karibu asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na kujamiana, na karibu asilimia 90 ya vifo hivi hutokea kwa wanaume wazee. Uwezekano wa kupata shambulio la moyo wakati wa kujamiana huongezeka ikiwa mtu ana miaka zaidi ya 50, uzito uliopitiliza na matatizo ya afya. Hii ni sawa na kusema unaanza kufanya mazoezi mazito kwa ghafla wakati mwili na umri haviruhusu.

2. Huongeza ukakamavu wa mifupa
Wanawake waliokoma kupata hedhi (menopausal women) ambao pia hujamiana angalau mara mbili kwa wiki wana kiwango kikubwa cha homoni ya  oestrogen mara mbili zaidi ya wale ambao hawajamiani. Homoni hii husaidia kulinda mifupa na kwa wanawake waliokoma kupata hedhi wakosapo homoni hii hupata ugonjwa wa mifupa ujulikanao kama osteoporosis.

3. Hupunguza msongo wa mawazo
Kujamiana hupunguza msongo wa mawazo na shinikizo la damu na humfanya mtu kupata usingizi mnono. Kufikia kilele ni sawa na kunywa 2-3mg za dawa ya diazepam (kumbuka diazepam hufanya mwili kupumzika, muscle relaxant), na hii ndiyo sababu kuu ya kwa nini watu hupata usingizi mzito baada ya kujamiana. Watu wanaojamiana huweza kuhimili vizuri msongo wa mawazo tofauti na wale ambao hawafanyi hivyo. Aidha watu wanaojamiana huwa na kiwango cha kawaida cha shinikizo la damu kuliko wale wasiojamiana. Pia kuwepo kwa viasili vya prostaglandins katika shahawa husaidia kupunguza msongo wa mawazo. Viasili hivi hunyonywa na sehemu za siri za mwanamke. Shahawa pia zina madini ya zinc, calcium, potassium, fructose na protini ambavyo vyote ni muhimu kwa afya njema.

4. Hupunguza maumivu
Kufikia kilele (orgasm) wakati wa kujamiana ni tiba ya maumivu. Homoni ya Oxytocin inayotolewa kwa wingi kabla na wakati wa kujamiana pamoja na viasili vya endorphins hupunguza maumivu ya kichwa, mgongo, kipandauso, baridi yabisi pamoja na dalili zinazotokea baada ya kukoma hedhi (post menopausal syndrome symptom).

5. Hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume
Wanaume walio na umri wa miaka 50 na zaidi na ambao hujamiana mara kwa mara wana uwezekano mdogo wa kupata saratani ya tezi dume (prostate cancer) hali inayotokana na kusafisha tezi dume mara kwa mara wakati wa kujamiana. Aidha kutoa shahawa wakati wa kujamiana mara 21 au zaidi kwa mwezi kunahusishwa na uwezekano mdogo wa kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume wenye umri mkubwa ikilinganishwa na kutoa shahawa mara 4 mpaka 7 kwa mwezi.

6. Huongeza uwezo wa kunusa
Baada ya kujamiana, kiwango cha homoni ya prolactin huongezeka, ambayo hufanya seli za ubongo (brain stem cells) kutengeneza seli mpya katika sehemu inayohusika kunusa  na kutambua harufu (brain olfactory bulb).

7. Hupunguza uzito na kumfanya mtu kuwa na afya njema
Kujamiana ni mazoezi mazuri. Wakati wa kujamiana, mapigo ya moyo huongezeka kutoka wastani 70/dakika mpaka 150/dakika ambayo ni sawa na mtu anayefanya mazoezi kwa kiwango cha juu. Kujamiana huchoma karibu 200 calories sawa na kukimbia dakika 15 katika mashine ya tredmill. Mwanamke anayefika kilele huchoma calories 47 zaidi.

 8. Huongeza kinga ya mwili
Kufanya mapenzi mara moja au mara mbili kwa wiki huongeza kiwango cha seli za kinga aina ya immunoglobulin A kwa robo tatu, na hivyo kumkinga mtu dhidi ya mafua na magonjwa mbalimbali.

9. Kufanya mapenzi huongeza urembo wa mwanamke
Wanawake wanaojamiana angalau mara nne kwa wiki huonekana kuwa na umri mdogo ikilinganishwa na umri wao kwa miaka 7 mpaka 12, hii inatokana na ukweli kuwa kujamiana huongeza homoni ya oestrogen ambayo hufanya nywele za wanawake kuwa na afya nzuri na ngozi zao kung’aa.

10. Kudhibiti mzunguko wa hedhi kuwa wa kawaida
Wanawake ambao hujamiana angalau mara moja kwa wiki (isipokuwa siku ambazo wako kwenye hedhi) huwa na mzunguko wa hedhi wa kawaida ikilinganishwa na wale ambao hufanya mapenzi kwa nadra au wale ambao hawafanyi kabisa.

11. Tendo la ndoa huongeza hali ya kujiamini
Ikiwa litafanyika baina ya wapendao, na tendo lenyewe likawa la furaha na upendo, kujamiana huongeza kujiamini.

12. Kuongeza ukakamavu katika misuli ya nyonga (pelvic floor muscles)
Na hivyo kuzuia mwanamke kupata matatizo ya mkojo au ugonjwa wa kibofu cha mkojo. Wanawake ambao wamekoma kupata hedhi, kufanya mapenzi mara kwa mara huondoa tatizo la kusinyaa kwa sehemu za siri za mwanamke (vagina atrophy) na hivyo kumwepusha na  maambukizi katika njia cha mkojo (Urinary Tract Infection).

13. Kufanya mapenzi huongeza kasi ya mzunguko wa damu mwilini
Unapojamiana na kufikia kilele, mzunguko wa damu huongezeka maradufu, hivyo kuongeza mzunguko wa hewa aina ya oksijeni kwenda kwenye viungo muhimu kama moyo, ubongo na figo hivyo kusaidia kuondoa uchafu na sumu mbalimbali mwilini.

14. Huongeza hali ya kujithamini au kuthamini mwili wako
Hakuna kitu kizuri kama mtu kutambua ana maumbile mazuri na ya kuvutia, haya yote hupatikana wakati mtu yupo uchi wakati wa kujamiana na mwenza wake kumwambia kwamba ana maumbile mazuri na ya kuvutia, hii huongeza hali ya kujithamini na kujipenda kwa binadamu yoyote.

15. Husaidia kuishi kwa muda mrefu
Kufanya mapenzi angalau mara mbili kwa wiki hurefusha maisha yako. Kila unapofikia kilele, homoni aina ya DHEA (Dihydroepiandrosterone) hutolewa kwa wingi kutokana na raha ya tendo na kufikia kilele.  DHEA huongeza kinga ya mwili, hurekebisha tishu zilizoharibika (hutibu vidonda), huongeza kiwango cha ufanyaji kazi cha ubongo, huiweka ngozi kuwa na afya bora na hupunguza msongo wa mawazo. Kwa hiyo, kuongeza kufikia kilele kuna uwezekano wa kurefusha maisha yako.

16. Kujamiana huongeza upendo na msisimko katika mapenzi 
kutokana na kuongezeka kwa homoni ya oxytocin (love hormone), ambayo huleta mshikamano, uaminifu, na unyenyekevu katika uhusiano au kwenye ndoa.

17. Uongeza uwezo wa kuzaa au kutunga mimba
Mara nyingi watu huuliza kama urefu wa uume una uhusiano wowote na uwezo wa kutunga mimba. Jibu zuri ni hapana! Kufanya mapenzi mara kwa mara huboresha shahawa za mwanamume, huzifanya kuwa katika kiwango kizuri, na kama unataka kupata mtoto, ni bora kufanya mapenzi mara kwa mara sio kutumia shahawa zilizokaa kwa muda wa siku nne.

Post a Comment

0 Comments