MUNGU ni mwema! Ni Jumamosi nyingine tumekutana kwenye kilinge chetu cha kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu maisha ya uhusiano.Tupo kwenye kizazi ambacho kina changamoto kubwa sana katika masuala ya uhusiano. Kizazi ambacho kimejaa usaliti, kizazi cha ulaghai na utapeli wa mapenzi. Kizazi ambacho watu wake wengi wamevaa ngozi ya kondoo kumbe ndani ni mbwa mwitu. Sarakasi za uhusiano ndizo zimejengeka kwenye akili za watu kiasi ambacho imefikia watu kutokuwa na imani tena.
Watu wengi sasa hivi hawaamini tena katika mapenzi ya kweli kutokana na magumu waliyopita, wamekata tamaa na wanaona hakuna umuhimu wa kupenda tena kwani uhusiano siyo jambo la kheri tena bali ni la shari.
Mimi na wewe sasa hivi ni mashahidi wa matukio mengi sana ya wapendanao kugombana, watu kupigana na hata wengine kuuana kutokana na sababu mbalimbali zinazohusiana na masuala haya ya uhusiano. Kwenye vyombo vya habari sasa hivi habari za mke kamuua mume au mume kamuua mke siyo ngeni. Zinatokea sana, hii inatokana na jinsi ambavyo watu wanaingia kwenye uhusiano na watu ambao si sahihi au tu hawana hofu ya Mungu.
Marafiki, inatupasa kujifunza hatua mbalimbali za maisha ya uhusiano. Kujua kwamba unataka kuingia kwenye uhusiano, je, ni mtu wa aina gani atakuwa sahihi kwako? Usiingie tu kwenye uhusiano sababu kwamba na wewe unataka kuwa na uhusiano au sijui umechoshwa na kelele za marafiki wanaotaka kumjua mtu wako, lazima umjue vizuri
mwenza wako ana sifa njema? Ni mtu mwenye moyo wa aina gani? Ana hofu ya Mungu? Siyo mkorofi? Hana rekodi za kufanya matukio ya uhalifu au hata ujambazi? Kuna watu wanaingia kwenye uhusiano na mtu hajui hata mwenza wake anafanya shughuli gani.
Yeye anachoangalia ni kupewa mapenzi au fedha za kufanyia starehe, ndugu zangu hii ni hatari. Unaweza kuishi na madhara yake ndiyo haya tunayoyashuhudia kila siku. Unaishi na mtu ambaye kwake kuua siyo tatizo.
Thamani ya binadamu kwake ni kitu cha sekunde moja au mbili tu. Anaweza kukutoa ngeu, anaweza kukujeruhi, anaweza pia kubadilisha jina ndani ya muda mfupi ukatoka kuitwa jina lako ulilopewa na wazazi wako, ukaitwa marehemu.
Ni vizuri sana kuanzisha uhusiano, kuukuza na mtu ambaye ana mwenendo mwema. Hakikisha uliye naye kweli ni mtu ambaye unaweza kumuamini kiasi cha kutosha? Imani kati yenu ipo? Mnaishi kwa upendo wa dhati au mnadanganyana? Ukiliona tatizo kwa mwenzako na ukaona linaweza kuwa na madhara huko mbeleni ni bora kuiahirisha safari.
Mtu unayekwenda kuishi naye lazima uwe na uhakika kwamba kweli anakupenda kwa dhati, ana roho ya huruma, ana ubinadamu? Muishi kweli mkiwa na amani ya moyo, siyo mnaishi kwa kuviziana. Mwanaume anaishi na mwenzake huku akiwa na hofu hata ya kula chakula alichoandaliwa unafikiri hapo kuna maisha? Au mwanamke anaishi akiwa na hofu ya kukatwa panga muda wowote maisha hayo ya kazi gani?
0 Comments