Twin Soul flame; tatizo sugu linalowatesa wapenzi wengi



NIjumaa nyingine nzuri, karibu jamvini! Mada niliyoanza kukufafanulia wiki iliyopita, ni kuhusu kitu kiitwacho Twin Soul Flame, yawezekana maneno haya ya Kingereza yakawa mageni kwako au pengine yakakufanya usielewe kwa urahisi maana yake!  Nilijaribu kukufafanulia kwa mifano kile ninachokimaanisha ambacho siyo kitu kigeni kabisa, kinawakuta watu wengi na pengine hata wewe ni miongoni mwa wanaoishi kwenye hili tatizo sugu la twin soul flame.
Unampenda sana mtu fulani, anapokuwa karibu na wewe unajihisi amani kubwa ndani ya moyo wako, unajihisi kukamilika, unaiona dunia kuwa tamu kwelikweli, lakini mapenzi yenu hayadumu kwa muda mrefu! Ikiibuka mitafaruku kati yenu inakuwa mikubwa kwelikweli na mwisho kila mmoja anaamua kuchukua hamsini zake.
Akiondoka unajihisi upweke wa hali ya juu mno, unajaribu kuwa na mtu mwingine, lakini unaona kama hafiti, unammisi sana, unateseka moyoni, unaumia na mwisho unaamua kumtafuta tena, mnaendelea na uhusiano wenu, baadaye mnaachana tena! Mzunguko unaendelea hivyohivyo katika maisha yenu yote.
Bila shaka sasa umenielewa, hali hii ndiyo inayoitwa ‘twin soul flame’. Wasichokijua watu wengi, ni kwamba uhusiano huu wa kimapenzi, huwa siyo uhusiano wa kawaida, kuna kitu fulani kinachohusiana na roho kinakuwa kimehusika kuwaunganisha.
Pengine umeshawahi kuwa na uhusiano na watu kadhaa, kama wewe ni mwanaume, ushawahi kuwa katika uhusiano na wanawake kadhaa na wewe kama ni mwanamke si ajabu umeshawahi kuwa kwenye uhusiano na watu kadhaa, lakini unapokutana na ‘twin soul flame’, mambo yote hubadilika kabisa.
Utajuaje kama huyo uliyekutana naye ndiye nusu ya pili ya roho yako? Kitaalam inaelezwa kwamba, hatua ya kwanza kabisa, unapokutana na mtu wa aina hii, hata kama ndiyo kwanza mnaonana, hatakuwa mgeni kwenye nafsi yako!
Utahisi kama pengine ulikuwa unamfahamu siku nyingi zilizopita na yeye atahisi hali hiyohiyo! Mtajikuta wote wawili mkivutana kama sumaku na hakuna ambaye ataweza kujizuia kwa mwenzake, mtajikuta tayari mmeshakuwa wapenzi, katika mazingira ambayo hayaelezeki.
Kitu kingine, mkishaanza kuwa karibu, utagundua kwamba mnafanana vitu vingi sana, kuanzia tabia, hobi na mambo mengine chungu nzima, lakini pia utagundua kwamba mnaanza kugongana maneno ya kuzungumza mara kwa mara, ulitaka kusema jambo fulani, lakini na yeye wakati huohuo akawa anataka kuzungumza jambo hilohilo, mwisho mnajikuta mkitamka neno moja kwa pamoja!
Hii maana yake ni kwamba akili zenu zinafanya kazi kwa kasi inayoendana, unachofikiri ndicho anachokifikiria! Na hii itakuwa inatokea mara kwa mara!
Kitu kingine, kitakuwa ni wewe kumuota mwenzi wako mara kwa mara na yeye kukuota mara kwa mara mkiwa mmelala! Hii nayo itakuwa inatokea mara kwa mara katika maisha yenu, yaani mnajikuta mmekuwa ni kama kitu kimoja!
Unaweza kuwasiliana na mwenzi wako bila hata kuzungumza, unaweza kumtazama tu akawa ameshaelewa unataka kusema nini na yeye akikutazama tu unaelewa alitaka kusema nini. Yote tisa, kumi ni kwamba mnapokutana faragha na mtu wa aina hii, hisia zenu zinapaa juu mno, yaani unajikuta ni kama unaishi kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.


Swali la kujiuliza, ni kwa nini watu wa aina hii, mapenzi yao huwa hayadumu? Kwa nini uhusiano wao unatawaliwa na migogoro ya mara kwa mara? Usikose sehemu ya mwisho wiki ijayo ambapo nitakueleza mbinu za kufanya unapogundua upo kwenye aina hii ya uhusiano.

Post a Comment

0 Comments