HALI hii huwatokea wanaume na wanawake. Ni tatizo linaloathiri uwezo wa kisaikolojia na kimwili wa mtu yeyote aliye katika umri wa kuzaa. Tatizo hili kitaalam huitwa loss of libido au sex drive. Uwepo wa libido na sex drive katika kiwango kilicho bora, ndivyo humsukuma binadamu ashiriki tendo hili. Libido au sex drive hutofautiana kiwango kati ya mtu na mtu.
Wapo wanaume au wanawake wenye kiwango kikubwa na wapo wenye kiwango kidogo na wenye kiwango cha wastani.
Mwanaume mwenye kiwango kidogo cha libido au sex drive, uhisi amepungukiwa nguvu za kiume, kumbe yupo vizuri ila tatizo hana hamu na hisia. Hivyohivyo mwanamke mwenye kiwango kidogo, hulalamika kutokuwa na hamu, msisimko wala hisia za tendo.
Watu wenye viwango vya juu vya libido au sex drive, awe mwanaume au mwanamke huwa hawatulii na hawatosheki, huangaika huku na kule kama ni mwanaume hutamani kila mwanamke anayemuona na kama ni mwanamke hivyohivyo kila mwanaume humuona anafaa.
Ingawa ongezeko hilo wengi huliona zuri kuliko upungufu, lakini ongezeko la libido au sex drive huleta madhara ya kupata magonjwa ya kuambukiza, migogoro ya kimapenzi na hata kuvunjika kwa uhusiano.
Upungufu wake pia huumiza kwani mwanaume hawezi kushiriki tendo la ndoa na mwanamke hupata maumivu wakati wa tendo la ndoa. Kwa ujumla, hisia na hamu ya tendo la ndoa huongozwa na mifumo ya kibaolojia, kisaikolojia na kijamii.
Kibaolojia tunahusisha zaidi vichocheo au homoni, aina nyingine za kemikali zipatikanazo mwilini ziitwazo neurotransmitters, hasa vichocheo vya testosterone na dopamine ambavyo vina kazi kubwa katika utengamano wa libido mwilini mwa binadamu.
Matatizo ya kijamii yanayoathiri hamu na hisia za tendo la ndoa ni majukumu ya kikazi na kifamilia, matatizo ya kisaikolojia ni yote yanayokusibu na kuumiza akili yako, mfano hali ya kujikataa mwenyewe, kukata tamaa na msongo wa mawazo. Haya yote huathiri hamu ya kuwa na tendo la ndoa, hisia au sex drive vinaweza kuathiriwa na uwepo wa magonjwa makali kama kisukari, magonjwa ya moyo, maumivu ya mwili, kansa, HIV, matumizi ya dawa kwa muda mrefu na baadhi ya madawa kama ya moyo, kansa, TB na mengine mengi.
Hali ya maisha na uhusiano kama siyo mzuri pia huathiri katika hamu na hisia za tendo la ndoa.
Umri huathiri hamu na hisia hasa katika kipindi cha balehe; mara nyingi hamu na hisia za kushiriki ngono huongezeka.
Mtu yeyote awe mwanamke au mwanaume mwenye hamu na hisia kubwa za kushiriki ngono, kitaalam huitwa hypersexuality na yule mwenye kiwango kidogo tunaita hyposexuality.
Huwa inatokea mtu akawa na hamu sana ya kuhitaji kushiriki ngono, lakini mazingira hayamruhusu au sheria fulanifulani zinambana kutokana na misingi au taratibu mbalimbali mfano za kidini au kijamii au kimaadili. Basi endapo itatokea atashindwa kujidhibiti au kudhibitiwa na akaipata fursa hiyo, basi huanza kushiriki kwa fujo bila kuangalia anayemfuatilia na kushiriki naye ni mtu wa aina gani. Kwa hiyo, wakati mwingine mtu anaweza kujikuta ametumbukia kwenye dimbwi la ngono bila kujijua alianza vipi, kumbe ni kushindwa kudhibiti hali ya hisia zake na hamu.
Haja na utashi wa kushiriki tendo la kujamiiana au sexual desire miongoni mwa binadamu husaidia kuimarisha maelewano mazuri endapo wawili hao watakuwa na mawasiliano mazuri.
Katika hili, endapo mmojawapo kila mara akiwa hayupo tayari yaani hana haja wala utashi wa kushiriki tendo hili, basi mgogoro mkubwa katika uhusiano utatokea na kuharibu umoja uliopo.
Mawasiliano mabovu katika mapenzi pia huvunja uhusiano na kusababisha matatizo makubwa kutokana na kutojali nini mwenza wako angependa au kupendelea katika mapenzi.
Endapo itatokea mtu hana hamu na hisia za kutosha katika kufanya tendo la ndoa, lakini siku zote haridhishwi na tendo linavyofanyika kutoka kwa mpenzi wake, basi tunasema mtu huyo ana njaa na kiu ya mapenzi ambayo haijakamilishwa hivyo yupo hatarini kupata tatizo liitwalo sexual frustration ambapo anashindwa kumaliza msongo wa mapenzi uliombana.
Mtu mwenye dalili hizi kama ni mwanamke huanza kufuatilia vijana wadogo kwani uhisi watu wazima wenzake ndiyo tatizo, kama ni mwanaume kijana huanza kufuatilia wamama watu wazima kwa kuhisi wasichana au wanawake wa rika lake ni tatizo. Kwa wanaume watu wazima na wazee hufuatilia wasichana wadogo, kwa makundi haya ya watu tunasema tayari wameathirika kimapenzi hawajawahi kuridhishwa, hivyo wapo sexually frustrated.
MATATIZO YA KISAIKOLOJIA
Wanazuoni na wasomi wa kale walishayaona haya tangu awali, mwanazuoni Sigmund Freud alizungumzia libido kuwa ni nguvu kubwa au nishati iliyo ndani ya penzi bila mtu mwenyewe kujifahamu na kujikuta ametumbukia kwenye mapenzi kwa kumpenda na kuwa na hamu kubwa ya kuwa na ampendaye.
Pia mwanazuoni huyo amezungumzia hatua mbalimbali za hamu na hisia za mapenzi na kujamiiana zinavyoanza tangu utotoni.
Itaendelea wiki ijayo.
0 Comments