ALIKIBA AFUNGUKA KUHUSU KUACHANA NA MKEWE

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Ali Kiba amesema hajaachana na mkewe bali amemruhusu arejee kwao Kenya kufanya kazi kama alivyomuomba.

Amesema licha ya uamuzi wake huo,  siku za hivi karibuni walikuwa na mgogoro lakini wameumaliza.

Tetesi za kuvunjika kwa ndoa hiyo  zilianza  Julai, 2019 lakini hivi karibuni zilishika kasi zaidi.

Akizungumza  jana Alhamisi Septemba 19, 2019 katika kipindi cha Ala za Roho kinachorushwa na Redio Clouds, Ali Kiba amesema yanayosemwa kuhusu ndoa yake,  yenye ukweli ni asilimia moja tu.

Amesema ukweli huo wa asilimia moja ni kuwa hivi sasa haishi na mkewe, ulitokea mgogoro kati yao lakini wameumaliza.

"Katika kila ndoa hakukosi mgogoro, na kwangu ndivyo ilivyotokea lakini namshukuru Mungu tuliyamaliza na sasa tupo sawa."

"Nawashauri watu wasipende kufurahia kuvunjika kwa ndoa za wenzao kwa kuwa jambo hilo Mungu ndio analiunganisha, " amesema Ali Kiba. .

Amebainisha kuwa amelazimika kutoa ufafanuzi kuhusu ndoa yake kwa kuwa ukimya wake unaweza kuleta athari katika familia yake.

"Mimi ninasafiri  mara kwa mara na mke wangu huwa anabaki mwenyewe. Mara ya mwisho  nilikuwa naenda Ulaya, hakufurahishwa na  akaniuliza ninaonaje akarudi kazini kwa kuwa amesoma na ana vyeti vyake."

" Nikaona isiwe tabu nimruhusu kwani anachoongea kina ukweli. Sasa atakaa tu bila kufanya kazi hadi lini, hivi ninavyoongea yupo kwao Mombasa lakini bado tunawasiliana vizuri tu," amesema msanii huyo.

Ameongeza,  "Hata leo (jana) nimeongea naye na sijawahi kumpa talaka licha ya changamoto zilizotokea hapo katikati."

Post a Comment

0 Comments