NI wiki nyingine tunakutana tena kupitia ukurasa huu nikiamini kwamba umzima, bukheri wa afya na unaendelea nyema na maisha yako kama kawaida. Mimi niko poa kabisa tayari kukuletea mada nyingine ambayo naamini itakuwa ni yenye faida kubwa katika maisha yako ya kimapenzi.
Mpenzi msomaji wangu, suala la kuoana si la kukurupuka, ni suala linalotakiwa kuchukua muda ambapo wawili waliotokea kupendana, hupata nafasi ya kuchunguzana katika mambo mbalimbali. Kabla ya kufikia hatua ya kuoana, ni lazima kwanza mtaanza kuwa marafiki wa kawaida. Kipindi hicho ndipo wewe utapata nafasi ya kubaini kama huyo uliye naye anastahili kuwa wako wa maisha. Mkishaona kwamba mmeridhiana kitabia, hapo mnaweza kuingia katika hatua ya uchumba na wakati huo penzi lenu halistahili kuwa la siri tena. Ndugu, jamaa na marafiki wanatakiwa kujua kwamba ninyi ni wanandoa watarajiwa!
Elewa tu kwamba, kama utakutana na mtu kwa mara ya kwanza na akakueleza kwamba anataka kukuoa, atakuwa anakudanganya, na kama huamini baada ya muda mfupi utamsikia akisema; “Lakini siwezi kukuoa mpaka tufanye mapenzi kwanza”, ukimkubalia, ujue basi hutamuona tena.
Ndio gia ambazo wavulana wengi wanatumia kuwarubuni wasichana kwa kuwaahidi kuwaoa ili tu wafanye nao mapenzi.
Kimsingi unapovutiwa na mtu fulani na ukakubali kuanzisha uhusiano naye, jambo la msingi ni kuwa makini sana na nyendo zake katika maisha yenu ya kila siku. Mchunguze kwa undani, je anafaa kuwa mke ama mume wako? Anakufaa au umedondoka katika penzi ambalo sio sahihi?
Isije ikatokea eti kwa sababu mmekuwa wapenzi kwa muda mrefu basi atakapokutamkia kwamba anataka kukuoa basi ukubali tu hata kama umeona kwamba maisha ya ndoa yenu yanaweza kutokuwa ya furaha kutokana na kuwepo kwa migongano ya mara kwa mara pindi mlipokuwa wapenzi wa kawaida.
Wapo wapenzi ambao wanaonekana tu kwamba hata wakija kuoana watakuwa na maisha mazuri. Ni dhahiri kwamba wapenzi ambao wamekaa kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja na haijawahi kutokea kusalitiana, kugombana, kutukanana, kuvunjiana heshima, wapenzi hawa wanaweza kuoana na wakaishi maisha ya raha mustarehe.
Wazungu wana msemo wao unaosema ‘the past gives the light of the future’ wakimaanisha kwamba mambo yaliyopita yanatoa mwanga wa nini kinaweza kutokea katika siku zijazo.Tunajua kwamba wapo ambao watajifanya wanyenyekevu, wapole, wenye mapenzi ya dhati lakini kumbe hamna lolote ni chui walioficha makucha.
Utakuja kushangaa vituko atakavyokuja kukufanyia pindi mtakapokuwa mmeoana, unaweza kusema sio yule aliyekuwa akikuahidi kutokukusaliti wala kukufanyia kitu chochote ambacho kitakuudhi hata siku moja.
Waswahili wanasema nyota njema huonekana asubuhi na kikubwa zaidi unatakiwa kuwa na imani. Amini kwamba huyo uliyempata ambaye unataka awe mwandani wako ndivyo alivyo na ndivyo atakavyokuwa hata mtakapokuja kuoana. Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
0 Comments