USIJIPE PRESHA, KAMA UNAMPENDA KWELI MUAMINI


Ili uweze kudumu katika uhusiano wako unatakiwa kujenga mazingira ya kumuamini sana mpenzi wako. Nasema hivyo kwa kuwa, mapenzi ni imani. Ni sawa na kuamini Mungu yupo licha ya kwamba hujawahi kumuona.

Vivyo hivyo, amini tu kwamba mpenzi wako anakupenda kwa dhati licha ya kwamba hujaufungua moyo wake na kathibitisha kwamba ndani yake uko wewe peke yako.

Mpende, muamini na weka akilini mwako kwamba, kamwe hawezi kukusaliti licha ya kwamba kinyume chake pia ni sawa. Hiyo itakusaidia wewe kuendelea kuishi maisha ya furaha na amani bila kuwa na presha.

Jiulize, ni wanaume wangapi ambao wake zao wanagawa penzi nje ya ndoa lakini wao wanawaamini kupita maelezo?

Ni wanawake wangapi ambao waume zao ni viwembe kwelikweli lakini wanawaamini kupindukia? Unadhani ni kwa nini?

Ni kwa sababu wamejijengea mazingira ya kuwaamini wenzao wao wa kiwango kikubwa na kuziba masikio yao kukwepa wambeya.

Tutambue tu kwamba, katika maisha kuna kitu kuridhika. Unapokuwa na mtu ambaye anakupa kila aina ya furaha maishani mwako bila kuonesha tabia zozote zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, huyo mpende, mheshimu na muamini.

Hata kama kuna uwezekano wa yeye kuwa anaficha makucha yake na kuyachomoa pale anapokuwa mbali na wewe, kwa sababu huna uhakika na hujawahi kumuona, chukulia kwamba yeye ni msafi kisha yaache maisha yenu yaendelee kuwepo.

Nasema hivyo kwa sababu, tukianza kuchunguzana hakuna ambaye ni msafi kwa asilimia mia moja.

Kila mtu anajiamini mwenyewe lakini huwezi kuiamini nafsi ya mwenzako kwa asilimia zote.
Ndiyo maana nikasema, unapoingia katika uhusiano na mtu ambaye umetokea kumpenda sana, ongea na moyo wako.

Moyo wako ndiyo utakueleza kama mpenzi wako ni muaminifu ama siyo na pindi utakapoona dalili za kwamba ni tapeli wa mapenzi mwenye lengo la kutaka kukuchezea kisha kukuacha solemba, usimng’ang’anie eti tu kwa sababu umeoza kwake, muache!

Tatizo tulilonalo wengi ni kutokuwa tayari kuwakosa wale ambao tumetokea kuwapenda sana bila kujua kwamba unaweza kutokea kumpenda mtu lakini yeye akawa hana mapenzi ya dhati moyoni mwake dhidi yako.

Ifike wakati tukubaliane na uhalisia kwamba, unapoona uliyenaye anakuzingua, yupo mwingine mwenye penzi la dhati kwako ambaye anasubiri umuache huyo uliyenaye ili awekeze penzi lake kwako.

Kwa kumalizia naomba niseme kwamba, mapenzi ya siku hizi usipoangalia yanaweza kukufanya ukawa chizi.

Hii ndiyo inayosababisha baadhi ya watu kufikia hatua ya kusema kwamba, hawahitaji kuwa na wapenzi katika maisha yao. Kwa nini? Kwa sababu kila uhusiano wanaoingia wanakutana na usanii.

Elewa kwamba, una haki ya kupenda na kupendwa, ukishampata yule unayedhani atayafanya maisha yako kuwa ya furaha, mpende kwa dhati na muamini kwamba hawezi kukusaliti lakini, wakati huo hutakiwi kubweteka, chunguza nyendo zake na kama utabaini kwamba anajiheshimu, ongeza mapenzi kwake lakini kama utabaini kuwa hajatulia, muache.

Post a Comment

0 Comments